IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WATAALAMU bingwa wa sheria wametofautiana kuhusu uwezo wa Mahakama kutengua kifungu cha Katiba na kutamka kuwa ni batili, hivyo suala la mgombea binafsi bado ni kitendawili.
'Marafiki’ hao wanne wa Mahakama walifika jana katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania kushauri kisheria kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ulioruhusu mgombea binafsi.
Wataalamu hao ni Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu, Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Othman Masoud na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Jwan Mwakyusa.
Mahakama iliiomba NEC ieleze iwapo Mahakama hiyo itaruhusu mgombea binafsi, imejiandaaje. ‘Marafiki’ wengine, walitakiwa kutoa ushauri kama Mahakama ina uwezo wa kusema kifungu cha Katiba kinaikiuka Katiba yenyewe.
Profesa Kabudi amesema, Mahakama haina mamlaka hiyo, labda Katiba yenyewe iwe inaeleza hivyo. Amesema, Mahakama haina uwezo huo kwa sababu ndiyo sheria mama ya nchi na iko juu ya sheria zote na lazima ifurahie ukuu wake.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, hakuna chombo au mhimili wowote; Bunge, Mahakama au Serikali, wenye uwezo wa kutamba kuwa uko juu ya Katiba. “Katiba ndiye baba si Mahakama, Bunge wala Serikali.”
Amesema,Katiba haina mbadala wake, wala sheria za kimataifa haziwezi kulinganishwa na Katiba ya nchi. Kabudi amesema, kutokana na ukuu huo wa Katiba, sheria zote za kimataifa ni lazima ziridhiwe na Bunge kabla ya kukubaliwa kutumika nchini.
Amesema si jukumu la Mahakama kusema Katiba ni mbaya, badala yake hilo ni jukumu la watu na akaongeza kuwa Mahakama inatakiwa kuwa mlezi wa Katiba.
Akizungumzia ibara ya 30 (3) (5), Profesa Kabudi amesema,kifungu hicho kinaipa Mahakama haki ya kutoa maoni na kushauri, ili vyombo vinavyohusika vichukue hatua, lakini mahakama hairuhusiwi kusema kifungu cha Katiba ni batili.
Msomi huyo amesema, Mahakama nje ya vifungu vya Katiba, kwenye sheria zingine inaruhusiwa kuita sheria ni batili na inakiuka Katiba ya nchi.
“Katiba haizalishwi, inajizaa, lakini Mahakama inazaliwa,” alisema Profesa Kabudi na kuliambia jopo la majaji hao kuwa wana mamlaka ya kushauri tu, si kusema kifungu fulani kwenye Katiba ni batili.
“Mnaweza kutoa maoni na kushauri na si kuagiza kuwa kifungu hicho ni kinyume cha Katiba kwani vifungu hivyo ni sehemu ya Katiba na ni Katiba … sijaja hapa kusema kama Katiba hii ni nzuri au mbaya, ila nimekuja kutoa ushauri huo,” amesema.
Profesa Mwaikusa amepingana na Profesa Kabudi, anasema, Mahakama ni mhimili pekee wenye mamlaka ya kulinda haki ya msingi ya mtu na inapoona inaporwa na chombo chochote hata iwe Katiba.
Kwa hali hiyo, alisema kwa mujibu wa ibara ya 107 ya Katiba, Mahakama haiwezi kunyang’anywa na mhimili mwingine haki hiyo ya kulinda uhuru na haki ya mtu mwingine.
“Kwa maoni yangu Mahakama Kuu ilikuwa na haki ya kusema kifungu cha Katiba kiko kinyume na Katiba yenyewe, kwa vile kinamnyang’anya mtu haki yake ya msingi,” aliongeza.
Profesa Mwaikusa amesema, Mahakama haiwezi kunyamaza inapoona haki ya mtu inavunjwa kwenye Katiba au inaporwa na mamlaka nyingine.
“Hivi kweli mahakama ikiona kifungu kinavunja haki ya msingi ya mtu ikae kimya eti marekebisho ni kazi ya Bunge … hapana.”
Amesema, Katiba hairuhusiwi kupora haki ya msingi ya mtu bali kazi yake ni kulinda haki ya mtu huyo na iwapo kuna kifungu kwenye Katiba kinapora haki hizo, lazima Mahakama iseme kifungu hicho ni batili.
“Haki ya msingi ya mtu ndio msingi wa Katiba, haki hizi hazitengenezwi na Katiba na wala Katiba hairuhusiwi kuzizika, kwani hiyo si kazi yake na hakuna sehemu haki hizo zinazaliwa,” alifafanua.
Amesema, ni jukumu la Bunge ambalo ni chombo cha kutunga sheria, kuhakikisha kinalinda haki ya msingi ya mtu na kuiweka kwenye sheria; hivyo Mahakama ndiyo maana inakuwa na mamlaka ya kulinda haki hizo hasa pale inapoona zinachezewa.
“Kupora haki hizi si kinyume cha Katiba tu bali ni hatari kubwa,” alisema na kuongeza kuwa hata nchi ambazo hazina Katiba zinatakiwa kuheshimu haki ya msingi ya binadamu, kwani mtu anapozaliwa huzikuta haki hizo zikiwapo.
Alisema Bunge lilitaka kuonesha ukuu wake wa kurekebisha sheria ya Katiba hadi kukiuka haki ya msingi ya mtu, jambo ambalo alisema halikubaliki.
Aliongeza kuwa Bunge lina mipaka ya kutunga sheria hizo na pale linapokosea, ni Mahakama ndiyo inakuwa na mamlaka ya kusema “ndiyo maana tuko hapa leo.”
Alisema kama vile Mahakama ilivyokataa kujadili adhabu iliyotolewa na Bunge katika kesi ya Augustine Mrema dhidi ya Spika, hivyo Mahakama inatakiwa iachwe huru ifanye kazi yake ya kulinda haki ya msingi ya mtu.
Msomi huyo alisema kifungu cha Katiba kinachojaribu kupora na kuvunja haki ya msingi ya mtu ni lazima Mahakama ikihoji na akaongeza kuwa Mahakama ina haki ya kuheshimu Katiba ambayo inalinda haki za binadamu na si inayovunja haki hizo.
Alisema ilichofanya Mahakama Kuu katika kesi hiyo ya mgombea binafsi, ilikuwa na haki ya kusikiliza shauri hilo na kutamka kuwa kifungu hicho kinakwenda kinyume na misingi ya Katiba ni sahihi.
“Lakini Mahakama ilikwenda mbali hadi kutoa amri kwa mamlaka zingine kuandaa taratibu za uchaguzi … hiyo si kazi yake, bali ilitakiwa kutamka tu kuwa kifungu hicho ni batili na kinakwenda kinyume na Katiba,” alisema.
Katika hoja yake, Masoud alisema marekebisho ya Katiba yakishafanyika, yanakuwa ni Katiba na hayawezi kuishi peke yake na akaeleza kuwa Mahakama haina mamlaka ya kukifuta kifungu hicho au kukiita batili.
Alisema ibara ya 30 (5) inatoa fursa kwa Mahakama kueleza kasoro za kifungu hicho kama wakiona hakioani na misingi ya Katiba, lakini hairuhusiwi kusema kifungu hicho ni kinyume cha Katiba yenyewe.
Alisema marekebisho yaliyofanywa na Bunge kwa kuondoa ibara ya 20 (1) si kwamba yalikiuka haki za binadamu si kweli, kwani hayakuongeza jambo jipya bali yaliimarisha Katiba.
Aliongeza kuwa kupitia vyama vya siasa watu wote wanapewa haki ya kutumia haki yao ya kugombea. Alisema vyama vya siasa ndio msingi wa demokrasia katika nchi. “Vifungu hivi haviondoi haki ya mtu kugombea, kwani vyama vina umuhimu wake,” alisema Masoud.
Kiravu akieleza nafasi ya Tume kushughulikia mgombea binafsi katika uchaguzi wa mwaka huu, alisema NEC imeanza mchakato huo kwa kufuata sheria zilizopo ambazo hazihusu kipengele cha mgombea binafsi.
Alisema hatua walizofikia katika mchakato huo ni za mwisho hasa katika maandalizi ya fomu maalumu za uteuzi, za uchaguzi na za matokeo ambazo zote zimezingatia sheria ya sasa.
Alisema iwapo Mahakama Kuu itaruhusu mgombea binafsi, suala la gharama kuongezeka litajitokeza, kwani tayari Tume imekamilisha mchakato wa kuchapa karatasi za kura ambazo zinaonesha vyama wanavyotoka wagombea.
Kiravu alisema suala ili tume iweze kujiandaa ilikuwa lazima ilifahamu mapema, ili kufanya maandalizi kwa kuanzia kwenye karatasi za kura, fomu za uteuzi na hata masanduku ya kura yanaweza pia kubadilika.
“Uamuzi ukifanyika mapema, hautamwathiri mzabuni atakayepatikana kuchapa karatasi hizo,” alisema.
Tatizo lingine alisema iwapo mgombea binafsi ataruhusiwa kwa sasa, Tume itahitaji muda zaidi wa kushughulikia mapingamizi, kwani ni lazima yataongezeka. “Inawezekana muda usitosheleze katika kushughulikia mapingamizi hayo.”
Alisema pia kwa sasa NEC inaandaa maadili ambayo viongozi wa vyama vilivyopo huyasaini na wagombea wa vyama hubanwa na maadili hayo. “Hatuelewi akija mgombea binafsi kama atalazimika kuyafuata au la.”
Eneo lingine alilozungumzia ni idadi ya mawakala kwenye vituo vya kupigia kura ambako alisema kwa sasa wanaandaa mazingira ya kuhudumia mawakala 18 wa vyama na iwapo mgombea binafsi ataruhusiwa, vituo hivyo vitajaa watu.
Alisema unahitajika muda wa kurekebisha sheria inayozungumzia mgombea urais na mwenza wake. Kesi hiyo itatolewa uamuzi siku itakayopangwa na Mahakama hiyo.
You Are Here: Home - - Mgombea binafsi hakijaeleweka
0 comments