Raia wa Canada aliyemtemea mate Watanzania: Polisi yakamilisha uchunguzi
KAIMU Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Charles Kinyela, amesema Jeshi la Polisi limekamilisha uchunguzi kuhusiana na tukio la raia wa Canada kuwatemea mate Watanzania.
Raia huyo wa Canada alimtemea mate askari wa usalama barabarani katika eneo la Banana, baada ya polisi huyo kumfuata na kumtaka aongeze mwendo ili kupunguza msongamano wa magari.
Hata hivyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi Makao Makuu, raia huyo aliyekuwa akiendesha gari T 17 CD 178 Toyota Land Cruiser Prado alimtemea mate tena mtangazaji wa TBC1, Jerry Muro aliyekuwa akimhoji kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kenyela alisema wameshafungua jalada kwa ajili ya kesi na kwamba limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba kwa maamuzi kabla ya kufikishwa mahakamani.
“Upelelezi umekamilika na tumefungua jalada liko kwa DCI, kwa sasa tukisubiri maamuzi yake ili afikishwe mahakamani,” alisema Kenyela.
Aidha, alisema serikali itachukua hatua stahili kuhusu tukio hilo la kufedhehesha lililofanywa na raia huyo ambaye pia ni Katibu Muhtasi wa Ubalozi wa Canada nchini.
Hata hivyo, alisema kwa sasa raia huyo yuko nje kwa dhamana baada ya kutoa maelezo yake kuhusiana na tukio hilo.
Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema inaangalia hatua za kuchukua dhidi ya ofisa huyo kulingana na taratibu za kidiplomasia.
Taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari jana ilieleza imepokea kwa masikitiko taarifa za kutemewa mawe kwa askari wa usalama barabarani, Koplo Samson na mtangazaji wa TBC1, Jerry Muro.
Taarifa hiyo ilieleza ni dhahiri kitendo hicho kilichofanywa na ofisa huyo wa Ubalozi wa Canada, Jean Touchette kimeidhalilisha nchi na Watanzania na kwamba kimeonyesha kiburi na dharau ya hali ya juu kwa chombo cha dola na vya habari.
“Tunasikitika kwamba kitendo hiki kimefanywa na ofisa ubalozi kutoka nchi inayosifika sana kimataifa kwa kufuata misingi ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
“Ni jambo la kusikitisha kuona tukio hilo limetokea wakati Serikali ya Tanzania na Canada zikiwa katika uhusiano mzuri siku nyingi. Serikali ya Tanzania haitakubali uhusiano huo uharibiwe na watu wa aina hii,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Ubalozi wa Canada nchini, imesema suala hilo wamelisikia na kwamba kwa sasa wanalishughulikia.
0 comments