IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SERIKALI imekiri kwamba fedha za mikopo nafuu zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, maarufu kama mabilioni ya JK zimeliwa na wajanja wachache waishio jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza kwenye awamu zote za utoaji wa mabilioni hayo, mbele ya Kamati ya Bunge inayoshughulikia Huduma za Jamii, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, alisema Dar es Salaam peke yake imepata zaidi ya sh bilioni tatu.
Profesa Kapuya alisema, fedha hizo zimeshindwa kuwafikia walengwa ambao ni wajasiriamali wadogo kutokana na ujanja uliofanyika hususan kwa jijini ambako kiasi kilichotolewa ni kikubwa kuliko maeneo mengine.
“Mpango wetu ni kugawa sh bilioni moja kila mkoa lakini baadhi ya mikoa na wilaya hazikupata na mingine kupata zaidi... kwa kweli hii ndiyo changamoto tuliyokabiliana nayo kwa awamu ya kwanza na ya pili ya mikopo ile lakini tumejipanga,” alisema Profesa Kapuya aliyetakiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kueleza sababu za mikopo hiyo kuishia kusikojulikana.
Profesa huyo alikiri kwamba wakati wa utoaji wa mikopo hiyo hapakuwa na malengo thabiti na kueleza kwamba serikali ilitegemea uhamasishaji kutoka kwa wakuu wa wilaya, mikoa na watendaji wengine ili kuanzishwa kwa vikundi vya kuweka na kukopa.
Alisema, kwa awamu ijayo serikali imejizatiti kufikisha fedha hizo kwenye maeneo yaliyokosa kabisa huku akijivunia kwamba mikopo ya mabilioni ya JK imefanikiwa kuongeza ajira 67,000 na kufanya idadi ya ajira zilizotolewa na serikali ya awamu ya nne kufikia 1,271,000 nchini kote.
Kadhalika, waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Urambo Magharibi, alisema mikopo hiyo imetolewa zaidi kwa wanaume ingawa hakueleza idadi ya waliorejesha na wanaoendelea kudaiwa hadi sasa.
Alisema, jumla ya wanaume waliopatiwa mikopo hiyo kwa viwango tofauti ni 17,697 wakati wanawake waliodhaniwa kuwa walengwa wakuu ambao wamekopeshwa fedha hizo ni 4258 idadi inayoelezwa kuwa ni nchi nzima.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jenista Mhagama, alimtaka Waziri Kapuya kandaa taarifa nyingine kwa ajili ya kamati ili kuonyesha idadi ya wakopaji kwa jinsi na rika huku ikiainisha mtiririko wa ulipaji wake.
You Are Here: Home - - 'Mabilioni ya JK yameliwa'
0 comments