Meneja wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,
Abdulrahaman Kinana
WAKATI mgombea urais, Dk Willibrod Slaa atapata fursa ya kujibu maswali ya wananchi Jumamosi kwenye kipindi maalum cha ITV, katibu huyo wa Chadema juzi alipambana vikali na meneja wa kampeni za CCM, Abdulrahaman Kinana kwenye kipindi cha "Tuongee Uchaguzi Mkuu" cha kituo cha Star TV.
Juvenalius Ngowi, muaandaaji wa mdahalo wa Jumamosi ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa And Vox Media Center ambayo inashirikiana na East Africa Business and Media Training Institute, alisema mdahalo huo utaongozwa na mwandishi wa habari aliyebobea, Jenerali Ulimwengu akisaidiana na Rose Mwakitwange.
"Mdahalo utakuwa na waalikwa 200 kutoka makundi tofauti ya kijamii na watauliza maswali ya moja kwa moja yatakayojibiwa na Dk Slaa," alisema Ngowi.
Alisema kuwa baada ya mdahalo huo utafuatia mdahalo wa mgombea wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
"Pia tuna mpango huo na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete japokuwa CCM hawajakataa au kukubali ombi letu," alisema.
Katika mdahalo wa juzi, Dk Slaa alirudia wito wake kwa mafisadi kukaa chonjo, akisema walioficha fedha zao nje ya nchi wazirudishe mara moja kabla ya kuingia Ikulu.
CCM imekataza wagombea wake kushiriki kwenye midahalo yoyote isipokuwa kwa ruhusa maalum, lakini juzi Kinana, ambaye hagombei nafasi yoyote, alilazimika kuingia kwenye mdahalo dhidi ya Dk Slaa, ambaye anaonekana kutoa upinzani mkali kwa chama hicho tawala.
Mchuano huo ulikuwa mkali kutokana na maswali yaliyokuwa yakiulizwa na waendeshaji wa kipindi hicho na wakati fulani Kinana alionekana kukwepa baadhi ya maswali, likiwemo la sababu za kushiriki kwenye mdahalo huo badala ya Kikwete ambaye anagombea urais.
Wananchi waliopiga simu walitaka kuona Dk Slaa akipambana na mgombea mwenzake na kuhoji sababu za KIkwete kujibiwa maswali na Kinana, ambaye hata hivyo alikwepa kujibu swali hilo.
Katika mdahalo huo, Dk Slaa alilalamika kuwa upinzani umekuwa ukiibiwa kura katika chaguzi nyingi tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini Kinana alikanusha madai hayo ya wizi wa kura, huku akisisitiza kuwa CCM imekuwa ikishinda kihalali katika chaguzi zote zilizopita.
“Kauli za wizi wa kura ni za upotoshaji kwa kuwa ndani ya chumba cha kupigia kura huwa kunakuwa na wakala wa kila chama na mara baada ya matokea kukamalika anatia saini, iweje wasema CCM wanaiba kura,” alisema Kinana.
Dk Slaa akimtania baba yake mzazi mzee Peter Slaa kwa kumchezea ndevu baada ya kumaliza kuwahutubia wananchi wa Karatu
Lakini Dk Slaa alisema anao ushahidi wa tuhuma hizo na kuitaka CCM kutokana kuhusika na vitendo hivyo.
“Hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, kanda ya Arusha katika kesi ya uchaguzi inaeleza wazi kuwa CCM waliniibia kura 3,000 mimi mwenyewe kwenye Jimbo la Karatu licha ya ukweli kwamba zililindwa. Hivyo namshangaa Kinana anaposema hakuna wizi wa kura,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alifafanua kuwa wizi wa kura umekuwa ukifanyika katika karatasi ya fomu ya matokeo (Result Form) na siyo kwenye kiboksi cha kutumbukiza kura wakati wa kupiga kura na kusema wizi huo huwa vigumu kugundulika.
Alitaja mbinu tatu ambazo hutumika kuwa ni kutumia fedha kurubuni mawakala, kubadilisha namba katika fomu ya matokea(Result Form) na kundaa vituo hewa vya kupigia kura.
Alisema chama chake kitayakubali matokea lakini akasisitiza ni yale ambayo hayana dosari wala mazingira ya wizi wa kura.
Katika mdahalo huo uliokuwa mkali ulisababisha Kinana kutoa kauli kuwa ushindi kwa CCM si lazima tofauti na wagombea mbalimbali wa chama hicho ambao wamekuwa wakieleza kuwa "ushindi kwa CCM ni lazima".
Kinana aliitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akijibu hoja ya Dk Slaa aliyeituhumu CCM kuandaa vijana wanaojulikana kama Green Guard kuwatumia kufanya fujo ili kufanikisha kauli mbiu ya "ushindi lazima".
"Dk Slaa ni kaka yangu. CCM ina wajibu wa kuhakikisha amani na utulivu; vyama vyote vina wajibu wa kuelimisha wanachama wao, kuendesha kampeni za kistaarabu. Ushindi si lazima... jukumu letu sote ni kuhakikisha amani na utulivu wa nchi hii.
Agenda yetu CCM ni kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo ndani ya nchi; tuelekeze wanachama wetu kuhakikisiha udini, ukabila havina nafasi," alisema.
Kinana alikanusha tuhuma za CCM kuwapa mafunzo ya kijeshi vijana hao na badala yake akaituhumu Chadema kuwa ina kundi la vijana wanaoitwa Red Guard ambao hufanya fujo.
Alisema: “Green Guard yetu siyo jeshi, lakini Chadema wana vijana pia wajulikanao kwa jina la Red Guard na tumekuwa tukiwaona kwenye mikutano ya Chadema wakilinda na kupiga watu. Tuna ushahidi kuwa walimpiga mama mmoja aliyekwenda kwenye mkutano wao akiwa amevalia nguo za kijani.”
Katika mahojiona hayo ambayo yalionekana kama mapambano kati ya CCM na Chadema, meneja huyo wa kampeni wa CCM alizishambulia ahadi za Dk Slaa kuwa hazitekelezeki huku akisistiza ahadi zinatolewa na Kikwete kuwa ndizo zinazotekelezeka.
“Kama Dk Slaa angekuwa ana nia ya kweli ya kutoa elimu na afya bure kwa Watanzania, angeanza kwa kutoa huduma za afya bure katika Taasisi ya CCBRT ambayo yeye ni mwenyekiti kwa kuwa katika taasisi hiyo serikali hutoa ruzuku ya Sh1 bilioni,” alisema Kinana.
Alisema Kikwete, ambaye kwa sasa anatetea nafasi hiyo kwa mara ya pili, alitekeleza ahadi zilizopita kwa asilimia 90 na kusisitiza ahadi zilizobaki asilimia 10 atazimalizia na kuanza kutekeleza zile alizoziahidi upya.
“Katika kipindi kilichopita Kikwete alitekeleza ahadi zake kwa silimia 90, wakati akiingia madarakani kulikuwa na wanafunzi vyuo vikuu 38,000 lakini leo kuna wanafunzi 118,000 haya ni mafanikio makubwa,” alisema Kinana.
Alisema serikali ya CCM inatarajia kumaliza tatizo la walimu katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Naye Dk Slaa alieleza kuwa ahadi yake ya kupunguza gharama za saruji ataipa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na nyumba bora za kuishi.
Dk Slaa alimshangaa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Deodorus Kamala aliyepinga hilo kuwa haliwezekani akisema hiyo inaonyesha watu wengi wanaopewa nafasi za kuiwakilisha Tanzania kwenye nafasi mbalimbali za kimataifa hawaweki mbele masilahi ya kitaifa.
“Ndiyo sababu mikataba mingi waliyoingia, ikiwamo ya madini, haiwanufaishi Watanzania,” alisema Slaa.
Dk Slaa alisema akiingia Ikulu atahakikisha mikataba yote mibovu inafumuliwa na kufanyiwa kazi upya kwa lengo la kuhakikisha wananchi wananufaika na rasimali zao.
Alisema Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kulipa kodi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisema kuwa inalipa asilimia 18, ikifuatiwa na Kenya asilimia 16 wakati Uganda inatoa asilimia 15.
Alisema katika umoja huo pia kuna kipengele kinachotoa ruhusa kwa nchi kutolipa gharama hizo hadi pindi inapokamilisha jambo fulani kuhusu wananchi wake na kwamba hata yeye ndivyo atakavyofanya.
“Tanzania inalipa kodi kubwa kuliko nchi nyingine Afrika Mashariki. Nikiingia Ikulu haitalipa kodi hadi wananchi wajenge nyumba bora na hiyo ndiyo dira ya Chadema," alisema.
Kuhusu Hosptali ya CCBRT kushindwa kutoa bure licha yeye kuwa mwanzilishi na mwenyekiti, Dk Slaa alisema hali hiyo inatokana na yeye kutokukusanya kodi toka kwa wananchi.
Alisema kama angekuwa anakusanya kodi ambazo ni fedha nyingi, angezitumia kuendesha hospitali hiyo ambayo hutumia Sh 6 bilioni kwa ajili ya uendeshaji wake.
“Taasisi ya CCBRT ambayo mimi ni mwenyekiti wake inatumia Sh6 bilioni kwa mwaka, serikali inatoa Sh1 bilioni hiyo ndiyo sababu wananchi wanalazimika kuchangia huduma,” alisema Dk Slaa.
Alisema kama ataingia madarakani na kuongeza serikali kukusanya mapato ya nchi huduma alizosema atazitoa bure, atatekeleza kwa kuwa atadhibiti ukusanyaji wa mapato na kuondoa matumizi mabovu.
Kuhusu kupunguza kodi ya saruji na vifaa vya ujenzi, alisema atatekeleza kwa vitendo katika mkakati wake wa kufuta nyumba zinazoezekwa kwa udongo.
0 comments