Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini, Leodgar Tenga naye akionyesha kustaajabu baada ya nyimbo hizo kugoma mbele ya rais Jk juzi Jumamosi.
Na Richard BukosRAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, juzi Jumamosi alimvaa Rais wa shirikisho la Soka nchini, Leodegar Tenga, baada ya mafundi mitambo wa uwanja wa taifa kushindwa kucheza nyimbo za Taifa la Morocco na Tanzania, kabla ya mechi dhidi ya timu hizo kuanza.
Tukio hilo lililotokea Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Kikwete alikuwa mgeni rasmi huku CD ya nyimbo za Taifa iligoma kucheza na kuwafanya viongozi hao kusimama uwanjani kwa dakika nane.
Wakati mafundi wakihangaika, Rais Kikwete alionekana kumlaumu Tenga na kumwambia amekerwa na tabia hiyo kwani si mara ya kwanza suala hilo kutokea uwanjani hapo.
“Hii si mara ya kwanza ni mara ya pili naona uzembe kama huu ukitokea uwanjani hapa,” alisema Kikwete ambaye anaomba ridhaa tena kwa wananchi ili aweze kuongoza kwa miaka mitano ijayo.
Kufuatia tukio hilo, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Florian Kaijage alimuomba radhi Rais Kikwete na wengine wote kufuatia tukio hilo.
0 comments