IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAGOMBEA watano miongoni mwa 11 walioomba kuteuliwa kuwania nafasi ya urais visiwani Zanzibar, wamependekezwa kwa kupewa alama za juu na kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Tanzania Daima Jumapili imebaini.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimesema kuwa wagombea hao walipewa nafasi hizo baada ya kujadiliwa na kikao hicho kilichokutana jana mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake, Rais Amani Abeid Karume.
Waliopendekezwa kwa kupata alama za juu ni pamoja na Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamuhuna na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman.
Vyanzo vya habari kutoka kwa wajumbe wa kikao hicho vimeeleza kuwa kazi ya kupendekeza majina hayo ilikuwa ngumu kutokana na wengi kuwa na sifa.
Pamoja na majina hayo matano kupata alama za juu, bado majina ya wagombea wote 11 yatapelekwa mjini Dodoma na kujadiliwa na Kamati Kuu (CC) ambayo inachagua majina matatu kwa ajili ya kupigiwa kura na Halmashauri Kuu (NEC), ili kupata jina moja la mgombea urais wa Zanzibar.
Habari zaidi zinasema kuwa baadhi ya wagombea walikuwa kwenye wakati mgumu, akiwemo Dk. Shein ambaye baadhi ya wajumbe walimhoji sababu za kutojiandikisha kupiga kura Zanzibar na nafasi ya chama iwapo atasimamishwa kuwania kiti hicho.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa Dk. Shein alitumia muda mwingi kufafanua jambo hili na kusisitiza kuwa hali hiyo haimwondolei sifa ya kugombea nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na Katiba ya Zanzibar.
Pia aliulizwa kwanini alibeza mipango ya kiuchumi ya Zanzibar alipotangaza sera zake baada ya kuchukua fomu, wakati Zanzibar ina programu nzuri za kiuchumi.
Akijibu swali hilo, Dk. Shein alisema hakuwa na nia mbaya isipokuwa alikuwa akijaribu kueleza malengo yake iwapo atapewa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar.
Katika kikao hicho zengwe kubwa lilielekezwa kwa Bilal, lakini kwa kutumia usomi wake na uzoefu katika masuala ya siasa na utawala aliweza kujieleza kiufasaha, hasa kuhusu swali alilokuwa ameulizwa, kwanini alifanyiwa sherehe wakati wa kurejesha fomu na wanacahama wa CCM katika viwanja vya Muembe Kisonge.
“Sioni kama ni kosa, yale yalikuwa ni mapenzi yao wanachama na nisingeweza kuwazuia na nilitoa shukurani tu nikaondoka, haukuwa mkutano uliotayarishwa na mtu,” kilikariri chanzo kimoja cha habari kutoka katika kikao hicho.
Habari zaidi zinasema kuwa baadhi ya wajumbe walimtaka aeleze kwanini wafuasi wake wamekuwa wakitoa vitisho vya kujitoa kwenye chama kama hatateuliwa kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, jambo ambalo Dk. Bilal alisema masuala hayo yeye hayamhusu kwani ni mambo yanayozungumzwa na watu kwa mapenzi yao binafsi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wa NEC Zanzibar, akiwamo Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
Wengine waliokuwepo ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Salim Ahmed Salim, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na mwanasiasa mkongwe, Ali Ameir Mohammed.
Hata hivyo mjadala mkubwa umejitokeza baada ya Rais mstaafu Dk. Salmin Amour Juma kuahirisha ghafla kuhudhuria mkutano huo, kinyume cha taarifa za awali ambazo zilidai kuwa kiongozi huyo alikuwa amejiandaa kuhudhuria kikao hicho.
“Wengi tumeshangazwa kwanini Dk. Salmin hajahudhuria kikao muhimu kama hiki, wakati yupo Zanzibar,” alihoji mjumbe mmoja wa kikao hicho.
Hata hivyo imedaiwa kwamba rais huyo mstaafu anatarajiwa kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu Dodoma, wiki ijayo baada ya kutohudhuria kikao hicho kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya macho yaliyokuwa yakimsumbua.
Wagombea wengine hawakupata wakati mgumu kwa kuwa walijieleza lakini hawakuulizwa maswali na kikao hicho, ambapo Rais Karume alitumia nafasi hiyo kuwaonya wajumbe na viongozi wa chama hicho wavunje makundi baada ya mgombea mmoja kupatikana.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Saleh Ramadhan Ferouz, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar inawataka wanachama wa CCM kuwa watulivu wakati mchakato wa kutafuta mgombea wa urais wa Zanzibar ukiwa unaendelea.
Alisema kikao hicho kimefanyika kwa kuzingatia ibara ya 115 (7)(b) ya Katiba ya CCM inayotoa madaraka kwa kamati maalumu kupokea majina ya wagombea wa urais na kuwajadili na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, ili na yenyewe itoe majina matatu kwenda katika kikao cha NEC.
NEC inatarajiwa kukutana mjini Dodoma Julai 9, mwaka huu, kupitisha jina moja kati ya 11 ya makada wa CCM walioomba uteuzi wa nafasi ya rais wa Zanzibar.
Suala la mgombea wa urais wa Zanzibar limekuwa na mvuto mkubwa na kujadiliwa kwa muda mrefu na wanachama wa CUF na CCM, tofauti na miaka ya nyuma.
Wanachama wa CUF wamekuwa wakitumia muda mwingi kujadili suala la mgombea wa urais wa CCM, wakiamini mgombea atakaechaguliwa kati ya hao ndiye atakayefanya kazi bega kwa bega na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kama kura ya maoni ya serikali ya umoja wa kitaifa itashinda.
Wakati wanachama wa CUF wakionekana kumuunga mkono Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, wanachama wa CCM wameonyesha kumuunga mkono Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Hoja ya msingi ya wanachama wa CUF ambayo wamekuwa wakiitumia ni kwamba Dk. Shein ni kiongozi mkimya na mwadilifu katika masuala ya uongozi, hana makundi Zanzibar na ana uwezo wa kuwaunganisha Wazanzibari wote.
“Naamini maridhiano ya Rais Karume na Maalim Seif yatakuwa salama kama atapewa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar Dk. Shein, wengine hawa wahafidhina,” alisema mwanachama mmoja wa CUF mkaazi wa Mtendeni.
Hata hivyo wanachama wa CCM Zanzibar waliohojiwa na gazeti hili katika matawi ya Magomeni, Kwamtipura, Kiembesamaki na maskani za Kaka Kisonge na Bambi Mkoani, wameonekana kumpa nafasi kubwa Dk. Bilal.
“Sifichi, kama jina la Dk. Bilal halitarudi siendi kupiga kura na Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa isitafute njia ya kuivuruga CCM,” alisema Khamis Juma, mwanachama wa Tawi la CCM Mgandini.
Mchakato wa Zanzibar, unaonekana kuchukua sura mpya, baada ya kujitokeza kwa siasa za Unguja na Pemba, wagombea ambao ni mara ya kwanza kujitokeza kuwania nafasi hiyo.
Wagombea hao ni Dk. Shein, Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mohamed Aboud na aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Hamad Bakar Mshindo.
Wanasiasa hao iwapo malengo yao yatafanikiwa watakuwa wameandika historia mpya kwa Zanzibar, kwa Kisiwa cha Pemba kutoa rais wa Zanzibar, lakini hadi sasa wajumbe 80 wa NEC Zanzibar wanaonekana kugawanyika kuhusu suala hili.
Wapo wanaotetea rais atoke Pemba na wale wanaotetea atoke kisiwani Unguja kama kuenzi wosia wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Sheikh Abeid Aman Karume.
Marais walioongoza Zanzibar wamekuwa wakitokea Unguja kwa awamu zote sita za uongozi na kuibua malalamiko kwa wananchi wa Pemba, jambo ambalo limeleta faraja mwaka huu baada ya wagombea watatu kujitokeza.
Marais waliowahi kuongoza Zanzibar ni Rais wa Kwanza, marehemu Abeid Aman Karume, Aboud Jumbe Mwinyi, Ali Hassan Mwinyi, marehemu Idrissa Abdulwakil, Dk. Salmin Amour Juma na Rais wa sasa, Amani Abeid Karume.
You Are Here: Home - - Bilal Kufanyiwa Zengwe Urais Zanzibar?
0 comments