MUUAJI wa kujitoa mhanga na wapiganaji wenye silaha wamevamia na kushambulia hoteli moja mjini Mogadishu, Somalia, taarifa za awali zikieleza kwamba wamewaua zaidi ya watu 32 wakiwemo baadhi ya wabunge, wanaokadiriwa kufikia sita. Mmoja wa wabunge aliyekuwepo katika hoteli hiyo ya Muna ambayo ni maarufu kwa viongozi wa serikali ya nchi hiyo alisema ilikuwepo miili ya watu waliofariki dunia kila mahali, na kuita tukio hilo mauaji ya halaiki. Mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema mara tu baada ya mashambulizi hayo kutokea yakiambatana ma mlipuko wa bomu aliona miili zaidi ya 27 ikiwa imelala kwenye baraza ya hoteli hiyo, ukiwemo wa mbunge mmoja. Alisema mlipuaji huyo wa kujitoa muhanga alijipenyeza na kujilipua karibu na sehemu ya mapokezi ya hoteli hiyo na kusababisha mapambani ya silaha yaliyochukua zaidi ya saa moja na nusu. Msemaji wa Umoja wa Afrika (AU), Meja Barigye Bahoku alisema haikuweza kufahamika idadi kamili ya waliouawa mara moja katika mashambulio hayo kwenye hoteli ya Muna, iliyopo umbali wa kilometa moja kutoka makazi ya rais, ambayo pia hutumi ana wabunge wanapokuwa mjini Mogadishu. Ofisa huyo wa usalama aliliambia shirika la habari la AFP kuwa hawana hakika ni kundi gani limefanya shambulio hilo lakini wanaamini ni wapiganaji wa kundi la al-Shabab walioingia katika hoteli hiyo wakiwa wamevalia sare za jeshi la usalama. “Ninachoweza kueleza kwa sasa ni kwamba wamewaua watu kadhaa wakiwemo wabunge. Nafikiri wabunge waliokufa wanafikia wanne,” alisema mmoja wa maofisa wa usalama wa serikali. Kundi la wapiganaji wa kiislamu la al-Shabab lilianza mashambulizi makali Jumatatu wiki hii, muda mfupi baada ya msemaji wake kutangaza vita kali dhidi ya vikosi vya kulinda amani vya AU, akisema kwamba askari hao zaidi ya 6,000 wanaoisaidia serikali dhaifu ya nchi hiyo ni “wavamizi”. Mkuu wa utoaji wa huduma za kusafirisha wagonjwa, Ali Muse alisema tangu Jumatatu wiki hii, mapigano yaliyoibuka katika mji huo wa Mogadishu yameripotiwa kusababisha vifo vya watu 40 na kujeruhi zaidi ya watu 130. Mwezi uliopita, al-Shabab ilidai kuhusika na milipuko miwili iliyosababisha vifo vya watu 76 nchini Uganda, ikidai mashambulizi hayo yalikuwa ni kulipiza kisasi kwa nchi hiyo kupeleka askari wake kwenye kikosi cha kulinda amani cha AU nchini Somalia. Mwaka jana, kundi hilo la al-Shabab lilishambulia kwa bomu la kutupwa kwa mkono dhidi ya hoteli hiyo mwaka uliopita na kuwajeruhi wabunge wawili. AFP |
You Are Here: Home - - Wabunge sita, raia 32 wauawa Somalia
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments