Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mitambo ya Dowans yauzwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KAMPUNI ya Marekani ya Symbion Power, imethibitisha kuwa imenunua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Dowans Tanzania Limited.


Hata hivyo, habari zaidi kuhusu mauzo hayo hazikutolewa kwa kuwa Dowans imepewa nguvu ya sheria ya kuzuia mtu kupewa siri za ndani za mipango hiyo bila idhini yake.


"Makubaliano yetu yamebanwa na vipengele vinavyozuia kuelezwa ovyo hadharani bila ruhusa ya muuzaji," alisema Mtendaji Mkuu wa Symbion Power, Paul Hinks.


Hinks aliwaambaia waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam kuwa tayari kampuni yake imesaini makubaliano ya ununuzi wa mitambo hiyo na Dowans na kwamba itatumika hapa nchini.




Dowans ndiyo iliyorithi mkataba wa kampuni tata ya Richmond Development LLC ambayo ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura nchini mwaka 2006 lakini ikashindwa kutekeleza mkataba huo.


Dowans iliingiza mitambo nchini na kuzalisha megawati 120 lakini mwaka 2008, Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) liliamua kuvunja mkataba huo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa sheria katika uhamishaji wa mkataba.


Hata hivyo, Dowans iliishtaki Tanesco kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Biashara (ICC) ambayo iliamuliwa kuwa mkataba huo ulivunjwa kimakosa hivyo ikaamuliwa Serikali iilipe kampuni hiyo fidia ya Sh94 bilioni.


Tatizo la upungufu wa umeme limeendelea kulikabili taifa katika vipindi tofauti ikiwamo sasa na mara zote limekuwa likiibua mjadala kuhusu mitambo hiyo ambayo wakati fulani serikali ilitaka kuinunua bila ya mafanikio.




Iliwahi pia kuripotiwa kuwa serikali ilikuwa inafanya mkakakti wa kubadili Sheria ya Ununuzi wa Umma ili iruhusu ununuzi wa vitu vilivyotumika kwa lengo la kujenga mazingira mazuri ya kununua mitambo hiyo.


Kwa sababu hiyo, hatua ya kampuni hiyo ya Kimarekani kununua mitambo hiyo inafuta uwezekano wa serikali kuitwaa.


Katika mkutano huo na waandishi wa habari hakukuwepo na mwakilishi wa Dowans na hata kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Symbion Power haikutaja jina kampuni hiyo imbayo imezusha mijadala mingi nchini.


Hinks alijigamba kuwa kampuni yake ni miongoni mwa zile zinazofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia mpango wake wa Millennium Challenge Corporation (MCC).


Isitoshe, akasema kampuni yake imeingia mkataba na Serikali ya Tanzania katika mpango mahsusi wa kuzalisha umeme vijijini chini ya Tanesco.Hata hivyo, alisema kuna uwezekano mkubwa wa kutumia mitambo hiyo kuzalisha umeme na kutatua tatizo la umeme linalokuwa linaikabili serikali mara kwa mara.


Alisema lengo la kampuni yake ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kupata umeme hata wakati ule ambao nchi inakabiliwa na upungufu wa nishati hiyo.Hata hivyo, alikiri kuwa kampuni yake inazo taarifa kwamba mzozo kati ya Dowans na Tanesco bado haujamalizika lakini akasema wanaamini ununuzi huo hauwezi kuingiliana na taratibu za kisheria na mahakama.


Alisema pamoja na mikwaruzano hiyo, jambo la kufurahisha ni kwamba kampuni yake imeamua kuingia katika mikakakti mizito ya kuwekaza Tanzania.


"Tunaunga mkono mikakati ya Wizara ya Nishati na Madini ya kutoa fursa za uwekezaji katika mpango wa ushirikiano wa kuzalisha nishati ya umeme," alisema.

0 comments

Post a Comment