Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sitta: Cheyo amejimaliza mwenyewe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Sitta: Cheyo amejimaliza mwenyewe
•  AWATAKA WABUNGE CCM KUHESHIMU VIAPO

na Martin Malera, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, amesema kuwa Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), amejimaliza mwenyewe kwa kuigeuka kambi ya upinzani, hivyo hatua aliyochukuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed (CUF), kumvua Uwaziri Kivuli ni sahihi.Akitangaza uamuzi huo jana bungeni, Sitta alisema amepata barua ya kiongozi huyo wa kambi ya upinzani, akimjulisha hatua aliyochukua kumwengua Cheyo katika nafasi ya Uwaziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya kukiuka msimamo wa kambi yao kwa kuiunga mkono Bajeti ya Serikali.
“Lakini jambo hili lilikuwa gumu zaidi baada ya kupata barua ya Cheyo, akipinga hatua ya kuenguliwa kwenye nafasi yake na kiongozi wa kambi ya upinzani na kutoa utetezi wake kwa nini aliiunga mkono Bajeti hiyo,” alisema Spika Sitta.
Alisema baada ya kupitia vitabu kadhaa vya sheria, alibaini kanuni ya 15 (2) ya Bunge, inampa kiongozi wa kambi ya upinzani mamlaka ya kuteua wasemaji wakuu wa kambi hiyo kwa wizara zilizoko serikalini.
Alisema baada ya kupitia barua ya Hamad na ile ya Cheyo, alilazimika kumwita mbunge huyo wa Bariadi Mashariki ili kujiridhisha kama alishiriki katika kuweka msimamo wa kambi ya upinzani.
“Aidha fasili ya 4 ya kanuni ya 16 imeelekeza kwamba vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni vinaweza kutunga kanuni zao kwa ajili ya uendeshaji bora wa shughuli zao za ‘Caucus’, hapa kambi ya upinzani ilifanya hivyo na inazo kanuni zake ambazo ni nzuri wala haziathiri chochote katika kanuni za Bunge,” alisema.
Sitta, alisema alichokifanya katika sakata hilo, baada ya kupelekewe malalamiko na Cheyo ni kujiridhisha kama kanuni zote zilifuatwa na kambi ya upinzani.
Huku akisikilizwa kwa makini na wabunge, Sitta alisema alizungumza na Cheyo mwenyewe na kubaini kuwa alishirikishwa katika maamuzi ya Kamati ya Upinzani.
Kwa kuzingatia hayo, Sitta alisema kitendo cha Cheyo kuunga mkono bajeti ya serikali wakati waliwekeana msimamo na wenzake wasiunge mkono, ni kitendo cha utovu wa nidhamu.
Alisisitiza kitendo hicho ni cha usaliti pia kwani hata kama suala hilo lingekuwa kwenye msimamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama kuna mbunge angepiga kura kuikataa bajeti, naye angeshughulikiwa ipasavyo.
“Kwa kuzingatia ufafanuzi huu ni dhahiri kitendo alichokifanya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani cha kumchukulia hatua za kinidhamu Cheyo kwa kosa la kwenda kinyume na msimamo wa kimsingi uliowekwa na kambi yake ni halali kikanuni na kiutaratibu wa Bunge. Basi hiyo ndiyo hali itakayotuongoza siku zijazo kwa kambi zote mbili,” alisema Sitta.
Alipofuatwa kutaka kujua msimamo wake baada ya uamuzi huo, Cheyo alisema hawezi kusema chochote hadi atakapoupitia uamuzi huo kwa umakini.
Cheyo alienguliwa juzi kwenye nafasi yake ya Uwaziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya kuisaliti kambi kwa kuiunga mkono Bajeti ya Serikali.
Akitangaza hatua hiyo, Hamad Rashid Mohamed (CUF), ambaye ni Mbunge wa Wavi, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya Cheyo kukiuka msimamo wa kambi yao.
Alisema hii ni mara ya pili kwa Cheyo kuiunga mkono Bajeti ya Serikali, licha ya msimamo wao, kwani mwaka jana alifanya hivyo na kusamehewa baada ya kuomba radhi, lakini mwaka huu amerudia.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, nafasi ya Cheyo sasa inachukuliwa na Mbunge wa Ziwani, Ali Said Salim, kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye awali alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa wizara hiyo.
Tags:

0 comments

Post a Comment