Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wanafunzi UDSM kizimbani

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WANAFUNZI watano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shitaka la kufanya mkusanyiko usio halali.

Wanafunzi hao ni Anthony Machibya, Owawa Juma, Sabinian Pius, Titus Ndula na Paul Issa.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela mbele ya hakimu mkazi, Victoria Nongwa kuwa wanafunzi hao walitenda kosa hilo Januari 19 mwaka huu saa 3:45 asubuhi katika maeneo ya chuo hicho.

Ilidaiwa wanafunzi hao walibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali ambao ulikuwa umejielekeza kuleta hasira na kujenga chuki kwa watu wengine.

Baadhi ya ujumbe uliokuwemo katika mabango hayo ni, "Nyerere angefufuka leo angelia machozi ya damu", "Kweli Kikwete umesahahu umaskini wa Watanzania wako", "Hivi Pinda wewe ni mtoto wa mkulima", "Wazazi wetu tuoneeni huruma tunateseka jamani" na "Vyuo vya uma vimeuzwa kwa matajiri".

Hata hivyo, wanafunzi hao walikana shitaka hilo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika. Kenyela aliwasilisha maombi kupinga dhamana kwa washitakiwa.

Maombi hayo yaliungwa mkono na hati ya kiapo, ambapo Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa mkoa wa Kinondoni, Koka Moita alidai kuwa washitakiwa wakiachiwa watavuruga zoezi la udahili linaloendelea chuo kikuu.

Moita alidai pia kuwa ana taarifa za kuaminika kwamba mshitakiwa wa pili ameandaa maandamano nchi nzima yanayotarajiwa kufanyika Januari 24, mwaka huu wakati hajatoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika na masuala ya ulinzi.

Wakili wa upande wa utetezi, Flugency Massawe alipinga hoja hizo kwa madai kuwa makosa yote wanashitakiwa nayo washitakiwa yanastahili dhamana na kwamba, hakuna kiapo kinachoendana na kosa la washitakiwa.

"Mahakama haifanyi kazi kwa hisia chuo kimefungwa kwa muda mrefu na hakuna chochote kilichofanywa na washitakiwa wakati huo," alisema Massawe.

Baada ya kusikiliza hoja zote hakimu Nongwa alitupilia mbali hoja za upande wa mashitaka kwa kuwa washitakiwa bado ni watuhumiwa, hadi mahakama itakapothibitisha kosa lao.

Hakimu Nongwa alitoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa akiwataka kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa serikali atakayesaini dhamana ya Sh 500,000.

Nongwa alisema washitakiwa pia hawaruhusiwi kwenda kwenye maeneo ya chuo kikuu bila ruhusa ya mahakama na hawaruhusiwi kufanya mikutano bila ruhusa kutoka mamlaka husika na watatakiwa kuripoti kituo cha polisi Oysterbay kila Ijumaa asubuhi.

Washitakiwa hao walirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 5 mwaka huu itakapotajwa tena.

Huku hayo yakiendelea Tumsifu Sanga anaripoti kuwa Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam, Suleiman Kova alisema hatatoa kibali cha kuandamana kwa wanafuzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam mpaka atakapopata uhakika wa hali ya usalama barabarani kwa siku hiyo.

Kamanda Kova alisema Jeshi lake limepokea barua ya wanafunzi hao ikilitaka jeshi la polisi kutoa ulinzi siku ya Jumamosi katika maandamano ya wanafunzi hao kupinga sera ya uchangiaji wa elimu ya juu ombi lao litafanyiwa kazi kwa muda wa masaa 48 na uwezekano wa kukataliwa ama kukubaliwa upo na si kuhusiana na maandamano kwa kuwa hawakuomba kibali cha kuandamana.

"Jeshi la polisi lina taratibu zake wao waliomba kupewa ulinzi hawakuomba kibali cha kufanya maandamano, hivyo tunatarajia kujadili barua yao ya kuomba ulizni na si maandamano kwa kuwa barua yao tumeipata na tunaifanyia kazi ndani ya masaa 48 na tutawapa jibu la barua yao kulingana na hali ya usalama itakavyokuwa siku hiyo," alisema Kamanda Kova.

Wakati huo huo, Hussein Issa na Patricia Kimelemeta wanaripoti kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimekiri kuwa sera ya uchangiaji wa elimu kwa vyuo vikuu nchini ina upungufu ambao yanahitaji kufanyiwa marekebisho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Makamu wa Chuo anayeshughulikia utawala, Profesa Yunus Mgaya alisema kuwa wanachosubiri wao ni kuona kuwa Waziri Maghembe anaiwasilisha bungeni ili ijadiliwa na kupitishwa.

"Kweli tumeona mapungufu yapo, tumeunda tume ambayo iko chini ya Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kwa ajili ya kukusanya maoni na kuikabidhi kwa waziri ili aweze kuifikisha bungeni kufanyiwa marekebisho,"alisema Profesa Mgaya.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, wanafunzi walipaswa kuwa na uvumilivu ili wajue uamuzi wa bungeni ambalo ndile lenye mamlaka ya kubadili sera.

Alisema kubainika kwa tatizo hilo kulitokana na fomu mbili za wanafunzi mapacha ambao wanalipiwa na mzazi mmoja huku kila mwanafunzi akiwa na daraja lake la malipo. Mmoja alikuwa analipiwa daraja A na mwingine C, hivyo kusababisha mkanganyiko baina ya wanafunzi hao.

Alisema hata hivyo katika fomu zilizojazwa na wanafunzi wengine kumekuwa na mikanganyiko mingine baada ya watoto wa vigogo kuwekwa katika daraja la kwanza na wanaotoka katika familia ya kawaida

daraja tatu.

Profesa Mgaya alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo, waliona bora sera hiyo ipitiwe upya.

Hata hivyo, udahili chuoni hapo unaendelea chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na mafisa wa usalama wa taifa waliotanda kila eneo.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini(Uvejuta), Silinde David alisema maandamano yao yatabaki pale pale hata kama viongozi wao wamekamatwa.

"Sisi tutafanya maandamano hata kama wenzetu wamekamatwa," alisisitiza.

Tags:

0 comments

Post a Comment