Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dokta Wilbroad Slaa yuko katika mashaka makubwa kufuatia kitendo cha watu wasiofahamika, kuingia kwenye chumba cha hoteli anayoishi mjini hapa na kutegesha mitambo inayosadikiwa kuwa ni ya kunasa mazungumzo yake. Taarifa zilizothibitishwa na Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Bw. Salum Msangi zimedai kuwa, jana mishale ya saa 5:00 usiku, kitu kimoja cheusi kilikutwa kwenye chaga ya kitanda cha mbunge huyo wa Karatu. Amesema mbunge huyo amefikia kwenye chumba namba 201 kilicho ghorofa ya kwanza ya hoteli ya Fifty Six. Licha ya Dk. Slaa, afande Msangi amesema kuwa kifaa kama hicho pia kimekutwa kwenye chaga ya kitanda cha mbunge wa Konde (CUF), Dk.Taarab Ali Taarab, ambaye naye amefikia chumba namba 202 kwenye hoteli hiyo hiyo. Gazeti hili ambalo liilifika eneo la tukio kiasi cha dakika 15 baada ya polisi kuwasili mahala hapo, lilikuta maafisa kadhaa wa polisi kutoka kitengo cha upelelezi mkoa wakifanya uchunguzi wao. Walionekana wakimhoji Dk. Slaa ambaye alikuwa na wabunge wenzake wa upinzani, wakiwemo Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), Halima Mdee (Viti Maalum), John Mwera (Tarime) na Grace Kihwelu (Viti Maalum). Mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dodoma (RCO), Salum Msangi, amesema ni kweli polisi wamekuta kifaa cheusi kikiwa kimenatishwa kwenye chaga chini ya godoro la kitanda cha Dk. Slaa, ndani ya chumba chumba namba 201. ``Kifaa hivyo tulikuta kinatoa mwanga mwekundu kama kimulimuli…pia kifaa kama hicho tulikikuta sehemu inayofanana na hiyo kwenye kitanda cha Mheshimiwa Dk.Taarab Ali Taarab (CUF), chumba namba 202,`` alisema. Akieleza zaidi tukio hilo, afande Msangi amesema kuwa baada ya kupelekewa taarifa mishale ya saa 5:00 usiku wa Alhamisi, walifika hotelini hapo na kufanya uchunguzi ili kujua kifaa hicho ni cha aina gani. ``Hadi sasa bado hatujajua ni kitu gani hasa... lakini uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuwa si bomu,`` akasema. ``Tunachukua vitu hivi na tutavipeleka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi,`` akasema mkuu huyo wa upelelezi. Pia aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi wanakamilisha kazi ya uchunguzi na mahojiano kwenye mishale ya 7:45 usiku, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi wa polisi utaanza mara moja. Katika hatua nyingine, afande Msangi amesema kuwa polisi imechukua chupa yenye mvinyo, ambayo inadaiwa kufikishwa mapokezi na mtu asiyejulikana aliyedai ni mzigo wa Dk. Slaa. Amesema juzi, mtu aliyejitambulisha kuwa ni mgeni wa Dk. Slaa, aliacha mzigo huo aliodai kuwa amemletea kama zawadi. ``Pia chupa hii yenye mvinyo tumeikuta ikiwa na vijitundu vidogo kwenye mfuniko... tumeichukua na tutaipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili afanye uchunguzi wa kimaabara na kujua kama kulikuwa na kitu chochote cha kudhuru,`` akasema. Akizungumzia tukio hilo, Dk. Slaa amesema jana asubuhi wakati akishiriki mkutano wa wabunge na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Beno Ndulu, alipigiwa simu na mtu mmoja, aliyemtahadharisha kuwa kuna kitu kimefungwa ndani ya chumba chake na kwamba akifika chumbani humo, awe makini. Hata hivyo, Dk. Slaa anasema hakuipa uzito sana taarifa ya mtu huyo ambaye hakumtaja jina ingawa wanafahamiana na hivyo akaendelea na kikao hicho. ``Lakini nilipofika kwenye chumba changu, kabla ya kulala nikaanza kupekua huku na huko... kweli nilikuta kifaa kidogo cheusi kikiwa kimenasishwa kwenye chaga, chini ya godoro. Baada ya kuona hivyo, nilikwenda chumba cha jirani yangu ambako ni kwa Mheshimiwa Dk.Taarab na kumjulisha. Naye kwa tahadhari, akaanza kupekua na akakuta kitu kama hicho,`` akasema. Akasema baada ya kuona hivyo, alimpigia simu Katibu wa Bunge, Dk. Kashilila, ili kumjulisha juu ya tukio hilo. Akasema kuwa naye (Dk. Kashilila), kwa haraka akaagiza Afisa Usalama wa Bunge kufika eneo hilo . ``Baada ya muda walifika polisi na tukawaonyesha... na wao wakachunguza kabla ya kuvinasua vitu hivyo,`` akasema Dk. Slaa mbele ya waandishi wa habari, maafisa wa polisi na wabunge wengine. Mbunge huyo ambaye mara kadhaa amesimama kidete kufichua uovu mbalimbali Serikalini, alisema yeye bado yuko imara na hatishiki na hali iliyomkuta, kwani sio mara ya kwanza kukumbwa na mambo yanayoashiria kumtishia maisha. Amesema yeye ana imani na jeshi la polisi na ana uhakika kuwa uchunguzi wao, utatoa picha halisi ya kwamba kifaa hicho kiliwekwa kwa malengo gani. ``Nilipata kusikia huko nyuma kuwa watu wanaweza kufungiwa vifaa vya kunasa sauti kwa siri, sasa siwezi kujua kama kweli kifaa hiki nacho kiliwekwa kwa malengo hayo,`` akasema mbunge huyo. Akielezea kuhusu kutumiwa mvinyo unaodhaniwa kuwa na sumu, mbunge huyo amesema juzi Februari 4, alipotoka bungeni, alifika mapokezi hotelini hapo na kuelezwa na mhudumu kuwa kuna mzigo wake ameletewa na ndugu yake. Akasema alipouona na kuufungua ili kujua ni mzigo gani, akakuta ni chupa ya mvinyo, lakini kilichomshangaza ni kukuta chupa hiyo ikiwa na vijitundu vidogo na ndipo hapo akawaambia wahudumu waendelee kuitunza. ``Sasa leo nilipokutana na mambo haya, nikawaeleza wahudumu wanipatie na ile chupa ili niwakabidhi polisi kwa sababu vitu hivi vinatia shaka,`` akaongeza. Kwa upande wake, mbunge wa Konde, Dk.Taarab Ali Taarab, yeye alisema baada ya kuingia chumbani kwake, kamwe hakuwa na taarifa yoyote juu ya vitu alivyowekewa. Akasema alikuja kustuka pale alipogongewa na mbunge mwenzake na kuelezwa juu ya kilichojiri chumbani kwake, hivyo akaamua kuchukua tahadhari kwa kupekua na ndipo alipokuta na yeye kawekewa kifaa kama hicho.
0 comments