IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SERIKALI imekubali kuwepo kwa uraia wa nchi mbili kwa Watanzania walioko nje ya nchi na kwamba wasichukuliwe kama wasaliti.
Kutokana na hatua hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iko kwenye mchakato wa kuwasilisha muswada kuhusu uraia wa nchi mbili kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema juzi bungeni mjini hapa, kuwa anafanya mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata baraka zao kutokana na suala hilo kuwa la Muungano.
Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Waziri Membe alisema siyo dhambi, Watanzania kutafuta riziki nje ya nchi na ni haki yao kubaki na uraia wa Tanzania.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania, kupatiwa haki yao ya msingi kwani licha ya kuwa ni manufaa kwao pia ni manufaa kwa nchi kutokana na fursa ya kuongeza pato la taifa.
“Tusiwaangalie Watanzania walioko nje ya nchi kama wasaliti, watu hawa ni raia wema lakini walikwenda kutafuta riziki tu ili wachumie juani na kulia kivulini, hivyo tunapowafutia uraia wa ndani hatuwatendei haki,” alisema Waziri Membe.
Alisema kwa kawaida watu wanaoweza kufutiwa uraia wa nchi zao ni wale wanaoondoka nchini kwa sababu mbalimbali kama vile uhaini au wakimbizi kutokana na vita.
Alisema kama Tanzania imeweza kutoa uraia kwa wakimbizi 169,000 kutoka Rwanda na Burundi, haiwezi kushindwa kuwabakishia uraia wao wananchi wake wanaokwenda kutafuta nje ya nchi.
Kuhusiana na suala la wakimbizi kutoka nchi jirani na kuingia nchini, Waziri Membe alisema Tanzania imechoka kupokea wakimbizi na kuonya kuwa wakimbizi wowote watakaoingia nchini hivi sasa kutoka Burundi, watakamatwa na kurejeshwa kwenye nchi zao.
Alisema hivi karibuni nchi ya Burundi, ilifanya uchaguzi ambapo vyama 12 vilivyosusia uchaguzi na kupatikana kwa taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa nchi hizo wameingia msituni.
“Tanzania siyo kichaka cha kuficha watu wahalifu, kiongozi yeyote wa chama kilichosusia uchaguzi atakayekimbilia nchini, atakamatwa na kurejeshwa kwao,” alisema Waziri Membe.
You Are Here: Home - - Serikali yaridhia uraia wa nchi mbili
0 comments