Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Bunge kujadili upya Sheria ya Gharama za Uchaguzi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa ambaye amewasilisha mapendekezo kwenye kamati ya Uongozi ya Bunge kutaka Bunge lipitie upya sheria ya gharama za uchaguzi
LISAINIWA kwa mbwembwe, lakini hata kabla ya kuanza kutumika, Sheria ya Gharama za Uchaguzi inarejeshwa bungeni kuangaliwa kasoro zake, hali inayoonyesha kuwa uwezekano wa kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni mdogo.

Tofauti na sheria nyingine zinazosainiwa bila ya uwepo wa viongozi wa vyama vya siasa, Rais Jakaya Kikwete alisaini sheria hiyo kwa kualika viongozi wa vyama hivyo, taasisi za kijamii na viongozi wa kidini katika hafla iliyofanyika Ikulu.

Lakini alisaini huku wabunge wa vyama vya upinzani wakiipinga kutokana na kuwa na kasoro nyingi ambazo walidai zinaweza kutumiwa kuvikandamiza vyama vya upinzani.

Na kilio chao kinaweza kuwa kimepata jibu baada ya Bunge, ambalo linaanza mkutano wake wa 19 kesho mjini Dodoma, kukubali kuirejesha suala hilo kwenye chombo hicho cha kutunga sheria baada ya mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa kuwasilisha mapendekezo kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge kutaka Bunge lipitie upya sheria hiyo na kuifanyia marekebisho kabla ya kuanza kutumika.

Bunge limefikia uamuzi huo ukiwa umebakia mwezi mmoja kabla ya mchakato wa uchaguzi mkuu kuanza kwenye ngazi ya vyama.

Slaa aliwasilisha pendekezo hilo katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

"Kamati ya Uongozi ya Bunge ilikutana kupanga ratiba ya vikao vya bunge, lakini baadaye Dk Slaa, kama mjumbe, akawasilisha pendekezo hilo na sisi tukaona ni vyema suala hilo likapata ufafanuzi zaidi kwa kuwashirikisha wabunge wote," alisema spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta.

"Tumeona katika sheria hii mambo mengi yako kinadharia, kwa mfano; sheria inasema kuwe na wajumbe wa kampeni wasiozidi 20 kwa mbunge na 10 kwa diwani na wagombea hao wawe wameidhinishwa na DASS au WEO.

"Hili ni jambo jema, lakini tafsiri yake ni kwamba serikali sasa itakuwa na ruhusa ya kukubali au kukataa nani aingie kwenye kampeni hizo na nani asiingie; na kama hiyo ndiyo tafsiri, kimsingi inaleta shida."

Spika Sitta alifafanua kuwa katika bunge hili, wabunge watazitazama tena kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo na kuzifanyia marekebisho.

"Kama tatizo ni sheria itabidi ijadiliwe upya na kama tatizo ni kanuni, tutamtaka waziri mkuu aziboreshe."

Alipoulizwa endapo kama suala hilo lijadiliwe bungeni katika mkutano unaoanza kesho, Spika Sitta alijibu: "Kwa nini isiwezekane?, Tumepanga kuwa na kikao cha siku nzima kuipitia sheria hiyo na kanuni."

Kwa mujibu wa Spika Sitta, ikiwa katika kuangalia sheria na kanuni zake tatizo likaonekana kwenye kanuni, waziri mkuu ndiye mwenye wajibu wa kuzirekebisha, lakini kama tatizo litakuwa ni sheria yenyewe, lazima irudishwe na kujadiliwa upya.

Awali, Dk Slaa aliliambia gazeti hili kuwa amewasilisha mapendekezo hayo kutokana na kile alichodai kuwa Rais Kikwete amedanganywa na kusaini sheria hiyo kimakosa.

Alisema aliamua kuliwasilisha suala hilo kwanza kwenye kamati ya uongozi ya Bunge ili kama angepuuzwa, alifikishe suala hilo bungeni mwenyewe kwa namna anayoona inafaa.

"Mapambano ndio yameanza; mimi ni mjumbe wa kamati ya uongozi ya Bunge na leo (jana) tulikuwa na kikao, nimehoji suala hilo kabla sijalifikisha bungeni kwa namna ambayo nitaona inafaa," alisema Dk Slaa.

"Bado nasisitiza kuwa Mwanasheria Mkuu amedanganya kwa kusema vifungu hivyo viko sahihi kwa kuwa Ofisi ya (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera na Uratibu wa Bunge-, Phillip) Marmo ndio iliyovifanyia marekebisho. Ofisi ya Marmo haina mamlaka ya kubadili vifungu vya sheria iliyopitishwa na Bunge.

"Lengo langu sio kumvunjia heshima Mwanasheria Mkuu na yeye anajua kuwa namheshimu sana, lakini lazima Watanzania tuone serikali yetu inafanya kazi kwa uwazi, ukweli na uwajibikaji," alisema.

Alisisitiza kuwa kilichojadiliwa bungeni ni vikundi vya sanaa na Bunge liliagiza viingizwe vifungu vya ufafanuzi na sio mabadiliko ya vifungu.

Dk Slaa analalamikia kifungu cha 7 (3) katika sheria hiyo, akidai kuwa kimechomekwa kinyemela kwa kuwa hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu kidogo cha pili, kinaeleza maana ya timu ya kampeni kuwa ni kundi la watu lililoundwa na mgombea wakati wa zoezi la uteuzi lenye madhumuni ya kumwakilisha au kumsaidia mgombea kwenye kampeni za uchaguzi ambaye amepitishwa kuwania.

"(a) Kwa kesi ya urais watathibitishwa na Msajili; (b) Kwa kesi ya ubunge watathibitishwa na Katibu Tawala wa Wilaya na (c) kwa kesi ya diwani watathibitishwa na Katibu Tarafa...," inaeleza sehemu ya sheria hiyo iliyosainiwa na Rais Kikwete Machi 17 mwaka huu.

Muswada wa sheria hiyo ulipitishwa kwa mbinde bungeni Februari 12 mwaka huu mjini Dodoma na kuibua malumbano makubwa baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pamoja na wabunge wengine kuhusu vipengele mbalimbali vya muswada huo.

Rais Kikwete, ambaye alitangaza kuwa angeunda sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha kwenye chaguzi wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, alieleza katika moja ya hotuba zake ataisaini sheria hiyo kwa mbwembwe tofauti na sheria nyingine.

"Sheria nyingine natia saini kimya kimya, lakini hii nitaisaini kwa mbwembwe," alisema Rais Kikwete wakati akifungua mkutano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akihutubia taifa mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kikwete aliweka wazi kwamba sheria hiyo imetungwa kwa nia ya kupata majawabu kwa tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi”.

Licha ya kwamba matukio ya rushwa katika uchaguzi kuwa ni ya muda mrefu, Rais Kikwete alisema yanaimarika siku hadi siku na mbaya zaidi “yanakua kwa kasi ya kutisha na hata kugeuzwa kuwa ndio utaratibu wa kawaida au utamaduni katika chaguzi nchini”.
Tags:

0 comments

Post a Comment