Dk. Salim, Meghji, Karume watajwa
Makundi yalenga urais wa 2015
KUIBUKA kwa jina la Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, kuwa mmoja wa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaotarajiwa kuchukua fomu za kuwania urais Zanzibar, Juni 21 mwaka huu, kumepandisha upya joto la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kuibua upya makundi ya kisiasa yaliyokuwepo mwaka 2005.
Tayari suala la nani ataziba pengo lake kuwa Mgombea Mwenza wa Rais Jakaya Kikwete, anayetarajiwa kutetea nafasi yake, limeibua mjadala na misuguano mizito ndani na nje ya CCM, lakini pia limeibua hoja nzito za kuwapo watu wenye maslahi binafsi nyuma ya hoja ya kumtaka Dk. Shein kwenda kuwania urais wa Zanzibar, akitokea katika nafasi ya juu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ambayo haina ukomo kikatiba.
Wakati majina kadhaa yanatajwa kuchukua nafasi ya Dk. Shein ya mgombea mwenza wa Kikwete kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, mjadala mzito unajikita kwenye changamoto nyuma ya nguvu ya Shein kisiasa Visiwani na nafasi ya Rais wa sasa wa Zanzibar, Amani Abeid Karume katika kudhibiti wagombea wengine, na hata ushawishi ama hata kwenda mwenyewe kuwa mgombea mwenza wa Kikwete.
Kwa mujibu wa Katiba, mgombea mwenza hutoka Visiwani kama mgombea urais ni wa Bara na kinyume chake.
Changamoto ya Dk. Shein kuwania urais wa Zanzibar inajikita nyuma ya historia yake kisiasa Zanzibar, hulka yake ndani na nje ya jamii ya Wazanzibari, makundi ya kisiasa Visiwani humo na sumu ya ubaguzi iliyojaa ndani ya vichwa vya wanasiasa na hata sehemu kubwa ya jamii Visiwani humo, mambo ambayo yana nguvu kubwa katika maamuzi ya kisiasa katika chaguzi zote.
Kuingia kwa Dk. Shein katika siasa za Zanzibar kumeelezwa na wanasiasa wenzake kuwa kunaweza kuwa mzigo mzito kwa CCM kutokana na historia ya kisiasa na kijamii ya kiongozi huyo Visiwani humo tokea aingie katika siasa mwaka 1995, lakini pia inaelezwa kwamba wanaomsukuma kuwania urais wa Zanzibar wanasukumwa zaidi na malengo yasiyo na maslahi kwa umma yakiwamo kutaka kudhibiti maamuzi ya kisiasa Visiwani humo na kuwadhibiti wagombea wengine wenye nguvu.
Wanasiasa wenye nguvu wa Zanzibar waliozungumza na Raia Mwema kwa masharti maalumu ikiwamo kutotajwa majina, wanamuelezea Dk. Shein kama mwanasiasa wa wastani ambaye hajawahi kuingia katika siasa za ushindani kwa nguvu yake binafsi na kwamba kwa siasa za sasa atapata wakati mgumu kukabiliana na mgombea wa chama cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF) Seif Shariff Hamad ambaye amegombea tangu mwaka 1995.
ALIKOTOKA KISIASA DK.SHEIN
Mwaka 1995 Dk. Shein aliiingia katika siasa kwa kuombwa baada ya CCM kutafuta wagombea katika kisiwa cha Pemba na aliahidiwa kupewa nafasi ya Unaibu Waziri hata akishindwa, na aliposhindwa, aliyekuwa Rais, Dk. Salmin Amour Juma, alimteua kuwa Mwakilishi na kumpa nafasi ya Unaibu Waziri wa Afya.
Wakati wa uchaguzi wa CCM mwaka 1997, Dk. Salmin alimuomba tena Shein kuwania ujumbe wa NEC, Mkoa wa Kusini Pemba, na huko alishika nafasi ya pili nyuma ya Mohamed Aboud aliyeongoza kwa zaidi ya mara mbili ya kura zake na kuingia kwa mara ya kwanza katika NEC.
Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2000, Dk. Shein anatajwa kuomba nafasi ya kazi nje ya nchi, lakini Rais Karume alipoteuliwa kuwa mgombea wa CCM akamuomba tena kuwania Jimbo la Mkanyageni, akiahidi kumpatia nafasi ya uwaziri ‘hata kama angeshindwa’ katika nafasi ya uwakilishi.
Uchaguzi wa mwaka 2000 uligubikwa na vituko na CUF kususia uchaguzi huo kisiwani Pemba, na hivyo Dk. Shein kuibuka mshindi jimbo la Mkanyageni na kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, wizara mpya iliyoanzishwa na Karume.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, Zanzibar iliingia katika mgogoro wa kisiasa uliosababisha mauaji ya watu takriban 30 ambayo yaliitia dosari Serikali ya Rais Benjamin Mkapa. Mkapa aliwatuma wasaidizi wake wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Jakaya Kikwete, na Dk. Shein akawa mmoja wa viongozi waliokuwamo katika timu hiyo kwenda kuieleza dunia kilichotokea na kuisafisha Tanzania kwenye uso wa kimataifa kuepusha viongozi wa juu kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Kabla joto la mauaji ya hayo ya 2001 halijapoa, nchi ikaingia katika mtikisiko mwingine baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma, kufariki dunia ghafla jijini Dar es Salaam. Kwa kuwa Dk. Omar alitokea Pemba, jina la Dk. Shein likajitokeza tena na akateuliwa kuchukua nafasi yake, na jina lake kupitishwa na CCM na hatimaye Bunge zima. Shein hakufanya kampeni na wala hakuwa amewania nafasi hiyo.
Mwaka 2005 baada ya mchakato kumpata mgombea wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu, Kikwete aliyepata nafasi hiyo, alielezwa kuwa na orodha ya watu aliotaka wawe wagombea wenza, jina la Dk. Shein halikuwamo.
Waliozungumza na Raia Mwema wanasema kwamba wazee wa CCM walimwambia Kikwete kwamba wanaona ni vyema akaendeleea na Dk. Shein kupunguza makundi, lakini pia ni kwa kuwa alikwisha kuanza kushika wadhifa huo na hivyo si vyema kumuengua.
Dk. Shein alipitishwa kwa nidhamu ya chama na hakuwa na kazi kubwa katika kampeni za urais wa mwaka 2005 kutokana na nguvu kubwa ya kisiasa ya Kikwete wakati huo.
Wanaotajwa sasa kuweza kuchukua nafasi ya Dk. Shein ya mgombea mwenza wa Kikwete katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, ni pamoja na Rais Karume, Waziri Mkuu Mstaafu na mwanadiplomasia anayeheshimika duniani, Dk. Salim Ahmed Salim na Waziri wa zamani wa fedha, Zakia Hamdani Meghji.
Katika majina hayo, jina la Dk. Salim limeelezwa kuwa zito lakini watu walio karibu naye wamesema mwanadiplomasia huyo ambaye aliwania urais mwaka 2005 amekuwa akisita sana kujiingiza tena katika siasa za moja kwa moja, huku baadhi ya wanasiasa wakimuelezea kuwa mtu anayeogopwa na wanasiasa wa sasa ndani ya CCM kutoka Bara na Visiwani.
Hivi karibuni kuliibuka tena taarifa za kumchafua Dk Salim katika mitandao ya intaneti, taarifa zilizoelezwa kutoka katika kundi lile lile lililotumika kumchafua mwanasiasa huyo wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 2005.
Lakini Dk. Salim mwenyewe amenukuliwa mara kadhaa na vyombo vya habari nchini akisisitiza kuwa hana nia yoyote ya kurudia kugombea nafasi yoyote ya uongozi serikalini.
Kuhusu urais wa Zanzibar, wengine ambao wamo pia katika orodha ya wanaotajwa kuwa na nia ya kuwania ni pamoja na Waziri Kiongozi wa sasa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud Mohamamed ambaye anatokea Wawi Kisiwani Pemba, Waziri Kiongozi mstaafu Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna.
Kwa upande wa Mohamed Aboud, ambaye anatokea Wawi, Pemba na mwenye asili ya Kiarabu, alikuwa akitajwa kuwa mtu aliyekuwa akiungwa mkono na Dk. Shein kuwania urais wa Zanzibar, ameelezwa kwamba nafasi yake kupata nafasi ya juu ya uongozi ni kubwa kutokana na historia ya siasa za ubaguzi na visasi vya kisiasa visiwani Zanzibar.
Visiwa vya Unguja na Pemba vimewahi kutawaliwa na Waarabu na baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 Waafrika walichukua madaraka kupinga ubaguzi na sasa zimeibuka tena hisia za ubaguzi ambapo watu wenye asili ya Kiarabu wamekuwa wakinung’unika kubaguliwa katika uongozi lakini wamekuwa na ushawishi mkubwa katika jamii.
Rais Karume ambaye anamaliza vipindi vyake viwili vya urais mwaka huu baada ya kuingia Ikulu mwaka 2000, nafasi yake kuwa mgombea mwenza wa Kikwete bado ni tata na anahofiwa kuwa na changamoto kubwa kutoka kwa makundi ya kisiasa ya Bara na Visiwani ndani ya CCM kabla ya kuteuliwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Habari zinasema ni Karume anayemsukuma sana Dk. Shein kiasi cha kuwatia hofu wawaniaji wengine, hasa walio chini yake kama Shamsi Vuai ambaye wiki iliyopita alilazimika kufuta mkutano wake na waandishi wa habari dakika za mwisho.
Habari zinasema Waziri huyo Kiongozi alikuwa ameitisha mkutano wiki iliyopita ili kutangaza nia yake ya kuwania urais, lakini kwa mawasiliano na Ikulu ya Zanzibar akalazimika kuufuta.
Wachunguzi wa mambo wanasema kinachogomba Zanzibar na ambacho kitakuwa na mwangwi mkubwa Bara miongoni mwa wana CCM ni kwamba kwa nafasi yake Karume hawezi kumnadi Dk. Shein kwa vile yeye mwenyewe hana ushawishi wa kutosha ndani ya CCM Zanzibar.
Kwa CCM Zanzibar, habari zinasema, kumnadi Dk. Shein ni sawa na kumtangazia ushindi wa bila jasho Maalim Seif ambaye majuzi amefikia maelewano na Rais Karume yaliyoanzia katika makubaliano binafsi kati yao.
Duru za habari zinasema kikwazo kwa Seif kati ya wote kinaweza kuwa ni Dk. Bilal ambaye anapigiwa debe sana na baadhi ya wana CCM wa Unguja na Mohamed Aboud ambaye anapendwa na Wapemba na wanasiasa wenye siasa za wastani.
Uchukuaji fomu za uongozi huo wa juu ndani ya CCM unaanza wiki ijayo na unatakiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Julai.
0 comments