Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - AU yabariki mabavu kumng’oa Gbagbo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SASA ni dhahiri kwamba, siku za Laurent Gbagbo wa Ivory Coast za kuing’ang'ania Ikulu ya nchi hiyo zinahesabika, kwani Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limeridhia na kumtambua rasmi Alassane Ouattara kuwa ndiye aliyeshinda urais katika uchaguzi mkuu wa Novemba 28, mwaka jana.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya jopo la Marais watano wa Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhu kwa mgogoro wa Ivory Coast, kubaini kwamba, Ouattara alishinda kihalali katika uchaguzi huo.

Mbali ya kutangaza kumtambua Ouattara, AU imeipa rungu Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) la kuhakikisha rais huyo anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa anaingia rasmi madarakani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alipozungumza na wanahabari wizarani kwake.

Alisema kwamba, tayari Ouattara yuko Abuja, Nigeria kukutana na Mwenyekiti wa ECOWAS, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ili kupanga mikakati ya kuingia Ikulu ya Ivory Coast inayong’ang’aniwa na Gbagbo.

Alisisitiza kwamba, AU imependekeza njia mbili zitumike kuhakikisha Ouattara anaingia madarakani, moja ikiwa kumshawishi Gbagbo aondoke madarakani kwa hiyari yake, na kama itashindikana, basi jukumu la matumizi ya nguvu litaachwa mikononi mwa ECOWAS.

“Niwe muwazi, uamuzi huu unaweza kuleta vita, lakini itakuwa vita halali, vita ya kupigania demokrasia ya kweli kwa sababu wananchi walishaamua katika visanduku vya kura.

“Kwa hiyo msishangae kama ikitokea vita, bado nasisitiza itakuwa vita halali na kipimo halali cha Ouattara kwenda Ikulu,” alisema Membe aliyeelezea kwa undani kiini cha kufikiwa kwa uamuzi huo, baada ya timu ya AU kufanya uchunguzi wa kina tangu kuanza kwa mgogoro wa uongozi nchini Ivory Coast mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema kwamba, kikubwa ambacho timu ya AU ilibaini ni upotoshwaji uliofanywa na Baraza la Katiba la nchi hiyo lililokwenda kinyume na Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast ambayo chini ya mwenyekiti wake, Yussuf Bakayoko ilimtangaza Ouattara kuwa mshindi.

“Tume ilitangaza matokeo ya kweli, lakini kwa sababu za kiusalama, mara baada ya Bakayoko kumtangaza mshindi alitoroshwa kwenda Ufaransa ambako yupo mpaka sasa.

“Lakini kuna ushahidi wa kutosha kwamba kura alizopata Ouattara na kutangazwa ni sahihi kwa sababu matokeo yote yalikuwa yanatumwa kwa wakati mmoja na tume kwenda Baraza la Katiba, ECOWAS, Umoja wa Mataifa na hata kwa wagombea wenyewe wa urais,” alisema Membe na kuongeza kwamba, Baraza la Katiba liliharibu hali ya hewa kwa kufuta matokeo katika baadhi ya majimbo, na kumtangaza Gbagbo mshindi kabla ya kurudiwa kwa uchaguzi.

Mpaka sasa uchaguzi haujarudiwa. Wajumbe waliokuwa wamepewa jukumu la kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa kisiasa Ivory Coast, mbali ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz, walikuwepo pia Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Idriss Deby Itno wa Chad na Blaise Compaore wa Burkina Faso.

Katika majukumu yao, viongozi wa Afrika walikutana mara ya kwanza mjini Nouakchott, Mauritania Februari 20 mwaka huu kabla ya kwenda Abidjan, Ivory Coast Februari 21 na 22 kukutana na pande mbili zinazovutana na pia kufanya mazungumzo na Tume ya Uchaguzi wa nchi hiyo na Baraza la Katiba ili kupata hali halisi ya jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa hadi matokeo ambayo yalipingwa na kusababisha Gbagbo na Ouattara kila mmoja kujitangazia ushindi.
Tags:

0 comments

Post a Comment