IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Hussein Issa,Phinias Bashaya,na Hawa Mathias
MSAJILI wa vyama vya Siasa nchini,John Tendwa ameshauri wafungwa waruhusiwe kupiga kura katika uchaguzi mkuu 2010.Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, Tendwa alisema kuwa wafungwa nao wana haki ya kupiga kura kama raia wengine.
"Nao wanahaki ya kupiga kura, sasa kwanini wasiruhusiwe kupiga kura ikiwa ni raia wa Tanzania, ina maana mtu kufungwa anapoteza haki zake zote?"alihoji.
Aliongeza kuwa anachokijua yeye ni kuwa wafungwa wasiohukumiwa kifungo cha maisha au hukumu ya kifo, wana haki ya kupiga kura.
Alisema nchi kama Afrika ya Kusini, Botswana na Lesotho kwanini waruhusu wafungwa wao wapige kura sisi huku tushindwe?.
Alibainisha kuwa katika nchi hizo wafungwa wasioruhusiwa kupiga kura ni wale waliohukumiwa kifo na vifungo vya maisha utaratibu ambao pia unaweza kutumika hapa nchini.
"Wapo wananchi waliojiandikisha kabla ya kuhukumiwa vifungo, lazima utaratibu uwepo kwani watu hawa baadaye watatokaa na kwenda kwenye jamii"alisema Tendwa.
Akizungumzia sheria ya gharama za uchaguzi iliyoanza kutumika Aprili Mosi mwaka huu, msajili huyo alisema ofisi yake ina ushahidi wa picha za video ambazo ziko kwenye CD zikionyesha matumizi ya magari ya serikali kipindi cha uchaguzi.
"Ofisi ya msajili imepokea taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa kupata CD zinazoonyesha wagombea wanavyopeana rushwa na matumizi ya gari la serikali limebeba nyama ya nyati na vitenge kuwapelekea wanakijiji wa eneo fulani"alisema Tendwa.
Alisema baada ya ushahidi huo watakaodhibitika wataondolewa kwenye uchaguzi hata kama zitakuwa zimebaki siku chache na hata wale watakaoshinda watawekewa pingamizi na ofisi ya msajili.
Tendwa alisema kuwa ofisi yake haitavumilia vitendo vya rushwa kama ilivyokuwa mwaka 2005 kuanzia mchakato wa kura za maoni ndani ya vyama aliosema ulitawaliwa na rushwa ya wazi kuanzia ngazi ya udiwani hadi wagombea urais.
Alisema wabunge wengi hawakupenda kuanzishwa kwa sheria hiyo na kudai kuanguka kwa robo tatu ya mawazi katika kura za maoni na robo tatu ya sura mpya katika nafasi ya wabunge ni matokeo ya ukali wa sheria ya gharama za uchaguzi.
Alidai mawaziri na wabunge wengi walioangushwa katika kura za maoni walibanwa na sheria na kudai wananchi walishawachoka ingawa kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo walijihusisha na vitendo vya rushwa kuwashawishi wapigakura.
You Are Here: Home - - Tendwa awapigia debe wafungwa wapige kura
0 comments