You Are Here: Home - - Profesa Baregu afukuzwa UDSM kwa madai ya kuelemea CHADEMA
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam kimegoma kumwongezea, Profesa Mwesiga Baregu, mkataba wa kuendelea kufundisha chuoni hapo kwa sababu ameegemea zaidi kwenye siasa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, amesema, kitendo cha Profesa Baregu kugombea na kushikilia nyadhifa kadhaa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesababisha akose sifa ya kuendelea kuwa mtumishi wa umma.
Waziri Ghasia amesema,waraka wa Mkuu wa Utumishi namba moja wa mwaka 2000 unatoa maelekezo kuhusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi na unaelekeza mambo yanayoruhusiwa na yale yasiyoruhusiwa kwa watumishi wa umma.
Ametaja miongoni mwa mambo yasiyoruhusiwa kwa watumishi wa umma kuwa ni kugombea nafasi yoyote chini ya katiba au uongozi wa ngazi yoyote katika chama cha siasa akiwa mtumishi wa umma.
Amevitaja baadhi ya vyeo vya Profesa Baregu kuwa ni mjumbe wa kamati kuu ya taifa ya Chadema baada ya kuchaguliwa na Baraza kuu la chama hicho mwezi Septemba mwaka jana.
“Kwa hiyo Prof. Baregu ni kiongozi wa Chadema na hivyo kukosa sifa ya kuendelea na utumishi wa umma,” amesema Ghasia.
Profesa Baregu alistaafu kazi chuoni hapo Februari 1999,baada ya hapo amekuwa anaajiriwa na chuo hicho kwa mkataba.
Kwa mara ya kwanza aliajiriwa kwa mkataba wa mwaka mmoja mwaka 2003 mara tu mara baada ya kurejea kutoka Harare Zimbabwe alipokuwa akifanya kazi tangu alipostaafu.
Baadaye alipewa mkataba mwingine wa kipindi cha miaka mwili kilichoisha mwaka 2006,aliongezewa tena mkataba mwingine uliokwisha Januari 2008.
Waziri Ghasia alisema jana kuwa, haki ya Profesa Baregu ya kuajiriwa kama ilivyo kwa watumishi wote ilikwisha pale alipostaafu kwa lazima na kwa mujibu wa sheria mwaka 1999.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kwa kuwa Baregu ni kiongozi wa kisiasa ajira yake katika utumishi wa umma ilikuwa sharti ikome kwa mujibu wa kanuni na taratibu za ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa.
Prof Baregu amesema,waraka uliotumika kumkosesha ajira unaenda kinyume na haki za binadamu hivyo anawasiliana na wanasheria wake ili waende kupinga sheria hiyo mahakamani kwa manufaa ya Watanzania wote.
Alisema jana kuwa, anafanya hivyo si kwa kwa kugombea ajira bali anaamini kwamba, kwa kuwa Serikali imekubali mfumo wa vyama vingi inapaswa itambue kuwa vyama vichanga vinahitaji watu makini kwa kutoa michango yao wakiwa na nyadhifa na si kuvikata miguu.
“Hapa sigombei ajira, ninachofanya ni kupinga sheria hii inayoonekana kama ya ubaguzi na inakiuka haki za binadamu kwani imewekwa na watawala,” alisema Prof. Baregu.
Amesema, anafanya hivyo ili taifa lisije likawa na waraka unaopingana na katiba ya nchi.
0 comments