Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Lipumba ataka mdahalo na Kikwete

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba ameshauri kuwepo na mdahalo wa wagombea urais ili kila mgombea aweze kuainisha mambo ya msingi atakayoyasimamia.
Profesa Lipumba ambaye pia ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CUF, alitoa ushauri huo juzi jijini Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea urais wa chama hicho kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Alisema ni muhimu kwa wagombea wa urais wa vyama vyote kuwepo na mdahalo utakaoainisha ni mambo yepi ya msingi ambayo atayasimamia na kuwaletea faida Watanzania.

“Ni muhimu kuwepo na mdahalo na si ubabaishaji ili uweze kuwaelezea Watanzania ni jambo gani ambalo utalisimamia na kuwatekelezea wananchi ili nao waweze kupata ufahamu na muelekeo wa nchi yao jinsi inavyokwenda,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema hali ya nchi kuwa mbaya kwa kukithiri kwa umaskini na kupanda kwa bei ya bidhaa ni dalili tosha itakayowawezesha Watanzania kuzinduka na kuacha kuichagua CCM kwa kuwa imewalaghai mambo mengi ya msingi.

“Watanzania wanatakiwa kuzinduka kuacha kumchagua tena Rais Kikwete; wanatakiwa kuwa makini na maamuzi kwa kuwa hali ni mbaya hakuna kitu walichokifanya na sasa akiingia tena katika kipindi hiki cha miaka mitano ni cha lala salama cha “Chukua chako Mapema” kama CCM ilivyo kawaida yake,” alisema Profesa Lipumba.

Mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma ni mchumi alisema kuwa haoni sababu ya kumchagua Kikwete kwa kuwa hali ya maisha ni ngumu, vijana hawana ajira walizoahidiwa kuwa ni hewa, bei za vyakula zimepanda hivyo kusababisha wananchi kula mlo mmoja kwa siku.

Naye mgombea urais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema ana uhakika asilimia 90 ya Wazanzibari watapiga kura ya ndiyo kuunga mkono uanzishwaji wa serikali ya mseto.

Alisema anaamini kila Mzanzibari atakuwa amechoshwa na migogoro ya kisiasa, mikwaruzano ya hapa na pale hivyo ni vema wakaamua kuundwa kwa serikali ya mseto itakayoleta faida kwa Wazanzibari na taifa zima kwa ujumla.
Tags:

0 comments

Post a Comment