IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
RAIS Jakaya Kikwete kwa mara nyingine amefanya mabadiliko ya vituo vya kazi kwa baadhi ya wakuu wa wilaya kwa kuwahamisha na kuwapangia vituo vipya, huku akitengua uteuzi wa Thobias M. Sijabaje aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Sumbawanga kutokana na kutosimamia vizuri zoezi la ugawaji wa vocha za pembejeo za kilimo katika wilaya ya Sumbawanga msimu wa mwaka 2009/2010.
Pamoja na mabadiliko hayo, Rais Kikwete pia amemteua Husna Mwilima aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba kuchukua nafasi ya Francis Miti anayehamia wilaya ya Ulanga.
Mwilima ambaye kabla hajawa Katibu Mkuu wa UWT alitokea Wilaya ya Hai alikokuwa Mkuu wa Wilaya, katika siku za hivi karibuni kabla hajaachia wadhifa huo UWT alikumbana na mgogoro na viongozi wenzake, hali ambayo wachambuzi wa mambo wanadai kuwa ndiyo iliyopelekea kung’oka katika nafasi hiyo.
Katika taarifa ya uteuzi huo iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, rais pia amemhamisha Mkuu wa Wilaya Ilala, Evance Balama, na kumpangia wilaya ya Mbeya kuchukua nafasi ya Leonidas Gama anayehamia Ilala.
Wengine walioguswa na mabadiliko hayo ni pamoja Gishul Mbegesi aliyekuwa Njombe na ambaye amehamishiwa wilaya ya Kilindi, Frank Uhaula aliyekuwa Tarime amehamishiwa Kiteto.
Aidha, mwanahabari, Sara Dumba, aliyekuwa Kilindi amehamishiwa Njombe; John Henjewele aliyekuwa Kiteto amehamishiwa Tarime; na Rashid Ndaile aliyekuwa Chunya amepelekwa Mkinga.
Wengine ni Florence Horombe aliyekuwa Bukombe kapelekwa Nzega; Zainab Kwikwega aliyekuwa Kasulu amehamishiwa Makete; Luteni Kanali John Mzurikwao aliyekuwa Mpanda amehamishiwa Sumbawanga; na Hawa Ngh’umbi aliyekuwa Makete amehamishiwa Bukombe.
Betty Machangu aliyekuwa Nzega amehamishiwa Kasulu; Dk. Rajab Lutengwe aliyekuwa Ulanga amepangiwa Mpanda; Francis Miti aliyekuwa Tandahimba amehamishiwa Ulanga; na Deodatus Kinawiro aliyekuwa Mkinga amehamishwa wilaya ya Chunya.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mabadiliko hayo ambayo yanaanza mara moja yanakusudia kuongeza ufanisi wa kazi, kuimarisha utendaji katika wilaya hizo.
You Are Here: Home - - JK apangua tena wakuu wa wilaya
0 comments