Rais Jakaya Kikwete na mgeni wake, Rais Hu Jintao wakifungua pazia kuashiria kuuzindua rasmi Uwanja wa taifa jijini Dar es salaam uliojengwa kwa msaada wa Serikali ya China. |
Exuper Kachenje na mashirika ya habari
WAKATI mgogoro wa kiuchumi ukiyasumbua mataifa makubwa na madogo duniani, Rais Hu Jintao wa China amesema nchi yake itaimarisha mawasiliano na ushirikiano wa karibu na Tanzania na nchi nyingine za Afrika, kwa lengo la kupunguza athari za mgogoro huo, huku akitangaza msaada wa kifedha, kielimu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, Rais Hu, ambaye uchumi wa taifa lake unakua kwa kasi tofauti na uchumi wa mataifa ya Magharibi, aliitoa hofu Tanzania dhidi ya mgogoro huo wa kifedha na kiuchumi unaoisumbua dunia kwa sasa.
"China inapenda kuwaeleza kuwa itaimarisha mawasiliano na uratibu na Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kwa mwelekeo wa kupunguza athari za mgogoro huo wa kiuchumi," alisema.
Jintao alisema taifa lake litachukua mtazamo mpana, wenye uwiano, endelevu na unaotekelezeka katika kuweza kubadilisha mfumo wa fedha wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuongeza uwakilishi wa mataifa ya kiafrika na yale yanayoendelea pamoja na sauti zao katika mabadiliko hayo.
"China itatekeleza ahadi yake ya kutopunguza msaada wake kwa Afrika na kuishawishi jumuiya ya kimataifa kuheshimu ahadi zao kwa bara hili,"alisema Jintao akirejea mwelekeo wa mataifa mengi makubwa, kufikiria kupunguza misaada yao kwa nchi zinazoendelea kutokana na matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyozikumba nchi hizo.
Mbali na mataifa hayo kufikiria kupunguza misaada yao kwa nchi changa, miradi mingi ya uwekezaji inaweza kupungua kutokana na msukosuko wa kifedha, hali kadhalika kupungua kwa idadi ya watalii ambao huziingizia nchi changa, hasa za Afrika mashariki fedha nyingi.
Lakini Jintao alisema matatizo hayo hayataifanya China ifikirie upya uhusiano wake na nchi hizo na badala yake itaendeleza mikakati yake barani Afrika na kutimiza ahadi zake.
Rais Jintao alikabidhi msaada wa Yuan 150 milioni sawa na zaidi ya Sh28 bilioni kusaidia Tanzania wakati huu ambao nchi mbalimbali duniani zimekumbwa na tatizo la kuyumba kwa uchumi.
Katika sherehe, iliyopambwa na matarumbeta, Rais Jintao aliahidi Yuan 120 milioni kwa ajili ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Yuan 30 milioni kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Rais Jintao alitia saini mikataba ya kiuchumi na Rais Kikwete, ukiwamo ule wa Tanzania na benki kubwa ya Exima ya China utakaotoa mikopo kwa miradi ambayo bado haijawekwa wazi.
Zaidi ya kampuni kubwa 40 zimewekeza Tanzania. Kwa mwaka 2007 peke yake, biashara kati ya mataifa hayo mawili ilikuwa kwa asilimia 48 na kufikia Dola 800 milioni za Kimarekani (sawa na karibu Sh1 trilioni).
Katika miaka ya sabini, China ilisaidia ujenzi wa reli inayoziunganisha Tanzania na Zambia. Hivi karibuni ilijenga uwanja wa kimataifa wa michezo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 waliokaa, ukiwa umegharimu zaidi ya Sh53 bilioni. Rais Jintao alizindua uwanja huo jana na umepewa jina la Uwanja wa Taifa.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayofaidika sana na misaada ya China na mataifa hayo yana uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 1964. Mwaka jana Tanzania ilikuwa taifa pekee lililokuwa mwenyeji wa mwenge wa Olimpiki kabla ya Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Beijing.
Awali Jintao alisema kwamba mbali ya mabadiliko yanayoikumba dunia katika nyanja mbalimbali, uhusiano na urafiki baina ya nchi hizo ulioanzishwa mwaka 1964, umeendelea kukua na kuneemeka.
Aliongeza kuwa uhusiano huo wa dhati na wa kujivunia unaonyesha mfano wa mshikamano na ushirikiano kati ya China na bara la Afrika na kati ya nchi mbili hizo katika nyanja mbalimbali.
Naye Rais Jakaya Kikwete alisema Tanzania na China zimenufaika kutokana na uhusiano baina ya nchi hizo, ulioanzishwa na viongozi watangulizi na kwamba, Tanzania itaendeleza uhusiano huo wa kipekee na China ili kujenga mshikamano zaidi.
Katika mazungumzo hayo yaliyochukua saa moja Ikulu, Rais Jintao alisema China na Tanzania zimeonyesha mtazamo mpya katika miaka ya karibuni, hasa kwenye kuaminiana kisiasa na ushirikiano katika viwanda, biashara na utamaduni na kwamba ipo haja ya kuongeza nguvu ya ushirikiano katika nyanja hizo, elimu pamoja na afya .
Akiwa katika ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini Tanzania Rais, Hu Jintao alipigiwa mizinga 21 kabla ya kukagua gwaride lililoandaliwa maalumu kwa ajili yake na vikosi vya ulinzi na usalama, pamoja na kuangalia ngoma za kiasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Ikiwa ni ziara yake ya pili barani Afrika, rais huyo alitaja mambo mbalimbali yatakayokuza ushirikiano kati ya China na bara hilo kuwa ni pamoja na kupunguza ushuru na kodi, kuzipunguzia madeni nchi za Afrika na kuziongezea misaada nchi za Afrika katika miaka mitatu ijayo
Alibainisha kuwa nchi yake itawaalika vijana wa Kitanzania kutembelea nchi yake na kwamba, itaongeza nafasi za masomo (scolarship) kwa vijana wa Tanzania. Rais Kikwete aliishukuru China kwa misaada yake katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu.
Alisema kuwa Tanzania inapenda kufanya kazi na China ili kudumisha uhusiano uliopo na kwamba, itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo katika sera na juhudi zake za kuheshimu mipaka.
Baada ya mkutano baina ya viongozi hao mikataba mbalimbali imetiwa saini kati ya nchi hizo ambapo pia Jumamosi baada ya kuwasili nchini, Rais Hu Jintao alikutana na Rais Amani Abeid Karume na kuzungumza naye.
Katika mazungumzo hayo, Rais Hu alisema nchi yake itaimarisha na kuongeza kiwango cha ushirikiano wa kibiashara baina ya China na Zanzibar ili kukuza uchumi wa Zanzibar.
Rais Jakaya Kikwete na mgeni wake, Rais Hu Jintao wakifungua pazia kuashiria kuuzindua rasmi Uwanja wa taifa jijini Dar es salaam uliojengwa kwa msaada wa Serikali ya China.
0 comments