Pages

Monday, April 11, 2011

Mbowe kuongoza maandamano Mbeya

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anatarajiwa kuongoza maandamano ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya, yenye lengo la  kushinikiza mswada kupinga muswada wa mapitio ya katiba  mpya.Maandamano hayo yanayotarajiwa Jumamosi ijayo, yamendaliwa na chama hicho cha upinzani.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya Mbowe, kila mbunge wa chama hicho, atakwenda katika mkoa mmoja kuongoza maandamano.Habari kuhusu kiongozi huyo kuongoza maandamano hayo mkoani Mbeya, zilitangazwa jana na Katibu wa Chadema wa mkoa huo, Eddo Makatta, alipokuwa akizungumza na waandishi habari.

Alisema chama hicho kinatarajia kufanya maandamano makubwa ya kupinga muswada na kwamba tayari maandalizi yameanza."Imeonekana kuna  ujanja ujanja ambao serikali inataka kuufanya kwa kuwatumia watu wachache,kutoa  maoni kuhusu katiba kwa  manufaa ya wachache na kuwakandamiza wananchi walio wengi,"alisema.

Alisema maandamano hayo yatafuatiwa na mkutano mkubwa utakaohutubiwa na Mbowe.Kuhusu hatua ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Mbeya,Sambwee Shitambala, kuhamia CCM alisema chama chake hakina taarifa rasmi  na kwamba habari hizo kimezipata kupitia vyombo vya habari.

Alisema hata hivyo kama kweli Shitambala  amemua kuhamia CCM, hajafanya kosa kwa sababu hiyo ni haki yake ya kikatiba."Chama chetu hakiwezi kulumbana naye, kwanza ni mchanga kisiasa na tunamuonea uhuruma kwa hatua hiyo ya kwenda katika chama kinachoendelea kupasuka na kukiacha chama  kinachozidi kuimarika," alisema Makatta.

Katibu huyo amemtaka Shitambala asitumie  vifaa mbalimbali vya Chadema.

No comments:

Post a Comment