Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk Shein kujenga chuo kijijini kwa Maalim Seif

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Ali Mohamed Shein jana aliahidi kujenga vyuo viwili wilayani Wete ambako anatoka mpinzani wake kwenye kinyang'anyiro hicho, Seif Sharif Hamad.

Moja ya vyuo hivyo ni chuo cha ufundi alichosema kitajengwa kwenye Kijiji cha Mtambwe ambako ni nyumbani kwa mgombea huyo.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye mkoa huo wa Kaskazini, Shein alisema lengo la ujenzi huo ni kupeleka elimu katika maeneo hayo, akisema kuwa elimu ni msingi wa maendeleo.

"Nitajenga chuo cha ualimu kwenye Kijiji cha Mchagamdogo lakini pia nitajenga chuo cha ufundi katika Kijiji cha Mtambwe," alisema makamu huyo wa rais wa Muungano anayemaliza muda wake.

Akishangiliwa na umati wa watu waliojitokeza kusikiliza sera zake, Dk Sheini aliahidi kumalizia majengo ya shule katika majimbo ya Ole na Kojani.

Alisema ndani ya miaka mitano atahakikisha ahadi zake zinatekelezwa, ikiwemo ya kupeleka umeme vijijini.

Awali mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini, Mberwa Hamad Mberwa aliwataka wapemba walio Bara kuwashauri wenzao walio huku kuichagua CCM sababu ndio iliyowafanya waweze kuishi katika eneo hilo.

"Wenzetu wa Kojani, Kambini, Mchangamdogo na Kiungoni wamezagaa katika maeneo ya Buguruni huko Bara na wamefika huko na kujituma. Kwa kweli wamefanikiwa, lakini wanapaswa kutambua kuwa kinachowafanya wabaki huko ni CCM na Muungano," alisema Mberwa.

Mberwa alisema CCM ndio inayodumisha Muungano na kwamba Muungano ndio uliowapeleka huko hivyo wana kila sababu ya kurudi kwao kuja kuwasaidia wenzao waliobaki kwa kuwashauri kuichagua CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alisema watu hao wanapaswa kukumbuka fadhira kwa kuichagua CCM ambayo alidai kuwa ndiyo muasisi wa Muungano uliowezesha wenzao kuhamia Bara.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo alimweleza Mgombea urais wa chama hicho adha inayokikabili Kisiwa cha Kojani kutokana na kukosa kivuko.

"Katika kipindi cha miaka mitano tumetekeleza sera za CCM kwa kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia. Bado barabara na kivuko naamini wewe utaweza," alisema Mberwa.

Mberwa alielezea kisa kilichowahi kumkuta alipokuwa akivuka katika kisiwa hicho na kuzama kutokana na ubovu wa kivuko hicho.

"Safari moja mimi na mwalimu mmoja tulikwedna kutoa elimu Kisiwa cha Kojani; wakati wa kurudi tulizama kwenye maji hadi tulipokuja kuokolewa," alisema Mbrewa.

"Lakini ninakuamini wewe unaweza kulitatua hili," alisema.
Dk Shein alikubali kuwa kama atachaguliwa atahakikisha kivuko hicho kinapatikana.

Naye naibu katibu wa CCM wa Zanzibar, Salehe Ramadhan Feruz aliwataka wakazi wa Wete kuichagua CCM baada ya kuiacha kwa kipindi cha miaka mitano kwa sababu imetekeleza ahadi zake.

"Majimbo yote ya wilaya hiyo hayaongozwi na CCM... safari hii tunaomba mchague Feruz awe mbunge," aliomba Feruz.
Tags:

0 comments

Post a Comment