Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mahakama yaamuru Chenge akamatwe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter BAADA ya kutoonekana mahakamani jana , Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kinondoni, Dar es Salaam imeamuru kukamatwa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Chenge ambaye yuko nje kwa dhamana akikabiliwa na mashitaka ya kusababisha vifo vya watu wawili, jana hakufika mahakamani hapo wala mdhamini wake bila taarifa.

Amri hiyo ilitolewa mahakamani hapo na Hakimu Sundi Fimbo, baada ya mwendesha mashitaka, Richard Rweyongeza kusoma maelezo ya awali ya mashitaka yanayomkabili mshitakiwa.

“Haijalishi kuwa mshitakiwa yuko kwenye kampeni au wapi, Mahakama haitambui jambo lolote kuhusu kampeni, hivyo kwa kuwa hajahudhuria mahali hapa, inabidi akamatwe kwa kushindwa kutekeleza amri ya Mahakama,” alisema Hakimu Fimbo.

Alifikia uamuzi huo baada ya masharti ya dhamana ambayo yanamtaka mshitakiwa kufika mahakamani siku ya kesi aliyopangiwa na bila hivyo atoe taarifa za kutofika kwake mahakamani.

Kwa niaba ya Hakimu Mkazi, Kwey Rusema, ambaye anasikiliza kesi hiyo, Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5 mwaka huu itakaposikilizwa tena.

Ilidaiwa kuwa Machi 27, 2007 mshitakiwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux namba T 512 ACE alimgonga mwendesha pikipiki ya magurudumu matatu - bajaj jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya Beatrice Costantine na Victoria George.

Awali baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama ilisema Chenge ana kesi ya kujibu na alitakiwa kufika mahakamani jana kuanza kusikiliza utetezi wake.

Chenge ambaye anatetea ubunge Bariadi Magharibi alisema ataleta mashahidi wawili ambao ni yeye na shahidi mwingine ambaye hakutajwa mahakamani.

Aidha, katika kesi hiyo shahidi wa mwisho wa upande wa mashitaka, Raymond Njeje, alidai kuwa stika ya bima aliyokuwa akitumia Chenge si mali yake.

Njeje alidai kuwa, stika hiyo ni ya gari namba T 571 AKH aina ya Toyota RAV4 nyeusi na si ya Toyota Hilux iliyosajiliwa kwa namba T 513 ACE ambalo alikuwa akiendesha Chenge wakati anapata ajali.

Alidai stika hiyo namba 11919156 inamilikiwa na Evarist Ses iliyotolewa mwaka 2007 kwa ajili ya matumizi ya miezi mitatu kuanzia Juni 29 hadi Septemba 28.

Gazeti hili lilimtafuta Chenge kwa njia ya simu jana akasema kuwa hayuko tayari kuzungumza chochote kwa sasa kuhusu kesi ambayo ipo mahakamani.

Mgaya Kingoba, anaripoti kutoka Bariadi kwamba Chenge alikuwa katika kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete zilizofanyika Bariadi Mashariki mkoani Shinyanga.

Katika kampeni hizo, Chenge ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alikuwa akizungumza akichanganya Kiswahili na Kisukuma, akiwataka wakazi wa jimbo hilo kutofanya makosa tena, akitolea mfano wa mazuri yaliyofanywa na chama hicho jimboni mwake.

Alikuwa akimnadi mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Bariadi Mashariki, Martin Makondo baada ya Rais Kikwete kumaliza kumnadi.

Mapema katika mkutano huo, Kikwete aliwaambia wananchi wa Bariadi Mashariki, kwamba miaka 15 waliyochagua Mbunge wa upinzani inatosha na sasa wakipe chama hicho nafasi ya kuongoza Halmashauri yao na wataona mabadiliko makubwa zaidi.

Alisema chini ya falsafa ya Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi, wananchi hao wana kila sababu ya kuichagua CCM kuongoza jimbo hilo na wataona tofauti na walivyokuwa na mbunge wa mpinzani.

Bariadi Mashariki imekuwa chini ya UDP, kuanzia mwaka 1995; kwanza chini ya Danhi Makanga ambaye baadaye aliihama na
kujiunga na CCM na sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kibondo na sasa linaongozwa na John Cheyo, Mwenyekiti wa UDP.

“Mmekuwa katika upinzani kwa muda mrefu, mnapaswa kuanza upya … miaka 15 chini ya upinzani inatosha, tupeni muone tofauti. Kila siku mboga ya aina moja inachosha,” alisema Rais Kikwete wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika kata ya Lagangabilili mjini hapa.

“Ukitupa miaka mitano tu, utaona kuwa mlichelewa sana. Fikirieni kuwa na Halmashauri ya CCM, wilaya mpya, mtaona tofauti yake.

Akimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Martin Makondo, alisema ni kijana mbichi, anayeleta uhai mpya katika wilaya mpya kwa sababu ni mtu aliyekamilika.

Kaulimbiu ya Uchaguzi ya CCM Bariadi Mashariki ni Mkoa mpya, Wilaya mpya na Mbunge mpya.

Makondo alisema anajua mahitaji ya wakazi wa jimbo hilo na
wanachotakiwa ni kuichagua CCM kuongoza ili kuendeleza mazuri
iliyoyafanya bila kuwa na mbunge wake kwa miaka 15.

Rais Kikwete jana alifanya mikutano katika miji ya Lagangabilili (Bariadi Mashariki); Mwandoya (Kisesa); Mwanhuzi (Meatu); Lalago, Maswa Mjini na Malampaka (Maswa); Mhunze (Kishapu) na kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga Mjini. Leo anaendelea na majimbo mengine mkoani hapa
Tags:

0 comments

Post a Comment