IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MAKUNDI ya wagombea urais Zanzibar baada ya Rais Aman Abeid Karume kumaliza muda wake mwaka huu, yameingiwa hofu kubwa baada ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, kutajwa kwamba ndiye chaguo la Rais Karume na vigogo wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata kutoka kwa watu wanaotajwa kutaka kugombea nafasi hiyo, wakiwemo baadhi ya mawaziri walio mjini hapa kuhudhuria mkutano wa 20 wa Bunge la Bajeti, walisema hatua hiyo imeibua hofu kwa makundi hayo ya rais kwani Dk. Shein pia anaungwa mkono kwa nguvu zote na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).
CUF inadaiwa kumuunga mkono Shein, kwani inaamini kuwa ndiye mtu pekee anayeweza kuheshimu na kudumisha maridhiano yaliyofikiwa kati ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, na Rais Karume ambayo yamezaa mpango wa kutaka kuunda Serikali ya Mseto baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Wakati makundi mengine yakiingiwa hofu ya kukosa nafasi hiyo, kambi ya Dk. Mohammed Gharib Bilali ambaye amepata kuwania nafasi hiyo na kumshinda Rais Karume kwenye kura za maoni, lakini akaenguliwa na vikao vya juu vya CCM, inadaiwa amejizatiti akiamini kwamba safari hii lazima aingie Ikulu ya Zanzibar.
“Rais Karume bora abaki pembeni akiangalia mchezo unavyokwenda. Dk. Bilal mara mbili amedhulumiwa haki yake, mwaka huu hana sababu ya kuachwa, lazima aende Ikulu,” alisema mmoja wa vigogo wa CCM kutoka Zanzibar ambaye yuko kwenye kambi ya Dk. Bilali.
Vigogo wengine wanaotajwa kuwania urais Zanzibar, Mbali ya Dk. Shein na Dk. Bilali, ni Mohammed Seif Khatib, Shamsi Vuai Nahodha, Mohammed Aboud, Balozi Ali Karume na Dk. Mwinyihaji Mkame Mwadini.
Wengine ni Waziri wa Elimu Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Habari, Ali Juma Shamuhuna, Naibu Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee na Waziri wa zamani wa Fedha, Amina Salum.
Takriban wote wanaotajwa kutaka kuingia katika kinyang’anyiro hicho hawajaeleza waziwazi nia yao, lakini kila mmoja anasema ikifika wakati atatangaza na baadhi yao wamesema wiki ijayo watatangaza nia yao ya kutaka kuchukua fomu muda utakapofika.
Habari zaidi kutoka kambi za wagombea wengine, zinasema kuwa wengi wanaelekea kumuunga mkono Dk. Shein, lakini lazima kiongozi huyo akae na makundi yote na kuzungumza nayo ili kuweka mambo sawa.
“Unajua lengo la wote ni kuhakikisha Zanzibar inapata kiongozi imara, atakayesukumu kurudumu la maendeleo na kuimarisha mshikamano ulioanzishwa kati ya Rais Karume na Maalim Seif. Naamini tukikaa na kukubaliana pamoja, hakuna tatizo,” alisema mmoja wa mawaziri wa Mungano wanaotajwa kutaka kumrithi Karume.
Kwa muda mrefu, Dk. Shein amekuwa akiombwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, achukue fomu ya kuwania nafasi hiyo kubwa ya kisiasa visiwani humo. Rais Karume anamaliza vipindi vyake viwili vya urais mwaka huu baada ya kuingia Ikulu mwaka 1995.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es salaam na Zanzibar, Dk. Shein alikuwepo visiwani humo wiki iliyopita na kufanya mazungumzo maalumu na Rais Karume na habari zinasema kiongozi huyo wa Zanzibar alimuomba Dk. Shein kukubali kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo moto.
Hamu ya Rais Karume kumtaka Dk. Shein kuwa mrithi wake inatokana na makamu huyo wa rais kuonekana ana msimamo wa wastani katika siasa za Zanzibar zilizo na chuki za Upemba na Uunguja, huku akionekana kuwa hana makundi kulinganisha na wagombea wengine.
Sababu nyingine ni Dk. Shein kuonyesha dhamira ya kutaka kuendeleza maridhiano yaliyofikiwa Novemba 5 mwaka jana kati ya Rais Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Awali Dk. Shein alikuwa mgumu kukubali ombi la Rais Karume kutokana na wana CCM wahafidhina wanaotoa salamu za chuki dhidi ya wana CCM wenye asili ya Pemba wanaowatishia kwamba kamwe wasijaribu kugusa fomu za kuwania urais.
Kujitokeza kwa Dk. Shein kunaelezwa kupata baraka zote za Rais Karume na baadhi ya viongozi wengine wa serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwani anaonekana kuwa mtu asiye na upande hadi sasa kati ya wanaotaka kuwania urais wa Zanzibar.
Kabla ya kuwa makamu wa rais, Dk. Shein aliwahi kuwania uwakilishi wa jimbo la Mkanyageni mwaka 2000 kisiwani Pemba, kijiji ambacho amezaliwa. Kiti hicho kinashikiliwa na mwakilishi wa CUF Haji Faki Shaali.
Kuingia kwa Dk. Shein katika kinyanganyiro cha urais wa Zanzibar kutasababisha mfadhaiko kwa baadhi ya watu wanaotaka kuwania nafasi hiyo kuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na rekodi yake ya uadilifu na nidhamu ndani ya chama kikongwe cha CCM.
Pia kutaibua changamoto mpya kwenye siasa za Zanzibar ambako tayari wanachama wa CCM wameshaanza kupigana vijembe kuhusu nia ya baadhi yao kuwania urais. Katika siasa za Zanzibar, watu kutoka Pemba wamekuwa wakilaumu ndani ya CCM kuwa wanabaguliwa.
You Are Here: Home - - Dk. Shein, Bilali waipasua Zanzibar
0 comments