Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Maombezi ya Padre yazua balaa Mwanza

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

 
PADRE mmoja wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Bugando amezua balaa mkoani hapa kutokana na staili yake ya maombi ambayo imestua baadhi ya watu na kulalamikia ngazi za juu, kitendo kilicholifanya kanisa kumzuia kufanya mambo ya aina hiyo.

Padri huyo, Pius Tulanalwo Bilulu amekuwa akiendesha maombi, hasa kwa akina mama na wasichana wadogo, wengi wao wakiwa wanafunzi wa sekondari, kwa kuwashika sehemu mbalimbali za mwili, zikiwemo sehemu ambazo zinachukuliwa kuwa ni mwiko kufanywa na mtabibu asiye na taaluma maalum.

Gazeti la Mwananchi lilifanya uchunguzi wa tuhuma za huduma hiyo, iliyochukuliwa na baadhi ya wanawake kuwa ni unyanyasaji, kwa kutuma waandishi wake ambao waliigiza kuwa wana mapepo na hivyo kushuhudia jinsi padri huyo anavyoendesha huduma yake kwa wahitaji ambao hutakiwa kuvua nguo zote isipokuwa chupi, kwa maelezo kuwa unapokemea mapepo, hukimbilia kujificha kwenye sehemu ambazo si rahisi kufikiwa.

Maombezi ya padre huyo yamejizolea umaarufu mkubwa kwa waumini wa dini mbalimbali mkoani Mwanza na mikoa ya jirani kutokana na imani kuwa kila anayeombewa hufanikiwa shida yake.

Wanafunzi waliokuwa wakimiminika kwenye ofisi ya padre huyo kabla ya mwisho wa wiki iliyopita, walikuwa wakitafuta baraka kwa ajili ya mitihani ya kidato cha nne iliyoanza jana, na wanawake wengine huenda kutafuta maombezi ya matatizo sugu kama kutozaa.

Mwananchi pia iliongea na uongozi wa Kanisa Katoliki wa parokia hiyo na pia Jimbo Kuu la Mwanza ambao walithibitiosha kuwepo kwa maombi hayo na hatua walizochukua hadi sasa. Fuatilia simulizi ya mwandishi wetu kuhusu huduma hiyo:

NIKIWA katika jengo la ofisi ya Parokia, nilikuwa miongoni mwa watu zaidi ya 12 ambao tulikuwa tumeketi katika benchi kusubiria kuingia kuombewa na padre Bilulu.

Kwangu mimi hofu ilikuwa kubwa, hii ni kwa sababu sikuwa na matatizo ya kweli ambayo yalinipeleka kuombewa bali kilichokuwa kikinisukuma kwenda kuombewa ilikuwa ni kutaka kujua ukweli juu ya maombi hayo na vitendo ambavyo wanawake wamekuwa wakilalamikia kutendewa.

Nilianza kuwaangalia haraka haraka watu waliokuwa wameketi nje ya ofisi hiyo na kuwasaili. Niliona kati ya hao walikuwepo mabinti ambao walikuwa wamevalia sare za shule ambazo niliweza kuzitambua kuwa ni sare za sekondari, na baada ya kuwauliza walieleza kuwa walifika hapo kwa ajili ya kuombewa ili waweze kushinda mtihani wa kidato cha nne ambao umeanza jana.

Katika idadi ya watu tuliokuwa tukingojea zamu yetu, wanafunzi walikuwa sita ambao wote walikuwa wasichana, na watu wengine wazima tulikuwa sita. Lakini katika watu hao wazima sita wanaume tulikuwa wawili, mimi na mwandishi mwenzangu ambaye alilazimika kujitambulisha kama mjomba wangu.

Nilipowadadisi wanafunzi hao kuhusu huduma waliyoifuata, mmoja anayesoma kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Mwanza, alinijibu akisema: “Huyo mwenzetu ana mapepo, lakini sisi tumekuja kuombewa kwa ajili ya mtihani. Jana wenzetu wengine walitoka hapa kuombewa wakatueleza nasi tumekuja kupata baraka.”

Tulikaa kwa muda tukingoja kuingia kwa zamu na wakatio huo ndani ya ofisi ya padre kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akiombewa. Kiasi cha dakika 45 tangu tufike alitoka. Alikuwa ni mama wa makamo ambaye alikuwa ameambatana na mwenzake.

Nilianza kuwadadisi kwa macho kuona hali zao, lakini sikuweza kugundua zaidi ya kuona walikuwa wakionekana kama watu walio na uchovu na macho yao yakiwa yameiva kwa wekundi.

Muda kidogo baada ya kutoka watu hao, Padre Bilulu naye alitoka na kufuata nyuma yao. Alipotufikia, alisimama na kuanza kuuliza mmoja baada ya mwingine. Sikuwa na wasiwasi kwa vile hiyo ilikuwa ni mara yetu ya pili kurudi baada ya kuonana naye na kutupangia muda wa saa 10:00 kuwa ndio tumuone na muda ulikuwa umewadia.

Baada ya kuzungumza na wale wengine, aliwapangia muda na sisi tukaruhusiwa kuingia ndani kwa ajili ya kuonana naye. Nikiwa ndani hofu ilirejea tena kwa kuwa niliamini kuwa nilikuwa nikifanya kosa kwa mtumishi huyo wa Mungu kwa kusema uongo.

Taratibu kwa sauti ya kusaili alituuliza ni nini kilikuwa kikitusibu mpaka kufuata maombi kwake. Mwandishi mwenzangu akaeleza kuwa ninasumbuliwa na mauza uza kutokana na kuwa na ndoto za jinamizi usiku.

Nami nilimweleza kuwa nimekuwa katika ndoto za kutisha mara nyingi kila ninapolala na wakati mwingine nimekuwa nikiota natembea katika ziwa lenye maji mengi, lakini kila ninapoamka hujikuta nikiwa nimeingia ndani ya beseni la maji na kujiloweka katika maji. Pia nilimweleza kuwa nimekuwa nikiota nakula nyama, lakini kila ninapoamka nimekuwa nikijikuta nakula makaratasi ndani.

Tulimweleza kuwa nimejaribu kutibiwa hospitali pamoja na kulazwa wodi ya wagonjwa wa akili; nilimweleza jinsi nilivyokwenda kwa waganga wa tiba za asili, lakini imeshindikana na sasa nimeshakata shauri kurudi kwa Mungu na hivyo baada ya kusikia kuwa padre amekuwa akiombea watu, tuliamua kuja kwake kupata maombi.

Mara baada ya kumweleza hayo, Padre Bilulu alieleza kuwa maelezo yetu yanaonyesha kuwa ninasumbuliwa na mapepo. Alieleza kuwa hakukuwa na njia nyingine ya kuniponya zaidi ya kuniombea ingawa alisema atafanya hivyo kwa sababu ya kuona nikiteseka lakini alikuwa amezuiliwa na wakuu wa kanisa.

Alianza kutueleza kuwa katika utaratibu wake, maombi yake yamekuwa yakifanyika kwa kugusa sehemu kadhaa za mwili na kwamba ni lazima yafanyike ukiwa umevua nguo zote isipokuwa chupi. Alidai (huku akionyesha kiganja chake) kuwa amekuwa akitumia mkono wake kutoa mapepo kwa vile mkono wa binadamu unayo nguvu inayohesabika kuwa ni 384 na mikono yake imekuwa ikitoa miale katika vidole.

Maelezo hayo yalinitisha kiasi nilifikiri kughaili kuendelea na mpango wangu wa kutaka kuchunguza maombi hayo. Hata hivyo nilihofia kurejea kazini kwangu nikiwa sina habari kamili na kwa vile nilikuwa katika uchunguzi, nilitambua kuwa nilipaswa kuvumilia ili kuona na kuthibitisha ukweli juu ya tuhuma kuwa maombi ya padre yamekuwa yakihusisha kushika watu sehemu mbalimbali zikiwemo za siri.

"Huwezi kumwombea mtu bila kumshika sehemu zenye mapepo. Ninawashika kukemea hayo mapepo wakati mwingine yanakimbilia sehemu za siri... sasa kumbe kwa padre kumshika mwanamke sehemu za siri ni kumdhalilisha,” alihoji padre huyo.

Baada ya maelezo hayo aliinuka na kufunga malango kwa funguo na kisha kunitaka nivue nguo zote. Kwanza nilitulia; sikuwa kama ninayeamini masikio yangu. Kitendo hicho kilimfanya padre huyo kuongea kwa ukali kidogo akisema "amka uvue nguo! pepo wee’. Nikatii na kuanza kutoa nguo.

Baada ya kumaliza kuvua na kubaki nikiwa na nguo ya ndani (chupi aina ya boxer), alinielekeza kukaa katika stuli na kuweka mikono yangu katika katika magoti lakini ikiwa imefunguliwa kama mtu anayeomba. Alichukua kitabu chake maalum na kumuomba mwandishi mwenzangu tushiriki wote katika maombi ya kukemea mapepo.

Akaanza ibada. Ilichukua kama dakika 45 kisha alitoka nje ya ofisi na kwenda katika chumba kingine na kurudi huku mikono yake ikionekana kupakwa mafuta. Alianza kuipitisha usoni, mabegani utosini, mgongoni na kisha tumboni na baada ya kumaliza hatua hiyo alitoka tena nje na kurejea akiwa na mfuko.

Katika mfuko huo, nilibaini kuwa kulikuwa na nguo maalum ambazo alianza kuzitoa, kwanza alitoa blanketi mbili na kutandika katika sakafu ya ofisi. Baadaye akatoa kitenge cha njano ambacho alikitandika juu ya blanketi hizo mbili na kisha kuniamuru kulala kifudifudi juu yake.

Kwa hakika muda wote huo sikuwa nimeona kitu chochote kikinipata toka nifanyiwe ishara zote za maombi. Sikukata tamaa, lakini kichwani nilikuwa nahangaika na mawazo. 

Pengine angeweza kunibaini kuwa nilikuwa nimekwenda hapo kwa ajili ya kumpeleleza, na hofu yangu nyingine ilikuwa ni kuwa huenda nilikuwa na mapepo ambayo yangeweza kuibuliwa siku hiyo. Niliamua kusubiri.

Baadaye alitoka tena nje ya ofisi na kuniacha nikiwa nimelala pale sakafuni, hatua hiyo ilimpa mwanya mwenzangu kunieleza kuwa itanibidi kujifanya nina mapepo kila anaponiombea ili tubaini atafanya nini. 

Nilikubali na baada ya kurudi alianza kunipuliza sehemu za matiti kwa mdomo wake na baadaye kuninyonya. Alihamia tumboni na kufanya vivyo hivyo katika kitovu changu pia.

Kitendo hicho kinishangaza kiasi cha kubaki nikiwa nimeduwa na akaanza kupaza sauti akisema 'tokeni…tokeni…tokeni mapepo nyie!’

Hapo ndipo niliona wakati wangu na mie wa kujifanya kuwa mapepo hayo yalikuwa yakitoka ambapo nilianza kuigiza kwa kupigapiga miguu na mikono. 

Katika hatua ya kustaajabu alishusha nguo yangu ya ndani na kunishika kende zangu huku akizichezesha na kusema: ‘Hata kama mmejificha katika sehemu hizi (sehemu za siri) tokaaa.’

Nilipiga piga miguu na kutupa mikono nikifuata mifano ya wenye mapepo ambao nimekuwa nikiwaona katika filamu za Kinigeria na baadaye kutulia tuli. Kitendo hicho kilimfanya padre huyo kuniita kwa sauti jina langu baada ya kumuuliza niliyekuwa naye.

Aliniita jina nami nikaitika kwa sauti ya unyonge kuonyesha nilikuwa katika hali ya kuchoka na fadhaa. Kisha akaniuliza nilikuwa nikijisikia vipi. 

Nilimjibu kuwa nilikuwa nikijisikia mwepesi sana na mwili kama ambao umetua kitu kizito. Alieleza kuwa nadhani sasa tumefanikiwa katika maombi yetu, lakini akaongezea kuwa inanipasa kuhakikisha nasali kila siku na ikiwezekana niwe ninafika kwake kwa ajili ya maombi.
Tags:

0 comments

Post a Comment