CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ambacho hivi karibuni kupitia Halmashauri Kuu (NEC) yake kiliunda kamati ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, kutafuta suluhu ya mpasuko miongoni mwa wabunge wake, kimeongezewa ukurasa mpya kwa kutangazwa kwa siri za kikao cha Halmashauri kuu (NEC) cha mwaka 1995, kilichopitisha wagombea watatu wa urais.
Siri hiyo ilitangazwa juzi Jumatatu, kwenye kongamano la Miaka 10 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam lililowashirikisha viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na baadhi ya wahadhiri waliotoa kauli kali ambazo zinamgusa moja kwa moja Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, aliyeanza mbio za urais mwaka 1995.
Kwa mujibu wa siri za kikao hicho (NEC-CCM) kilichopitisha majina ya Benjamin Mkapa, Cleopa Msuya na Kikwete ili mmojawapo achaguliwe kuwa mgombea urais wa chama hicho, Mwenyekiti wa kikao, wakati huo Rais Ali Hassan Mwinyi, alizidiwa nguvu kikaoni, akazomewa katika kitendo cha utovu wa maadili kwa baadhi ya wajumbe ambao inadaiwa walikuwa wamehongwa fedha.
Kutokana na Mwinyi kuzidiwa kikaoni baada ya kuibuka zogo wakati akielezea sababu za baadhi ya wagombea kukatwa majina yao, Mwalimu Julius Nyerere alilazimika kuingilia kati, akitoa vitisho dhidi ya waliokuwa na jazba zinazodaiwa kuchochewa na kuhongwa fedha na kuwapo kwa mtandao mahsusi wa vijana.
Siri hizi zilivujishwa Jumatatu na aliyekuwa mjumbe katika NEC hiyo, Joseph Butiku, ambaye sasa ameweka bayana kuwa tatizo la msingi CCM na serikalini ni mtandao ambao amedai umekuwa pingamizi kwa baadhi ya viongozi waadilifu kupewa madaraka.
“Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi Nyerere hakuwa Rais wala Mwenyekiti wa CCM, alikuwa ni Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi). Mtandao umeanzia pale, wengi waliokuwamo serikalini sasa ni sehemu ya mtandao. Wakati ule, niliwafuata wana-CCM wawili mmoja mgombea na mwingine mgawa fedha.
“Nilimfuata huyu mgawa fedha nikamuuliza akakataa kukiri lakini nikamwambia hizi fedha unazogawa kwa nini usiwawezeshe tu vijana kwenye miradi yao na badala yake mnazitumia kupata uongozi…hakuwa na jibu na hadi leo ananikwepa. Mwenzake alikuwa mgombea urais.
“Huyu nilimfuata nikamwambia wenzako wanataka uwe rais lakini tatizo lako unafukuzana sana na mali. Akasema kweli. Alikuwa na fedha nyingi zilizobainika ni kutoka nchi moja. Nikamuuliza hizi fedha zako umemwambia Waziri Mkuu (alikuwa David Msuya). Akasema sikumwambia. Nikamweleza kamwambie na ikibidi uzirejeshe…sijui kama alifanya hivyo.
“Sasa kikaja kikao cha NEC; Rais Mwinyi ndiye anaongoza kikao akiwa Mwenyekiti wa CCM. Akaanza kutaja majina fulani yamekatwa, alitajwa mtu fulani nusu ya kikao wakakataa, wakaanza kuimba jina fulani, kama genge hivi. Mwalimu Nyerere ambaye alialikwa kwenye kikao hicho akaomba kuzungumza.
“Alipokubaliwa akaanza kwa kuuliza maswali matatu kutokana na zogo hilo, kwanza akauliza, ninyi ni wahuni au viongozi? Pili, je, hivi ndivyo mnavyochagua Rais? Tatu, Watanzania kama wangewaona, je, wangeamini kuwa ninyi ni viongozi wao?
“Baada ya maswali hayo, ndipo hali ikatulia. Ilifikia hatua ikawa ni uchaguzi kati ya uchafu unaoshabikiwa na wema, akaonya kama ni hivyo (wanashikilia msimamo) twendeni kwa wananchi. Ninyi piteni huko, nasi tupite huku tuone,” alifichua Butiku huku akipewa ishara na viongozi wenzake wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Warioba pamoja na Brigedia Jenerali mstaafu Hashim Mbita, kuacha kuyarejea matukio hayo bila mafanikio.
“Mniache niseme. Maana huu ndio wakati wake. Siwezi kukaa nayo moyoni na kufa nayo haya,” alisema Butiku na kuendelea; “Sasa haya yaliyojengwa yameanza kuibuka hadharani, Umoja wa Vijana CCM wanagombea majengo (mkataba wa kinyonyaji wa ujenzi, eneo la makao makuu UVCCM Dar es Salaam).
“Nyerere aliacha nchi ikiwa moja. Leo imekuwa nchi ya vipande. Nasema hatuwezi kuishi ndani ya takataka kwa muda mrefu. Wengine wakisema wanafukuzwa kazi. Wengine wanaambiwa walitaka urais. Mtandao katika CCM uondolewe. Mliuleta wenyewe. Mkauondoe, hasa vijana, hamna mzee humo labda Kikwete.
“Mtandao unasema fulani asipate kazi, cheo. Salim (Dk. Salim Ahmed Salim) wewe uko NEC mkaondoe mtandao. Mkishindwa kuuondoa ili sisi tuwe na uhakika wa maisha ya wajukuu zetu, tutavaa migolole na mikwaju mje mtuondoe barabarani.
“Tujitambue kwanza sisi ni Watanzania. Haya makundi…mitandao haina maana. Msaidieni Rais (wanamtandao) acheni majungu. Wezi waliomzunguka kama wapo msaidieni awaondoe. Hatuwezi kuwa na Rais compromised, tutamsaidia kuondokana na majungu. Hatukumchagua Rais awe mtumwa wa wafanyabiashara, wafanyabiashara wamemfanya Rais mtumwa,” alisema Butiku.
Katika mjadala huo, kutokana na wazungumzaji wengi kuonyesha hatari inayozidi kulikabili taifa kwa kutokuwa na miiko ya uongozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Dar es Salaam, Methodius Kilaini, alisema; “Nashukuru kama Taifa tumeanza kutambua kuwa tunatembea bila nguo.” Akimaanisha udhaifu umeanza kuzungumzwa wazi na kutafutiwa ufumbuzi na Watanzania wenyewe.
“Tumeanza kutambua tunatembea bila nguo, mwanzo ilikuwa vigumu kuambiana. Tulikuwa tunatembea bila nguo lakini hatuambiani…vijana endeleeni kupiga kelele (dhidi ya rushwa, ufisadi na dhuluma) zitasikika kuliko hata wazee.
“Nashukuru kusikia mapendekezo ya kurejeshwa Azimio la Arusha hata kama likiwa limekarabatiwa…hatuwezi kubaki kutokuwa na chombo kinachotoa mwongozo kwa viongozi. Siku hizi watu wenye maadili mabovu wanakuwa viongozi na wanaendeleza uchafu wao huo.
“Nyerere alikuwa pia na viongozi wasio na maadili lakini alijaribu kuwarekebisha japokuwa si wote walirekebishika. Alikuwa na wanafunzi wake kwenye uongozi ingawa wengine wamekuwa wanafunzi wabaya.
“Siku hizi, unakuwa na viongozi wabovu serikalini, ukijaribu kuwarekebisha hata hawarekebishiki. Kama fisadi anaingia na ufisadi wake kwenye uongozi basi anauendeleza,” alisema Askofu Kilaini, ambaye mantiki kwenye kauli zake hizo zilidhihirika kuzidisha utulivu wa washiriki kumsikiliza kwa makini zaidi, na kuongeza kuwa; “Tanzania ya leo ndiyo nchi pekee mtu anaingia kama mwekezaji akiwa na dola moja lakini anaondoka na dola milioni moja.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Philip Mangula alishauri Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuanza kutoa mafunzo kwa viongozi kama ilivyo nchini China ambako viongozi wanaoteuliwa au kuchaguliwa hupewa mafunzo ya miezi mitatu ili kujua wajibu wao kwa umma, akisema hiyo ndiyo sehemu muafaka ya kupokezana kile alichoita ‘vijiti.’
Rose-Mary Nyerere mtoto wa Mwalimu Nyerere na aliyewahi kuwa Mbunge alionyeshwa kukerwa na msamiati aliouita wa sasa hivi wa upendeleo kwa tiketi aliyoiita kuwa ni “watoto wa wakubwa” akisema wao walishiriki kukata kuni Jeshi la Kujenga Taifa na shughuli nyingine ngumu akitolea mfano licha ya kuwa na kilo 47 kwa wakati huo, aliweza kubeba mzigo wa kilo 57 akiwa JKT.
Naye, Mwanasheria mahiri Tundu Lisu alisema viongozi wengi wanashindwa kumuenzi Mwalimu Nyerere katika kipengele cha ujasiri, akitoa mifano maeneo ambayo Nyerere alionyesha ujasiri ambayo ni kumkosoa wazi wazi Rais aliyeko madarakani, kumwita Waziri Mkuu aliyeko madarakani muhuni, kupingana na wakoloni kiasi cha kufunguliwa kesi ya uchochezi.
“Siku hizi viongozi wanaogopa gharama za ujasiri tofauti na ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere,” alisema Lisu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya bia Tanzania (TBL) Arnold Kileo alisema: “ CCM imekosa maadili kiasi cha kushindwa kuwanyoshea kidole viongozi wa Serikali wasio na maadili na akashauri haja ya kutathmini mfumo wa elimu nchini na hasa mitaala ambayo hubadilika kulingana na matakwa ya kiongozi aliyepo madarakani.
Mkutano huo wa Mwalimu Nyerere, umekuja wakati hali ya kisiasa nchini ikiwa tete kiasi cha miezi tisa tu kabla ya Uchaguzi Mguu wa mwaka 2010. Maoni ya wengi ni kwamba kuna ombwe katika uongozi wa nchi na ndani ya vyama vya siasa.
Hali hiyo imechochewa zaidi na kuwapo kwa makundi ya wazi wazi ndani ya mfumo yaliyotokana na kuwapo kwa mfululizo wa tuhuma za ufisadi dhidi ya wanasiasa, watendaji serikalini na wafanyabiashara wengine ambao ni viongozi wa juu ndani ya chama tawala. Kipindi hiki pia kimeshuhudia viongozi wa dini wakijitokeza kuikosoa Serikali.
|
0 comments