SAKATA la Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda kutangaza nia ya kuwania urais ndani ya Kikao cha Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, sasa linaitikisa Chadema baada ya Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Joliana Shonza kupingana hadharani na bosi wake, John Heche.
Wakati Heche akiwa tayari ametoa tamko kumshambulia Shibuda akisema chama hicho hakitaruhusu mgombea wake urais atangaze nia kwenye vikao vya CCM, Shonza ameibuka na kusema tamko hilo la bosi wake siyo la Bavicha ila ni lake binafsi.
Jana, Shonza akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, alilikana tamko la Heche wiki iliyoipita akisema hakuna kikao ambacho baraza hilo lilikaa na kutoa kauli moja kumjadili Shibuda.
Hii ni mara ya tatu kwa Shibuda kusababisha mgongano ndani ya Chadema. Aliwahi kupinga msimamo wa kutotambua matokeo ya urais wa Jakaya Kikwete na badala yake, alishiriki tafrija Ikulu ndogo Chamwino, baada ya mkuu huyo wa nchi kuzindua Bunge la 10 na pia, aliwahi kupinga msimamo wa chama hicho kukataa posho bungeni badala yake alitaka ziongezwe hadi Sh500,000 huku akiziita ni, “ujira wa mwiha” na kuwarushia makombora baadhi ya viongozi wake akisema ni wabunge wafanyabiashara.
Katika sakata hilo la sasa, Shonzi alisema: “Naomba ifahamike kwamba tamko alilolitoa Heche siyo la Baraza, bali ni lake kama Heche. Alipokuwa akitoa tamko hilo hakukuwa na kikao chochote cha Baraza cha viongozi wa kitaifa wala Sekretarieti ya Baraza la Vijana la Chadema ili kulijadili suala hili kwa kina bali, alitumia mwamvuli wa vijana kuhalalisha hoja yake.”
Shonza alisema tamko alilolitoa dhidi ya Shibuda liliandaliwa na kuandikwa na Ofisa Habari wa Chadema Makao Makuu, kitu ambacho ni kinyume na utaratibu na kanuni za Bavicha.
“Bavicha tumejikamilisha kwa maana ya kwamba, tuna uongozi wetu kamili wa taifa. Tuna ofisi zetu ambazo ni nje ya ofisi za makao makuu sasa iweje tamko hilo likaandaliwe makao makuu tena na mtu ambaye hahusiki na Bavicha?”
Shonza alisema kama utaratibu huo alioutumia Heche ungekuwa unatumiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kufanya uamuzi binafsi pasipo kuyajadili na sekretarieti ya chama, wasingeweza kufikia matunda yanayoonekana hivi sasa.
Msimamo wa Heche
Wakati Makamu huyo akimrushia makombora bosi wake, jana Heche naye alitoa tamko akisema: “Natoa taarifa kwa umma kwamba baada ya mashauriano, Katibu wa Bavicha, Deogratias Siale ameitisha kikao cha sekretariati taifa Alhamisi, Mei 24, 2012, kwa ajili ya kujadili na kuwasilisha mapendekezo kwenye vikao halali vya chama kwa ajili ya hatua zaidi.”
Aliongeza, “Wakati huohuo, nimejulishwa kuwa Makamu wangu (Shonza), leo amezungumza na vyombo vya habari na kukanusha taarifa niliyotoa kwa niaba ya Bavicha. Itambulike kuwa majukumu na mamlaka ya mwenyekiti na kiongozi mwingine yeyote wa Baraza yanabainishwa na Kanuni za Baraza letu kifungu 5.4.1, ambayo mwenyekiti ndiye msemaji mkuu wa Baraza na pia ndiye kiongozi mkuu wa Baraza katika ngazi husika.”
Alisema kifungu cha 5.4.2 kinabainisha majukumu ya makamu mwenyekiti ambaye anapaswa kufanya kazi chini ya mwenyekiti na ndiye msaidizi wake.
Alisema Katiba ya chama ambayo ndiyo msingi mama wa shughuli za Baraza katika kanuni zake kifungu cha 7.7.1, inabainisha kazi za mwenyekiti na pia anaweza kufanya nini na wakati gani kwa kushauriana na nani.
“Kwa kutumia kifungu hiki, nilipokea ushauri kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Bavicha, akiwemo makamu mwenyekiti na kushauriana na Katibu na kuona haja ya kutoa kauli na mwongozo wa nini kitafuata kwa niaba ya baraza kama hatua ya kwanza,” alisema na kuongeza:
Bavicha Shinyanga
Bavicha Mkoa wa Shinyanga nalo jana limetoa tamko na kumkosoa Shibuda. Tamko hilo lililotolewa na Mwenyekiti wake, Nzemo Renatus, lilisema: “Tatizo letu na Shibuda ni kutoa kauli hii huku katiba ya Chadema na taratibu zake anazifahamu.
Lakini mbaya zaidi anakidhalilisha chama kwa kutoa kauli nzito katika kikao cha mahasimu wetu wakuu wa kisiasa, CCM huku akiwa mwanachama wetu. Ni sawa na mvuvi anayetoboa mtumbwi wake mwenyewe akiwa katikati ya Ziwa au Bahari.”
“Kwa niaba ya Bavicha Mkoa wa Shinyanga, naungana na kauli ya Mwenyekiti wa Bavicha Taifa. Tunaomba aitishe kamati ya utendaji ya Taifa haraka iwezekanavyo tuweze kupitisha maazimio ya kauli tatanishi za Mbunge Shibuda.”
0 comments