BAADA ya miaka 18, Denmark, kupitia Shirika lake la Misaada ya Maendeleo (DANIDA), limejitoa kufadhili Mpango wa Elimu ya Demokrasia na Utafiti (REDET) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Raia Mwema imethibitisha.
Ingawa taarifa za kujitoa kwa DANIDA zinahusishwa na mwenendo wa REDET katika matokeo ya utafiti wa kisiasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, yaliyodaiwa yalikuwa yanachakachuliwa, Mwenyekiti Mwenza wa REDET Dk. Benson Bana, amepuuza taarifa hizo akieleza sababu nyingine.
Miongoni mwa waliolalamikia taarifa za utafiti wa REDET ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa anagombea urais na aliyeshindwa na Jakaya Kikwete wa CCM, alipata kudai kwamba matokeo ya utafiti wa REDET yaliyokuwa yakikitabiria chama chake na yeye kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana yaliongozwa na tafiti batili zilizokuwa zikikipendelea chama tawala.
REDET ni miongoni mwa asasi zilizotoa taarifa za utafiti, kabla ya Uchaguzi Mkuu, zilizotabiri kwamba mgombea wa CCM, Kikwete, angeshinda huku Dk. Slaa na wagombea wengine, akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, wakifuatia kwa mbali.
Akizungumzia kujitoa kwa DANIDA kufadhili REDET wiki hii, Dk. Slaa ameliambia Raia Mwema katika mahojiano maalumu kwamba hatua hiyo ya DANIDA ni ya kupongezwa japo “walipaswa kujitoa muda mrefu uliopita, maana tulikwishakulalamika mara nyingi sana. Hawa (REDET) wanapanga matokeo halafu wanatafuta njia ya kuyachakachua.”
Taarifa zilizosambazwa awali zilieleza kuwa DANIDA, mfadhili mkuu wa REDET, ilijitoa kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa taasisi hiyo ya kitaaluma hasa baada ya kulalamikiwa na baadhi ya makundi ya kijamii, wakiwamo wanasiasa.
Hata hivyo, katika mahojiano yake na Raia Mwema, Dk. Bana alithibitisha kujiondoa kwa DANIDA lakini akisema sababu ya kitendo hicho si mwenendo wa REDET bali ni kwamba majukumu ya asasi hiyo yamefikia hitimisho.
“REDET katika majukumu yake ilikuwa na awamu sita za utendaji ambazo zilipaswa kukamilishwa Desemba 31 mwaka 2010. Kila programu ilikuwa na madhumuni na zilipangwa kukamilishwa Desemba mwaka jana. Hata mikataba ya ajira za watendaji ilieleza kwisha wakati huo,” alisema Dk. Bana, akisisitiza kwamba ‘maisha’ ya REDET kimajukumu yalipaswa kukamilika mwishoni mwa mwaka jana.
Lakini kuhusu kujitoa kwa mfadhili na sababu za kujitoa kwake alisema; “DANIDA ni mfadhili mkuu na kwa kweli tunawashukuru sana; wamekuwa wakitufadhili tangu mwaka 1992.
“Sera zao zimebadilika hasa katika masuala ya utawala bora na ubinafsishaji; kubadilika kwa sera zao huko kwao ni lazima kutaathiri sisi tunaofadhiliwa.
“Kujitoa kwao si suala la ghafla. Ilikuwa ikijulikana watajitoa kwa sababu hata kazi za REDET zilikuwa na ukomo ambao umekwisha kufika Desemba 31, 2010.
“Haijawahi kutokea Afrika kwa mfadhili kuendelea kufadhili taasisi moja kwa miaka 18. Hiyo inaonyesha jinsi gani REDET imekuwa na hadhi kubwa na kazi zake ni za viwango vya kitaaluma.”
Kwa upande mwingine alisema kuna baadhi ya kazi ambazo zilipaswa kukamilishwa na REDET lakini hazikufanyika kwa wakati kutokana na Uchaguzi Mkuu (wa mwaka jana) na kwamba zitakamilishwa katika mwaka huu.
Alizitaja kazi hizo ambazo tayari zimekwisha kutolewa fedha kwa ajili ya utekelezaji kuwa ni pamoja na utafiti kuhusu hali ya kisiasa nchini na uwezeshaji, lengo likiwa ni pamoja na kuitazama Serikali ilivyotimiza wajibu wake kwa umma.
Kazi nyingine kiporo aliitaja kuwa ni mkutano wa mabadiliko ya kidemokrasia Afrika Mashariki.
Mbali na kujitoa kwa mfadhili huyo, uchunguzi wa gazeti hili pia ulibaini kuwa REDET iko katika mchakato wa ‘kufumuliwa’ ikiwa ni pamoja na kubadilisha muundo wake na hata majukumu yake ya awali.
Kutokana na taarifa hizo, Dk. Bana aliulizwa na kukiri kuwapo kwa mpango huo akibainisha kuwa tayari rasimu ya mapendekezo imeridhiwa na Bodi ya Baraza la Chuo cha Fani na Sayansi ya Jamii.
“Nikwambie tu kwamba tayari rasimu ya mapendekezo ya kuibadili REDET imekwisha kupitishwa na Bodi ya Baraza la Chuo cha Fani na Sayansi ya Jamii.
“REDET kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itabadilishwa na kuwa taasisi au kituo cha utafiti na shughuli nyingine hasa za kitaaluma.
“Wakati inaanzishwa, utakumbuka, ndio ulikuwa mwanzo wa mfumo wa vyama vingi na lengo lilikuwa kutoa elimu ya uraia na uwezeshaji kidemokrasia; sasa shughuli zitaweza kubadilika kulingana na mambo mawili:
“Kwanza ni theme (maudhui) na pia mwenendo wa hali ya kisiasa nchini Tanzania. Programu zetu za awali zilikuwa katika awamu sita kwa mihula mitatu mitatu, na tulikuwa tunafanya tathmini baada ya kila kipindi. Sasa, katika mtazamo mpya, tunaweza kuwa na programu za muda mrefu na zitakazofanyiwa tathmini, kwa mfano, kila miaka mitano,” alisema Dk. Bana.
Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri wa CHADEMA John Mrema ameiambia Raia Mwema kwamba ni kweli chama chake kimekuwa na malalamiko kuhusiana na jinsi REDET ilivyokuwa inatumika kisiasa kwa maslahi ya CCM.
“Ni kweli tulilalamika kwa kukutana na watu mbalimbali ana kwa ana na pia kwa kuandika barua rasmi kuelezea kutoridhishwa kwetu na tafiti za REDET kabla ya uchaguzi wa mwaka jana. Kwanza walikuwa wakienda mikoani wanafikia kwa wakuu wa wilaya ambao wanawapa maelekezo ya nini cha kufanya.
“Halafu wanaelekezwa kwa makatibu tarafa na wajumbe wa nyumba kumi ambao wote ni makada wa CCM. Viongozi hao wa CCM ndio waliokuwa wakiwaongoza watafiti wa REDET juu ya watu wa kuwahoji,” anasema Mrema.
Juhudi za kuupata ubalozi wa Denmark nchini kuzungumzia sababu za kujitoa kwa DANIDA kufadhili REDET hazikuzaa matunda, ingawa zinaendelea.
Hata hivyo, taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, zinaonyesha kuwa Ubalozi wa nchi hiyo Tanzania umekuwa ukifanya mapitio ya mipango-kazi ya REDET. Taarifa hizo zilitolewa Julai 1, mwaka jana.
Ubalozi huo umekuwa ukifanya uhakiki wa mipango ya REDET kwa kutumia jopo la wataalamu ili kujiridhisha kuwa asasi hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa malengo yake ambayo ni kuwezesha mchakato wa kidemokrasia kupitia tafiti, machapisho na elimu ya moja kwa moja inapobidi.
Katika awamu yake ya sita kwenye mipango yake, ubalozi wa Denmark unaeleza kuwa kazi ya REDET ilikuwa ni uwezeshaji kidemokrasia, elimu ya uraia na uwajibikaji.
Tathmini ya kazi za REDET inaonyesha kufanyika kwa mara ya mwisho na timu maalumu ubalozini kuanzia Februari 4 hadi 14, mwaka 2009.
Walioshiriki katika tathmini au mapitio hayo ni pamoja na Anders Baltzer Jørgensen, aliyekuwa mshauri wa masuala huduma za kiufundi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Denmark.
Wengine ni Bornwell Chikulo, Jan Kees van Donge na Steen Skovgaard Larsen wote washauri wa masuala ya nje wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark.
Jopo hilo la tathmini katika kufanya kazi yake lilipata kukutana na baadhi ya wafanyakazi wa REDET, akiwamo mwanzishili na Mwenyekiti wa kwanza wa REDET, Profesa Rwekaza Mukandala. Pia jopo hilo lilikutana na wadau wengine wa REDET Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Dk. Bana pia alirejea kauli yake ya mara kwa mara kuwa wale ambao wamekuwa hawaridhishwi na matokeo ya tafiti za REDET, wamekuwa wakitoa hoja zao nje ya misingi ya taaluma ambayo ndiyo iliyokuwa ikitumiwa na REDET kutafiti.
“Nimekuwa nikiwaeleza, kama unapinga utafiti wa REDET fanya hivyo kwa kutumia utafiti pia Mara nyingi wengi wao wamekuwa wakipinga kwa kelele zisizozingatia tafiti. Sisi ni wanataaluma, tunatumia mipango ya kitaaluma na matokeo yetu yanazingatia taaluma,” alisema.
Matokeo ya mwisho ya utafiti wa REDET kuhusu nafasi ya urais, siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, yalionyesha kuwa mgombea wa CCM, Kikwete angepata asilimia 71.2, Dk. Slaa (CHADEMA) asilimia 12.3 na Profesa Lipumba (CUF) 10.1 ya kura zote, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Kikwete kuwa mshindi kwa asilimia 61.17 akifuatiwa na Dk. Slaa asilimia 26.34 na Profesa Lipumba aslimia 8.06.
0 comments