ASISITIZA MIJADALA YA DOWANS, KATIBA ISIWASAHAU VIJANA
MBUNGE wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amelitaka taifa kujipanga kukabiliana na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira ya vijana ili kuepuka maafa kama yale yanayotokea sasa katika nchi za Tunisia na Misri.
Lowassa, aliyekuwa akihutubia wakati wa mahafali ya kwanza ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii kilichopo Monduli, alisema wananchi wanapaswa kulijadili tatizo hilo linalozidi kukua kila siku wakati wanapojadili masuala mengine yanayogusa masilahi ya taifa kama Dowans na Katiba.
“Tuzungumze Dowans, tuzungumze Katiba, tuzungumze pia kuhusu tatizo la ajira ya vijana wetu. Ndiyo tunaweza,” alisema Lowassa.
Katika hotuba yake hiyo, Lowassa alitumia maneno yaliyotolewa wiki iliyopita na Rais wa Marekani, Barrack Obama, wakati akihutubia Bunge la nchi hiyo aliposisitiza kuhusu umuhimu wa kutengeneza ajira mpya kwa ajili ya vijana wa taifa hilo kubwa duniani.
“Iwapo nchi kubwa kama Marekani zinaona umuhimu wa kuwekeza katika ukuaji wa ajira, ubora wa ajira na tija ipatikanayo na muono huo, nchi changa kama Tanzania inapaswa kuwa na mikakati mipana zaidi,” alisema Lowassa akisisitiza kuhusu unyeti wa tatizo hilo.
Akifafanua, Lowassa alisema wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana na serikali katika kubuni njia ya kukabiliana na tatizo hilo la ajira ambalo iwapo halitadhibitiwa linaweza kuleta madhara makubwa.
“Sekta zinazoshughulikia tatizo la ukosefu wa ajira zijitahidi kupunguza tatizo hilo kwani ni bomu ambalo likilipuka hakutakuwa na amani na utulivu tulionao hivi sasa. Tuliwahi bomu hili kabla halijalipuka,” alisema.
Alisema pamoja na jitihada za serikali za kutatua tatizo hilo, bado kuna changamoto kubwa katika kuongeza tija za uzalishaji wa ajira hapa nchini.
Alisema hapo zamani takwimu zilikuwa zikionyesha kuwa vijana wengi waliokosa ajira ni wale ambao hawakuwa na elimu lakini hivi sasa mambo ni tofauti, kwani hata wenye elimu nao wamekumbwa.
Alisema ukosefu wa ajira hasa kwa watu wenye elimu ya kukidhi viwango ni hatari kwa taifa na iwapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa kutatua hali hiyo, nchi inaweza kuingia katika matatizo makubwa.
“Ndugu zangu wananchi na wahitimu sote tutakumbuka mwaka 2005 CCM, ilitambua ukali wa tatizo hili ikaahidi kutengeneza ajira milioni moja ndani ya miaka mitano. Leo tunapogeuka nyuma na kuangalia namna ahadi na dhamira hiyo ilivyotekelezwa, jibu tunalopata liko wazi, kwamba bado tatizo lipo na ni kubwa,’’ alisema.
Aliongeza kuwa tatizo la jira kwa vijana hapa nchini ni kubwa na linazidi kukua siku hadi siku, hali iliyosababisha kushindwa kufikia malengo ya Mpango ya Kupunguza Umasikini na kukuza Uchumi (Mkukuta), ambayo yalitaka hadi kufikia mwaka jana kuwe kumepungua kwa tatizo hilo hadi kufikia asilimia 6.9.
Lowassa alisema takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2006 zinaonyesha kuwa hadi wakati huo asilimia 11.7 ya vijana walikuwa hawana ajira ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2000 wakati idadi ilikuwa asilimia 13.
Akionyesha namna tatizo hilo lilivyo kubwa, alisema Septemba mwaka 2008, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Ladius Komba, aliwasilisha mada mjini Monrovia nchini Liberia na kunukuliwa akisema wastani wa vijana wasio na ajira mjini unafikia asilimia 16.5 ikilinganishwa na vijijini ambako ni wastani wa asilimia 7.5.
Akiendelea kumnukuu Komba, alisema takwimu hizo zilionyesha hali kuwa mbaya zaidi kwa Jiji la Dar es Salaam ambako idadi ya watu waliokuwa hawana ajira walikuwa ni asilimia 31.5.
Alisema kuwa ni wazi idadi hiyo ni kubwa ambayo inahitajika kutafutiwa ufumbuzi na wadau mbalimbali kabla suala hilo halijalipuka, kwani ni wazi kwamba tukiwa kama taifa tunapaswa kutambua tumekalia bomu linaloweza kulipuka wakati wowote.
Lowassa alitumia fursa hiyo kupinga kuwa hoja zinazotolewa na watu mbalimbali kuwa Tanzania ni nchi maskini na kusisitiza kuwa si maskini bali ni nchi changa kwasababu ina matatizo ya kutumia rasilimali nyingi ilizonazo.
“Nasisitiza sisi si maskini, ni wachanga, tuna utajiri mkubwa sana wa rasilimali bado tunahitaji muono mpana wa jinsi ya kutumia rasilimali hizo kukuza uchumi wa taifa,’’ alisema.
Alisema kuna ushauri mbalimbali uliotolewa na wataalamu ambao unapaswa kufuatwa kwa kubadili mitaala iliyopo ya elimu ili iwe inayomuwezesha muhitimu ajiajiri kulingana na fani aliyoisomea.
Katika mahafali hayo Lowassa aliahidi kutoa msaada wa kompyuta baada ya kusikia changamoto zinazokikabili chuo hicho.
Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1978 kilipitia katika hatua tofauti kabla ya hivi sasa kugeuzwa na kuwa chuo cha maendeleo ya jamii na kufanya mahafali yake ya kwanza tangu kianze kutoa elimu ya maendeleo ya jamii.
0 comments