IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba jana waliendeleza uonyonge mbele ya watani zao wa jadi Yanga baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, licha ya wekundu hao wa Msimbazi kutawala zaidi kipindi cha kwanza na kukosa mabao matatu ya wazi katika dakika tatu za kwanza.
Simba pia ilifungwa na Yanga kwa penalti 3-1 katika mchezo wa Ngao ya Jamii ya maandalizi ya ufunguzi wa msimu Agosti.
Yanga iliyocheza chini ya kiwango na kuwatia hofu mashabiki wake walioanza kukata tamaa kutokana na mchezo mbovu katika kipindi hicho cha kwanza kabla haijazinduka katika kipindi cha pili, iliandika bao pekee lililoitoa kifua mbele na kudhihirisha umwamba mbele ya wapinzani wake hao wakubwa lililofungwa na Jerrson Tegete katika dakika ya 70.
Tegete alifunga bao hilo lililowazindua mashabiki wa Yanga na kuwanyamazisha Simba, baada ya kupenyezewa mpira na Ernest Boakey aliyekimbia na mpira kwa hatua chache kabla hajatoa chumba kwa mfungaji aliyemvuta kipa wa Simba Juma Kaseja na kuubetua mpira kwa juu na kujaa wavuni.
Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi na katika sekunde ya 28 Rashid Gumbo alipiga krosi iliyomkuta Amri Kiemba katika nafasi nzuri ya kufunga lakini alipiga mpira uliokolewa na kipa wa Yanga Yaw Berko. Berko aliokoa tena mpira wa Emmanuel Okwi aliyetaka kufunga katika sekunde ya 57.
Simba ilipoteza tena nafasi nyingine nzuri katika dakika ya tatu kutokana na mpira wa kona na Patric Ochan nusura aifungie timu yake bao la kuongoza katika dakika ya saba lakini shuti lake kali la umbali wa kama mita 35 liliokolewa na Berko na kuwa kona.
Iliwachukua Yanga dakika ya 24 kulifikia kwa mara ya kwanza lango la Simba wakati Tegete alipokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini Kaseja alikuwa makini na kuudaka mpira huo wa juu.
Simba walikianza kwanguvu kipindi cha pili na katika dakika ya 51 washambuliaji wake waligongeana vizuri lakini walishindwa kumalizia baada ya kipa wa Yanga kuuwahi mpira huo kabla haujaleta madhara.
Joseph Owino aliikosesha Simba bao la kusawazisha katika dakika ya 84 baada ya kubaki na lango huku kipa wa Yanga akiwa ameanguka, lakini alipaisha mpira kutoka mita 12.
Kocha wa Yanga Costa Papic ambaye alitolewa uwanjani na muamuzi Ibrahim Kidue wa Tanga katika dakika za majeruhi alisema baada ya mchezo huo kuwa hakutarajia kabisa timu yake kucheza hovyo kiasi hicho.
"Kwa kweli sikutegemea kabisa Yanga kucheza vibaya namna ile lakini wapenzi hatimaye watafurahia ushindi pamoja na pointi tatu tulizoondoka nazo katika mchezo huu wa ugenini," alisema Mserbia Papic.
Papic pia alilalamikia kutolewa katika sekunde za mwisho akisisitiza kuwa hakufanya kosa lolote kwani alikuwa akitoa maelekezo kwa wachezaji wake kama inavyotakiwa.
Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri alisema baada ya mchezo huo kuwa walipoteza mechi hiyo kwasababu wachezaji wake walishindwa kufunga licha ya kupata nafasi nyingi, wakati Yanga walipata nafasi moja ya uhakika na kuitumia kuibukia na ushindi.
Timu zilikuwa:Simba;Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amri Kiemba, Amir Maftah, Juma Nyoso, Joseph Owino, Jerry Santo, Rashid Gumbo, Emmanuel Okwi, Patric Ochan/Mohamed Kijuso (dk.50) na Amri Kiemba.
Yanga: Yaw Berka, Shadrack Nsajigwa, Stephen Mwasika, Isack Boakye, Nadir Haroub Cannavaro, Ernest Boakeye, Athuman Idd Chuki/Godfrey Bonny (dk 65), Abdi Kassim/Yanha Tumbo (57), Jerry Tegete/Kigi Makassy (90), Nurdin Bakari.
You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - YANGA YAENDELEZA UBABE MWANZA
0 comments