Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Waziri aua polisi Zanzibar

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

ASKARI wa Jeshi la Polisi, Koplo Ali Khamis Haji (40), amefariki dunia baada ya kugongwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa SMZ, Ramadhan Abdallah Shaban, eneo la Mombasa, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Askari huyo alikuwa akitokea katika kituo chake cha kazi Polisi Ng’ambo na kupakiwa katika Vespa iliyokuwa ikiendeshwa na Said Abdallah Suleiman yenye namba za usajili Z 830 CA, lakini baada ya kufika katika eneo hilo, ghafla gari la waziri lenye namba za usajili Z 247 BH lilikatisha na kuingia barabara kuu itokayo Mwanakwerekwe kwenda Kiembesamaki akitokea upande wa pili wa kijiji cha kulelea watoto yatima cha SOS.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokea Januri 13 saa 10:30 asubuhi na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali pamoja na kifo cha askari huyo mwenye namba E 3665, ambaye aliumia mguu wa kushoto na uti wa mgongo, ambapo marehemu alikimbizwa na kulazwa siku moja katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Kamishna huyo alisema kwamba uchunguzi wa suala hilo umegawanyika sehemu mbili, kujua chanzo cha kifo pamoja na chanzo cha ajali, kwa vile baada ya kutokea kwa ajali hiyo, hali ya marehemu ilikuwa ikiendelea vizuri kwa vile alikuwa akitibiwa na kurejea nyumbani, lakini ghafla alifariki dunia njiani Januri 28, wakati akikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kwamba dereva aliyempakia marehemu, Said Abdallah Suleiman, mkazi wa Kwaalimsha, ameshahojiwa na polisi, pamoja na maiti ya marehemu ilikwisha kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, lakini Waziri Shaban hajachukuliwa maelezo, gari lake halijakaguliwa, ikiwamo leseni na bima pamoja na kutochorwa kwa ramani ya tukio hilo.
Kutokana na uzito wa tukio hilo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mjini Maghribi, Shafi Iddi Hassan, amekwisha kumtaarifu mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Zanzibar kuhusiana na suala hilo ambalo limeibua mjadala mkubwa kwa baadhi ya askari Zanzibar, kutokana na faili la kesi hiyo kutofikishwa mahakamani tangu kutokea kwa ajali hiyo Januari 13, mwaka huu.
“Kilichosalia hadi sasa katika ajali hiyo, gari la waziri, leseni pamoja na bima bado havijakaguliwa, na hata ramani ya tukio hilo bado haijachorwa ili kujua nani alikuwa mkosaji,” kilidokeza chanzo kimoja kutoka katika ajali hiyo.
Taarifa kutoka katika eneo la tukio, zinasema Waziri Shaban alikuwa akiendesha gari hilo, akitokea barabara ya SOS akielekea Kiembesamaki na ndipo alipomgonga mwendesha Vespa huyo aliyekuwa amempakia askari, ambao walikuwa katika njia kuu ya barabara itokayo Mwanakwerekwe kuelekea Kiembesamaki.
Tangu kutokea ajali hiyo, afya ya marehemu ilikuwa ikizorota, kutokana na maumivu makali katika mguu wa kushoto na maeneo ya kiuno chake, na alifariki dunia akiwa anakimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, na kuzikwa Januari 28 katika eneo la Kisauni, Wilaya ya Magharibi mjini Unguja, lakini hadi jana hakuna ripoti yoyote iliyotolewa licha ya kuelezwa kwamba uchunguzi wa kitabibu ulifanyika kabla ya marehemu kuzikwa.
Maziko ya Koplo Ali Khamis Haji yalihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo askari aliokuwa akifanya nao kazi, pamoja na Waziri Ramadhan Abdallah Shaban, katika Kijiji cha Kisauni, ambapo marehemu ameacha wake wawili na watoto kadhaa.
Ajali hiyo iliyosababisha kifo cha askari wa Jeshi la Polisi, imekuja muda mfupi tangu kutolewa kwa hukumu ya Mbunge wa Bariadi Mashariki na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye alitozwa faini na kuachiwa huru.
Tags:

0 comments

Post a Comment