Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA: Kikwete aanza kusafisha njia

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MWENYEKITI wa CCM Rais Jakaya Kikwete, leo anaanza ziara ndefu ya kutembelea na kuimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya shina mkoani Dar es Salaam.

Akiwa katika ziara hiyo inayoonekana kuwa ni kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu; Rais Kikwete atazungumza na viongozi ngazi mbalimbali kuanzia mabalozi wa nyumba kumi hadi juu.

Katika ziara hiyo, RaisKikwete pia amepanga kuwatembelea waathirika wa mabomu Mbagala na kuzungumza nao.

Ziara hiyo ndefu ambayo ni ya kwanza kufanywa na Rais Kikwete tangu aingie Ikulu mwaka 2005, inafanyika wakati CCM ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotishia uhai wake, baadhi yake ni kushamiri kwa makundi ndani ya chama hicho, kitisho cha kumeguka na baadhi ya vigogo wake kukimbilia CCJ.

Uongozi wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam kupitia kwa Katibu wake, Kirumbe Ng'enda, jana ulitoa ratiba ya ziara hiyo inayoonyesha kuwa mwenyekiti huyo wa taifa atakutana na kuzungumza na makundi mbalimbali wakiwemo mabalozi wa nyumba kumi, ambao kwa muundo wa chama, ndiyo nguzo kuu ya ushindi wake katika chaguzi.

CCM imekuwa ikitajwa kutumia zaidi mabalozi wa nyumba kumi kama nguzo kuu ya ushindi wake katika chaguzi, kutokana na wao kuwa karibu wananchi ambao ndiyo wapiga kura. Chama hicho kimekuwa kikiwatumia viongozi hao kama nguzo kuu ya ushindi tangu kuanzishwa kwake, mfumo ambao ulirithiwa kutoka TANU.

Wadadisi wa mambo ya kisiasa wanaichambua ziara hiyo hasa mkakati wake wa kuwafikia viongozi hadi wa mashina na matawi, kama njia moja wapo kuwapanga vema wanachama, ili kuweza kukivusha chama salama katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Ng'enda alipoulizwa kwanini ziara hiyo inaonekana kuwa ndefu kuliko zote zilizowahi kufanywa na Rais Kikwete kama mwenyekiti wa CCM tangu aingie madarakani alijibu: "Kweli ni ndefu, mwenyekiti wetu kama unavyojua ni kiongozi mkuu wa nchi hivyo si rahisi kupata nafasi kila wakati.

"Mara kadhaa ameomba muda mrefu kutembelea chama na kuzungumza na viongozi wote wakiwemo wa mashina, lakini ratiba imekuwa ikimbana. Wakati mwingine akitaka kufanya hivyo, ziara huingiliana na shughuli za kiserikali."

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, leo rais atawasili katika ofisi CCM mkoa kati ya saa 5:30 hadi saa 6:00, kisha msafara wake utaelekea ukumbi wa Karimjee ambako kati ya saa 6:00 na 8:00 mchana atapokea taarifa za kazi za chama mkoa na wilaya zake.

Sehemu ya ratiba hiyo inafafanua kwamba, siku inayofuata Rais Kikwete atakuwa wilaya ya Kiondoni ambako atapokea taarifa fupi na kufungua jengo la CCM la wilaya ambalo jiwe lake la msingi liliwekwa na kisha kusalimiana na wananchi. Jiwe la msingi la jingo hilo liliwekwa na Marehemu Rashid Kawawa.

Ratiba hiyo inaonyesha kwamba, siku hiyo hiyo mwenyekiti huyo atakutana na viongozi wa kata, matawi na mashina katika Ukumbi wa Vijana Kinondoni.

Februari 5 ambayo ni siku yenyewe ya kuzaliwa CCM, Rais ataanza ziara yake kwenye kata ya Sandali na kupokelewa na viongozi na wanachama wa wilaya ya Temeke na kupewa taarifa fupi ya ujenzi wa ofisi ya kata.

Kwenye ratiba hiyo, inaonyeshwa Rais atafungua ofisi mpya ya CCM kata ya sandali na kusalimiana na wanachama na kwenda ofisi ya chama hicho tawi la Mgulani ambako atafungua tawi jipya la Chuo Kikuu -DUCE.

Hata hivyo, King'enda alipoulizwa kuhusu tawi hilo kama liko ndani ya majengo ya chuo, alisema: "Wanafunzi wanapokuwa nje ya chuo wako huru kushiriki siasa, hili tawi haliko katika majengo ya chuo liko nje."

Siku hiyo, ratiba inaonyesha rais atakwenda hadi kata ya Mbagala Kuu ambako atawatembelea wananchi walioathirika na mabomu kutoka kambi ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ). Baada ya hapo atakwenda ukumbi wa PTA (sabasaba) ambako atazungumza na viongozi wa mashina, matawi, Kata, Mabaraza ya Jumuiya na Baraza la Wazee wa chama.

Kwa mujibu wa ratiba, baada ya hapo Rais ataondoka kuelekea kata ya Vingunguti ambako atapokelewa na viongozi wa chama kisha kupokea taarifa fupi ya mradi wa uwekezaji kati ya chama na Kampuni ya Kobil na kuuufungua rasmi.

Rais baada ya hapo msafara wa Rais utakwenda ukumbi wa Korea ambako atafanya mazungumzo na viongozi wa kata, matawi, mashina, Jumuiya na wazee wa chama.

Februari sita, Rais atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo ya miaka 33 ya kuzaliwa CCM, lakini kabla ya hapo ataongoza matembezi ya mshikamano hadi viwanja vya Mnazi mmoja.

King'enda alifafanua kwamba, uamuzi wa kusogeza mbele maadhimisho hadi Jumamosi umelenga kutoa fursa wananchama na wananchi wengine kuhudhuria sherehe hizo kwa kuwa Februari 5, ambayo ni Ijumaa ni siku ya kazi.

Tangu sakata la Richmond liibuke, hasa baada ya kashfa hiyo kufika bungeni na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili walioitumikia Wizara ya Madini na Nishati Wakati wa mchakato wa zabuni hiyo; kumekuwa na mvutano mkali ndani ya CCM ambao umezua makundi mawili makubwa. Moja ni lile linalojulikana kama la wapinga ufisadi na lile la mafisadi.

Mpasuko huu umeifanya CCM kuwa katika hali mbaya, ingawa wenyewe wanasema hali ni shwari. Mvutano huo unajionyesha dhahri miongoni mwa wanachama, hasa baadhi ya viongozi wa chama uliifanya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kuunda kamati maalumu ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, kushughulikia hali hiyo.

Ni kutokana na mvutano huo, baada ya CCJ kuanzishwa, kumekuwa na fununu kuwa baadhi ya vigogo wa CCM hasa wa kundi la wapiganaji wanataka kuingia huo. Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wanadai kuwa hiyo ni janja ya CCM; baada ya kuona hali ni tete ndani wamekiasisi chama hicho (CCJ) kwa lengo la kupima upepo, ili kiweza (CCM) kujipanga vizuri kabla ya uchaguzi mkuu.
Tags:

0 comments

Post a Comment