Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mwanza: Polisi waridhia maandamano ya Chadema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Polisi mkoani Mwanza wameridhia maandamano yaliyoandaliwa na Chadema, kupinga  malipo ya fidia kwa Kampuni ya Dowans, kuongezeka kwa gharama za maisha na kupanda kwa gharama za umeme.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi alisema tayari wamekwishakamilisha maandalizi ya maandamano hayo, yatakayofanyika leo kuanzia saa 8: 00 mchana na kufuatiwa na mkutano wa hadhara.

Maandamano ya Mwanza yanafanyika takriban miezi miwili tangu kutokee mauaji ya raia waliopigwa risasi na polisi mkoani Arusha, wakati walipokuwa wakizuia maandamano ya Chadema mkoani humo.

Katika tukio hilo la Januari 6, mwaka huu watu kadhaa walijeruhiwa, polisi wa Arusha walimwaga damu za watu kadhaa, walioshiriki na wasioshiriki maandamano yaliyoandaliwa na Chadema.

Risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika katika jitihada za polisi kuzima maandamano ya Chadema, wakitekeleza amri ya Mkuu wa Jeshi hilo, Ispekta Jenerali Said Mwema ambaye awali aliyapiga marufuku baada ya kuwa yameruhisiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye.

Jana Mushumbusi alisema maandamano ya Mwanza yatahitimishwa kwa mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Viwanja vya Furahisha, Kirumba jijini hapa kuanzia saa10:00 jioni.

Tayari Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amewasili jijini hapa kwa lengo la kushiriki maandamano hayo ya kwanza kufanyika Mwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, Oktoba 31 mwaka jana.

Dk Slaa aliwasili jijini Mwanza jana mchana. Viongozi wengine wa Chadema wanaotarajiwa kushiriki maandamano na baadaye mkutano ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Mushumbusi alisema mbali na viongozi wa taifa wa Chadema, wabunge wote wa chama hicho wanatarajiwa kuhudhuria maandamano hayo.

Aliwataka wapenzi, wanachama na Watanzania wote kwa ujumla wanaochukia ufisadi kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza kushiriki.

“Sisi maandalizi yetu yamekamilika na viongozi wote wa kitaifa wa chama na wabunge wote wa Chadema wamethibitisha kuhudhuria maandamano yetu ambayo yataanzia Kituo cha Mabasi cha Buzuruga, Nyakato na kupita Barabara ya Mwanza-Musoma, Nyerere, Kenyatta na kuingia Barabara ya Uwanja wa Ndege kwenda hadi katika Viwanja vya Furahisha,” alifafanua katibu huyo wa Chadema.

Mushumbusi alisema kutokana na wao kufanya maandamano ya amani, chama chake kimeandika barua ya taarifa kwa Jeshi la Polisi na kuzingatia sheria ya kutoa taarifa kwa jeshi hilo saa 48 kabla ya kuandamana na wala siyo kuomba kibali.

“Barua ya kuwataarifu Jeshi la Polisi kuhusiana na maandamano tuliwakabidhi tangu Februari 20, mwaka huu na Jeshi la Polisi limekubaliana na maandamano yetu na njia ambazo tutapitia, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi, tutaendelea na maandamano yetu kama yalivyopangwa,” alieleza Mshumbisi.

Katibu huyo alisema lengo la maandamano yao ni kupinga vitendo vya ufisadi, malipo ya Sh94 bilioni ya tozo kwa ajili ya kampuni ya Dowans, kupinga kupanda na kuongezeka kwa bei ya umeme nchini na kuongezeka kwa gharama za maisha.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Simon Sirro alipoulizwa kuhusu maandamano hayo, alisema jeshi lake limejipanga na kusema hawana tatizo na maandamano hayo na kwamba watahakikisha wanatoa ulinzi mkali kulinda watu wasio na nia njema kutumia mwanya huo kuzusha vurugu.

“Hatuna tatizo na maandamano, haya tumeridhia na kukubaliana ni wapi watapita, tumejipanga kwa ulinzi ili kuhakikisha maandamano hayo yanakuwa ya amani na salama kwa watu wengine na mali zao,” alieleza Kamanda Sirro.

Wachunguzi wa mambo waliozungumzia maandamano hayo walisema huenda yakapata ushiriki wa watu wengi kutoka na mada ziliyopangwa kuzungumzwa, kuwagusa watu wengi.
Tags:

0 comments

Post a Comment