Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Yanga, Simba zakabwa koo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa barani Afrika, Yanga na Simba jana zilianza kwa kusuasua katika kampeni zao baada ya kukabwa koo na wapinzani wao na kulazimishwa sare.
Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Yanga ilijiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele baada ya kulazimisha sare ya 4-4 dhidi ya Dedebit ya Ethiopia.
Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi ya aina yake na kufanikiwa kufunga bao katika dakika ya tisa, lililowekwa wavuni na Nadir Haroub ‘Canavaro’ aliyeunganisha faulo safi iliyopigwa na Omega Seme iliyomshinda kipa wa Dedebit Biryam Habtamu.
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Dedebit, lakini mabeki wa timu hiyo walikuwa makini na kuondosha hatari zote zilizojitokeza langoni mwa timu yao.
Dedebit walizinduka na kuanza kuigeuzia kibao Yanga na kufanikiwa kuchomoa bao hilo katika dakika ya 25 lililowekwa wavuni na Getaneh Kabede baada ya beki wa Yanga, Isaac Boakye, kumpa Damit Tikabu pasi akiwa katika eneo la hatari ambaye alimpasia mfungaji.
Baada ya bao hilo, Dedebit walizidisha mashambulizi langoni mwa Yanga na kufanikiwa kufunga bao la pili katika dakika ya 36 lililofungwa na Birhanu Bogale akimalizia kazi safi ya Tikabu aliyemlamba chenga Canavaro kabla ya kumpasia mfungaji.
Dedebit walifunga bao la tatu dakika ya 42 lililowekwa wavuni na Tikabu, aliyefunga kwa shuti la mbali nje ya 18 baada ya kupokea pasi ‘bomba’ ya mbali iliyopigwa na Getaneh Kabede.
Yanga walifunga bao la pili lililofungwa dakika ya 44 na Nurdin Bakari aliyepiga shuti la mbali nje ya 18 baada ya kutumia vizuri pasi ya Godfrey Bonny.
Hadi mwamuzi wa mchezo huo, Abdulqadir Beldin wa Sudan anapuliza filimbi ya mapumziko, Dedebit ilitoka uwanjani ikiwa mbele kwa mabao 3-2.
Kipindi cha pili, timu hizo zilirejea uwanjani zikiwa na nguvu mpya, lakini walikuwa ni Dedebit waliopata bao la nne dakika ya 61 lililofungwa na Mesten Wondemu aliyeunganisha krosi safi ya Tikabu.
Yanga walifunga bao la tatu dakika ya 87 lililofungwa na Jerry Tegete aliyeunganisha mpira uliomshinda kipa wa Dedebit na kuukwamisha mpira wavuni.
Dedebit waliendelea kulisakama lango la Yanga, ambako mashabiki wa soka wa Tanzania waliwashangilia kwa nguvu Wahabeshi hao hali ambayo ilionyesha kuwakatisha tamaa Yanga.
Mashabiki wakiamini Yanga imelala, Tegete alifunga bao la kusawazisha dakika za nyongeza kwa shuti la mbali, baada ya kupewa pasi safi ya Davies Mwape.
Baada ya mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Fred Felix Minziro, alisema kukosekana kwa viungo Athumani Idd na Abdi Kassim, kunaigharimu timu hiyo ambayo imepata wakati mgumu katika mchezo huo baada ya nafasi za viungo kufa.
Minziro alisema, katika mchezo huo wachezaji hawakuwa na morali kutokana na mgogoro unaoitawala klabu hiyo hivi sasa kutokana na baadhi ya viongozi kutimuliwa katika timu hiyo.
Minziro alisema, ili kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano unaotarajiwa kuchezwa kati ya Februari 11 na 13, ataipanga vilivyo timu yake kwa ajili ya mchezo huo.
Beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Canavaro’ alisema anashangazwa na jinsi walivyocheza, hasa tatizo likiwa ni kutosaidiana kwa baadhi ya wachezaji hali ambayo imesababisha kukubali kipigo cha mabao hayo.
Canavaro alisema kipigo hicho kimemuumiza na kuwa sababu nyingine iliyosababisha kutoka sare hiyo ni mgogoro wa viongozi ulioanza hivi karibuni ambao kwa kiasi fulani unaathiri jitihada za timu.
Dedebiti iliwakilishwa na Biryam Habtamu, Birhanu Bogale, Mengistu Assefa, Shwaibu Gabriel Ahmed, Damit Tikabu, Getaneh Kabede/Temesgen Tekle, Eprem Zelu/Mulegeta Mihret, Mohamed Adam, Behailu Assefa na Mesten Wondemu/Teddele Mendesha.
Yanga: Yaw Berko/Nelson Kimath, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasyika, Isaac Boakye/Ibrahim Mwaipopo, Nadir Haroub Canavaro, Nurdin Bakari, Godfrey Bonny, Omega Seme, Jerry Tegete, Davies Mwape, Idd Mbaga/Nsa Job.
Wakati hali ikiwa hivyo Jangwani, mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba nayo ililazimisha sare ya bila kufungana dhidi ya Elan de Mitsoudje ya Comoromchezo uliochezwa Moron visiwani humo.
Matokeo hayo hayakutegemewa na mashabiki wengi wa soka hapa nchini, hasa kutokana na historia ya timu za Comoro ambazo zimekuwa zikija hapa nchini kuwa dhaifu.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mzambia Patrick Phiri alisema licha ya kugemea upinzani lakini matokeo hayo hayakumfurahisha, hivyo ameishausoma mchezo wa timu hiyo na kuwa ataufanyia kazi ili mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam timu yake iibuke na ushindi na kusonga mbele.
Wawakilishi wengine, KMKM ya Zanzibar nayo ilipata kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 4-0 kutoka kwa FC Motema kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Zanzibar, ukiwa ni mchezo wa kombe la shirikisho.
MKesho kwenye uwanja huo, mabingwa wa Zanzibar, Zanzibar Ocean View leo wanashuka kuwakaribisha AS Vita ambao ni mabingwa wa Congo DRC.
Kwa matokeo hayo Yanga na Simba zina kibarua kuhakikisha zinashinda katika michezo yao ya marudiano ili ziweze kusonga mbele, ingawaje KMKM ndiyo ina kibarua kigumu kutokana na kukubali kipigo hicho kikubwa.
Tags:

0 comments

Post a Comment