Rais Barack Obama ametoa pendekezo la kuongeza kodi kwa matajiri pamoja na kupunguza matumizi ya serikali kwa kile alichokiita mtazamo wa sawa katika kupunguza nakisi kubwa kwenye bajeti ya Marekani.
Katika hotuba mjini Washington DC alieleza mipango yake ya kuongeza kodi na kubana matumizi kwa nia ya kupunguza nakisi kwa dola trilioni $4 kufikia mwaka 2023.
Aliteta juu ya mipango ya chama cha Republican akisema mipango hiyo itaumiza masikini na watu wazee.
Wanachama wa Republican wamesema kuongezwa kwa kodi "si sawa".
"Lazima tuishi kulingana na uwezo wetu,kupunguza nakisi ya bajeti yetu,na tuanze mchakato utakaotuwezesha kulipa deni letu,"Bwana Obama alisema katika hotuba yake akiwa katika Chuo kikuu cha George Washington.
"Na lazima tufanye katika njia ambayo italinda uchumi wetu,na italinda wawekezaji,tunahitaji kukuwa, tuwe na nafasi za ajira,na tuwe na mustakabali mzuri."
Kuongezeka kwa nakisi kubwa katika bajeti ya Marekani kunatarajiwa kuwa suala kuu wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2012,na katika siku za hivi karibuni,wanachama wa Republican wameandaa mipango yao wenyewe ya kupunguza nakisi hiyo, ikiwa ni kupunguza matumizi ya bima ya afya na masuala mengine ya kijamii kwa watu maskini na wazee pamoja na matumizi katika elimu.
Nakisi hiyo ya bajeti inakisiwa itafikia dola trilioni $1.5 mwaka huu na wote wanachama wa chama cha Democratic na Republican wamesema kubana matumizi ni jambo la kupewa kipau mbele.
No comments:
Post a Comment