Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Chadema: Rais ametuuza

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
YASUSIA MCHAKATO WA KATIBA ALIOSAINI JK, CUF NAO WAALIKWA IKULU


CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011, kimekiuka makubaliano yao, hivyo kimeamua kususia mchakato mzima wa kuratibu maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia sheria hiyo.Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuonyesha kutoridhishwa na namna kiongozi huyo wa nchi, alivyowachezea akili.


"Kitendo cha Rais Kikwete kuusaini muswada huo bila ya kuupitia ni kinyume na makubaliano, jambo ambalo linatufanya tususie mchakato mzima wa kuuratibu maoni ya kwa ajili ya Katiba Mpya kupitia sheria ailiyoisaini,"alisema Mnyika na kuendelea:


“Tumeamua kujitoa kwenye mchakato mzima wa kuratibu Marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Katiba kutokana na Rais kukiuka makubaliano yetu Ikulu yaliyomtaka aupitie kwanza kabla ya kuusaini.” Mnyika aliendelea kueleza kuwa Chadema iliwasilisha waraka wa mapendekezo sita kwa Rais ikiwa ni pamoja na kumtaka asiusaini muswada huo kutokana na wananchi kutoshirikishwa ipasavyo kwenye mchakato wa ukusanyaji wa maoni.


Alisema mapendekezo mengine ni uundaji wa tume huru, upatikanaji wa uwakilishi kutoka pande zote mbili za Muungano; Zanzibar na Bara ili kutoa fursa ya kupata maoni yao katika marekebisho hayo. "Suala la tatu ni uundaji wa Bunge la Katiba na kupunguza mamlaka ya Rais na jambo la nne ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano pamoja na mfumo mzima wa uwakilishi wa pamoja katika muundo wa Bunge la Katiba."


Mnyika alisema kutokana na hali hiyo iliyojitokeza ya Rais kutowasikiliza, watawasilisha waraka huo waliompa, kwa wananchi ili nao wausome na kutoa maoni yao.


Alisema katika kutekeleza mkakati huo, hawatafanya maandamano yeyote, isipokuwa watatoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya Katiba wanayopaswa kuwa nayo.


“Nia yetu ni mzuri, lengo ni kuboresha upatikanaji wa Katiba iwe bora na itakayoweza kutoa nafasi ya ushiriki wa pande zote. Lakini kinachofanyika sasa ni kinyume. Tumeamua kuwarudishia wananchi wenyewe ili waweze kuamua kama tumekosea au la,”alieleza. Tamko hilo la Chadema limekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kutia saini muswada huo hivyo kuufanya kuwa sheria.


Rais Kikwete alitia saini muswada huo ikiwa ni siku moja baada ya yeye na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kukubaliana kwamba ipo haja ya kuendelea kuuboresha muswada ili ukidhi mahitaji ya kuaminiana na muafaka wa kitaifa. Pia, walikubaliana yawepo mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.


CUF nao wakubaliwa kukutana JK
Katika hatua nyingine, Chama Cha Wananchi (CUF) kimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili kujadili Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 2011, iliyotiwa saini juzi na mkuu huyo wa nchi. Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa baada ya kupata ombi hilo, Rais Kikwete alikubali kukutana nao.


"Ofisi ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka CUF kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete," ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza: " Rais amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza maandalizi ya mkutano huo yafanyike mara moja."


Wasomi, wanaharakati wapinga
Wakati huo huo, wasomi, wanaharakati na wanasiasa wametoa maoni tofauti kuhusu hatua ya Rais Kikwete kusaini sheria hiyo, huku Jukwaa la Katiba likieleza kuwa litafanya maandamano nchi nzima, kupinga hatua hiyo.


Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba aliliambia Mwananchi jana kuwa hatua hiyo ya Rais, ni sawa na ‘maombolezo kwa taifa’.“Wananchi hawana uwezo wa kwenda Ikulu kuzungumza na Rais, uwezo wao ni kufanya maandamano ya amani yasiyo na ukomo nchi nzima,”alisema Kibamba anayeongoza Jukwaa hilo lenye Asasi za Kiraia zaidi ya 180.


“Serikali hii siyo sikivu, inaandaa Katiba kwa maslahi yake. Sisi tunatoa juma moja kwa polisi kukubali madai yetu ya kufanya maandamano vinginevyo uvumilivu basi,”alisema Kibamba.


Alisema kitendo cha Rais Kikwete kusaini muswada huo muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Chadema ni dharau kwa chama hicho na wananchi.




Bana asema Rais ametimiza wajibu
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Benson Bana alisema Rais ametimiza wajibu wake katika kusaini muswada huo kuwa sheria. Alisema kabla ya wananchi kuanza kulaumu, wanatakiwa kusubiri kwanza Rais aunde tume hiyo ndipo watoe maoni yao.


“ Duniani kote Katiba haiwezi kutosheleza mahitaji ya kila mtu, ni lazima pande fulani zitailalamikia hata kama itakuwa inafaa kwa asilimia kubwa,”alisema Dk Bana.


Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama hicho kinasubiri kuiona Tume ya Katiba itakayoundwa na Rais. “Tunaunga mkono Rais kusaini muswada huo, tunachosubiri ni kuiona tume hiyo ikikusanya maoni ya wananchi, wakichakachua maoni ndipo tutakapoingilia kati,”alisema Mtatiro.

0 comments

Post a Comment