Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Phiri AikimbiaSimba atua Azam miaka miwili

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Na Erasto Stanslaus
KOCHA Mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri ameitema rasmi timu yake na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Azam FC.

Phiri aliondoka jijini Dar es Salaam ghafla Jumatatu wiki iliyopita kwenda Zambia, akidai kuwa amepata matatizo ya kifamilia na alitarajiwa kurejea nchini Alhamisi ya juma hilo, lakini alishindwa kufanya hivyo baada ya kudai kuwa alikosa ndege.

Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa kocha huyo taarifa zilienea kuwa, Azam wametumia mwanya huo kumpata Phiri ambaye aliiongoza Simba kutwaa ubingwa bila kufungwa msimu uliopita.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa klabu ya Azam, tayari klabu hiyo imemalizana na Phiri na wanafanya mpango ili aweze kusaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.

Azam ambao walianza kumwinda kocha huyo kwa muda mrefu lakini ilishindikana kutokana na msimamo wake wa kutotaka kuifundisha timu nyingine ya Tanzania, lakini ujumbe uliosafiri hadi Zambia kumfuata umefanikiwa kumnasa kocha huyo ambaye mkataba wake na Simba utamalizika Novemba mwaka huu.

“Kweli tayari tumemalizana na Phiri, kilichobaki hapa ni kusaini mkataba wa miaka miwili na sasa tutafanya utaratibu wa kufuatilia mkataba wake ambao ametuambia unamalizika mwezi ujao,” alisema kiongozi huyo.

Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema, anachofahamu kuwa kocha angerudi jana mchana na moja kwa moja atajiunga na timu yake iliyopo jijini Mwanza kwa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Yanga utakaopigwa Oktoba 16, mwaka huu.

“Hizo taarifa sizijui, ninachojua mimi na uongozi wa Simba kuwa Phiri ni kocha wetu na ana mkataba unaomalizika Novemba na leo (jana) tayari tumemkatia tiketi ya kuja moja kwa moja Mwanza,” alisema Ndimbo kwa njia ya simu kutoka Mwanza.

Hata hivyo, Championi Jumatatu lilikuwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jana likisubiri kuona kama Phiri atatua lakini hadi muda wa saa 8:00 mchana ambao uongozi wa Simba ulitangaza atarejea, kocha huyo hakufika na taarifa ambayo Championi iliipata uwanjani hapo ilisema kuwa ndege itawasili saa 3:00 usiku.

“ Ndege imepata hitilafu itawasili usiku saa 3:00,” alisema Katibu Mkuu wa Simba Evodius Mtawala aliyekuwa uwanjani hapo.

Habari zaidi zinasema, hata kama Phiri angerejea jana na kuungana na Simba, kocha huyo atajiunga na Azam FC baada ya kumalizika kwa mkataba wake, Novemba mwaka huu.
Tags:

0 comments

Post a Comment