MIVUTANO ya makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajia kufanikisha jitihada za Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhitimisha vyema mpango wake wa kuongeza idadi ya wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CHADEMA imejipanga kujiimarisha zaidi katika ngazi ya ubunge kutokana na kile kinachobainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, chama chenye wabunge wengi ndicho kinachounda Serikali.
Na kutokana na masharti hayo ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kutoka chama kingine na kile kitakachounda Serikali, yaani chenye wabunge wengi.
Mwenendo wa kisiasa nchini unabainisha kuwa nguvu za chama hicho zimeongezeka na msingi wa ongezeko hilo ni utendaji wa wabunge wa chama hicho ndani ya Bunge, na tayari katika baadhi ya majimbo ambako chama hicho hakina wabunge dalili zinaonyesha mafaniko.
Kutokana na hali hiyo, taarifa zaidi zinabainisha kuwa huenda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akaingia katika kinyang’anyiro cha ubunge na hivyo kutorejea katika kinyang’anyiro cha urais, kama ilivyokuwa mwaka 2005.
Taarifa hizo zinaendelea kubainisha kuwa uamuzi wa chama hicho kuwa na mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu mwakani utaegemea zaidi Katiba ya chama hicho.
Katiba ya chama hicho inatoa fursa kwa mwanachama yeyote wa chama hicho kugombea nafasi ya urais. Hata hivyo, mbali na uwezekano wa chama hicho kuteua mgombea mwingine wa urais badala ya Mbowe, fursa nyingine iliyokuwapo ni kuunga mkono mgombea urais wa chama kingine cha upinzani.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, Mbowe aligombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, baada ya kuamua kutotetea nafasi yake ya ubunge. Mbowe alikuwa mbunge wa Hai na alikuwa kati ya wabunge machachari katika Bunge lililokuwa chini ya Spika, Pius Msekwa.
Taarifa zilizotufikia zinabainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa makundi yanayovutana CCM na hususan ngazi ya majimbo ya uchaguzi wa wabunge kuinufaisha CHADEMA.
Uchunguzi wetu unabainisha kuwa takriban katika kila mikoa na hata katika majimbo mengi ya uchaguzi Tanzania Bara, CCM imegawanyika katika makundi kama ilivyokuwa katika Jimbo la Uchaguzi la Tarime.
Katika Jimbo la Tarime, CCM iligawanyika katika kambi mbili zilizokuwa zikiongozwa na Christopher Gachuma na Kisiery Chambiri.
Kutokana na mgawanyiko huo na kutokana na ukweli kwamba CCM ilihitaji mgombea mmoja kutoka kundi mojawapo, kambi ambayo ilishindwa kutoa mgombea ilitoa ushirikiano kwa mgombea wa CHADEMA.
Hali hiyo ya mgawanyiko Tarime ndiyo iliyopo katika baadhi ya majimbo, ambayo ni pamoja na Vunjo, ambalo kwa sasa mbunge wake ni Aloyce`Kimaro.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa msimamo wa Kimaro katika vita dhidi ya ufisadi ndiyo chanzo cha kuibuka kwa kundi linalompinga. Kimaro amekuwa mstari wa mbele kushinikiza hatua zichukuliwe dhidi ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa au yeye mwenyewe (Mkapa) atoe maelezo kwa umma kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Kutokana na msimamo huo, inaelezwa kuwa wameibuka baadhi ya wana-CCM wanaomkingia kifua Mkapa, ambao pia wamejipanga kwa kushirikiana na mitandao mingine ndani ya CCM kumng’oa mbunge huyo.
Mbali na Vunjo, majimbo mengine ambayo CCM haiko salama ni pamoja na baadhi yaliyomo mkoani Mbeya, ikielezwa kuwa baadhi ya kambi ndani ya CCM zimeandaa wagombea watakaochuana na wabunge wa CCM kwa tiketi ya chama hicho katika kura za maoni.
Majimbo mengine ambayo wabunge wa sasa wa CCM wameandaliwa wapinzani kutoka katika makundi pinzani ndani ya chama hicho ni pamoja na Nzega mkoani Tabora, ambalo Mbunge wake ni Lucas Selelii, Lupa mkoani Mbeya, ambalo mbunge wake ni Victor Mwambalaswa, ambako taarifa zinabainisha kuwa huenda mbunge wa zamani wa Jimbo hilo, Njelu Kasaka, akajitokeza kumpinga.
Lakini mbali na makundi hayo, baadhi ya majimbo ambayo CHADEMA inatarajiwa kutoa ushindani ni pamoja na Mbeya Vijijini, ambako mbunge wake wa sasa Luckson Mwanjale alipata ushindi wa asilimia 35 ya waliopaswa kupiga kura.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Freeman Mbowe huenda akaenda kugombea ubunge katika jimbo lake la zamani la Hai ambalo kwa sasa mbunge wake ni Fuya Kimbita.
Mkurugenzi wa masuala ya Bunge Halmashauri wa CHADEMA, John Mrema, kuhusu uwezekano wa Mbowe kuwania ubunge pamoja na mikakati ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
Mkurugenzi wa masuala ya Bunge Halmashauri wa CHADEMA, John Mrema
‘‘Ni mapema mno kusema kuwa Mwenyekiti wetu (Mbowe) atakwenda kugombea ubunge na kutogombea urais. CHADEMA ni chama kinachofuata demokrasia wagombea huchukua fomu na kupitishwa na mkutano mkuu. Hatua hizo zote bado hazijafikiwa,’’ alisema Mrema, ambaye naye taarifa zinabainisha kuwa huenda akagombea ubunge katika jimbo mojawapo mkoani Kilimanjaro.
Lakini mbali na kutokuwa muwazi katika suala hilo, Mrema alisema Operesheni Sangara imekifanya chama hicho kutambua nafasi na nguvu zake ndani ya jamii ya Watanzania.
‘‘Ipo mikoa ambayo tuna uhakika wa kuongeza idadi ya wabunge. Kwa mfano, mkoani Mara tunataraji kutwaa majimbo saba. Na mikoa mingine tunayotarajia kupata wabunge ni pamoja na Dar es Salaam, Mwanza.’’
Alisema mikoa ya Kigoma, Kilimanjaro, Arusha na baadhi ya mikoa mingine idadi ya wabunge wa chama hicho wanataraji itaongezeka kutokana na mwitikio wa wananchi kuhusu utendaji wa chama hicho.
Taarifa nyingine zilizotufikia zinabainisha kuwa hivi karibuni taasisi moja ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilifanya utafiti katika majimbo 10 nchini ili kubaini kama wabunge wa sasa wanaweza kung’olewa au la.
Baadhi ya majimbo yaliyohusishwa na utafiti wa taasisi hiyo ni pamoja na Karatu, ambalo Mbunge wake ni Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA), Kigoma Kaskazini-Kabwe Zitto (CHADEMA), Urambo Mashariki-Samuel Sitta (CCM), Mbozi Mashariki-Godfrey Zambi (CCM), Simanjiro-Christopher ole Sendeka (CCM), Mpanda Kati-Saidi Arfi (CHADEMA) na Moshi Mjini-Philemon Ndesamburo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, baadhi ya majimbo imebainika kuwa ni vigumu kuwang’oa wabunge wa sasa kwa kura kupitia uchaguzi huru na wa haki.
Utafiti katika majimbo hayo unaelezwa kulenga kusaidia kundi fulani katika siasa kutokana na kuonekana dhahiri kuyahusu majimbo yenye wabunge wanaokera baadhi ya wanasiasa, hususan wale wanaoguswa na tuhuma mbalimbali za ufisadi zilizoanikwa hadharani katika miaka ya karibuni.
0 comments