KAULI ya Rais Jakaya Kikwete kuwa anajiandaa kujibu tuhuma za udhaifu wake katika kufanya maamuzi magumu zilizotolewa kwenye kongamo lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, imewasha moto mpya baada ya waliomtuhumu kueleza bayana kuwa wanasubiri kwa hamu majibu ya kiongozi huyo wa nchi. Mawaziri wa zamani, Matheo Qares na Mussa Nkhangaa, mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Joseph Butiku na makada wengine wa CCM walieleza wasiwasi wao kuhusu utendaji wa Rais Kikwete hasa katika kufanya maamuzi magumu dhidi ya mafisadi wakati wa kongamamo hilo la kuadhimisha miaka 10 tangu kifo cha muasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere. Ilifikia wakati walisema kama Kikwete hatafanya maamuzi magumu kabla ya 2010, basi CCM itafute mwanachama mwingine agombee urais kwa tiketi ya chama hicho, huku wengine wakisema CCM imepoteza hadhi kutokana na kutekwa na matajiri. Lakini Kikwete, ambaye alirejea juzi kutoka ziara ndefu iliyohusisha nchi za Jamaica, Trinidad na Tobago, Cuba na Marekani, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hashangai kuwa watu hao wametoa tuhuma dhidi yake. Kikwete aliwaambia waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akisema: â€Japo bado sijapata taarifa vizuri kuhusu yote yaliyozungumzwa katika kongamano hilo, siwezi kushangazwa sana, lakini ninakwenda kupata taarifa kamili na kujadiliana na wenzangu kisha nitajibu mambo yote yaliyokuwa na maana na yale ambayo hayana maana na yaliyosemwa kwa chuki, tutayapuuza tu.†Tamko hilo la Kikwete halikuachwa lipite na wananchi mbalimbali walioongea na Mwananchi, na hasa watoaji wa tuhuma hizo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, makada hao walisema hawatishwi na uamuzi huo wa rais kwa kuwa ana uhuru wa kusema, huku Nkhangaa akisema atayatafakari majibu ya Rais Kikwete na ikibidi atajibu tena mapigo. "Kumjibu, itategemea 'nature' (aina) ya majibu yake," alisema Nkhangaa ambaye katika kongamano hilo aliweka bayana kuwa CCM sasa imetekwa na wafanyabiashara matajiri na kuachana na sera zake za kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi, ndiyo maana imekuwa vigumu kuwashughulikia mafisadi. Alifafanua kwamba kongamano hilo halikuwa na lengo la kumchafua Rais Kikwete bali watu walitoa maoni yao kulingana na mada iliyokuwa mbele yao ya "Mstakabali wa Taifa". "Mjadala ulikuwa unazungumzia mustakabali wa taifa na wote walitoa maoni yao kulingana na namna wanavyoona na wala hakukuwepo na lengo la kumchafua mtu," alisema Nkhangaa. Matheo Qares, ambaye aliwahi kuwa waziri wa Menejimenti na Utumishi wa Umma, alisema jana kuwa jukumu la kujibu hoja atakazotoa rais ni juu ya viongozi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Alisema katika hali hiyo ya malumbano hana ushauri wowote kwa Rais Kikwete na wala hawezi kutolea maoni kauli yake ya juzi kwa kuwa hilo si juu yake. "Sio juu yangu kumshauri ajibu au asijibu, hii ni juu yake na watu anaodhani wanaweza kumshauri," alisema Qares kwa mkato akirejea kauli ya Rais Kikwete kuwa atakaa na wenzake kuandaa majibu. Hata hivyo, baadaye Qares aliliambia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen kuwa "hoja kwamba rais atajibu tuhuma hizo au la, mimi sijui, mkawaulize kina Butiku wenye hiyo foundation (taasisi) na 'walioorganize (walioandaa)' hiyo forum' (kongamano)". "Mambo aliyozungumza rais mimi hayanihusu, kina Butiku ndio wako katika nafasi nzuri kujibu hoja hiyo mimi sijui hayo," alisema. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa dini wamemshauri Rais Kikwete asijibu shutuma zilizotolewa dhidi yake kwa sababu hazitajenga na badala yake zitachochea zaidi mgawanyiko wa kitaifa. "Mimi naona ni busara zaidi angekaa kimya," alisema katibu mkuu wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT), Leonard Mtaita. "Sizungumzii tu katika suala hili la rais, bali hata viongozi wengine ambao wanalumbana kama malumbano yale ya (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Utawala Bora) Sophia Simba na (Mbunge wa Same Mashariki) Anne Kilango." Alielezea malumbano hayo kuwa yanawachanganya wananchi na yanawagawanya kulingana na pande zinazosigana, jambo ambalo alisema ni hatari kwa umoja wa taifa. Mtaita aliishauri serikali kutumia vyombo vyake katika kutatua matatizo baina yao kwa sababu kuyaweka hadharani, hakujengi bali kunabomoa. Katibu mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila alisema asingependa kuchangia lolote kuhusu tamko la Rais Kikwete, lakini angependa kuona Tanzania inakuwa na amani. Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amesema kauli ya Rais Kikwete imekata mzizi wa fitina kwa kuwa imetoa majibu sahihi kwa tuhuma dhidi yake. “Rais Kikwete jana (juzi) amemaliza kila kitu, sasa mambo yanakwenda. Si mnaona alivyofanya,†alisema Makamba jana alipokuwa akiwatambulisha waliokuwa wanachama wa TLP mkoani Kilimanjaro ambao ni katibu mkuu, Aidani Majawanga na katibu mwenezi Shabani Mtego baada ya kujiunga na CCM. Bila ya kufafanua kauli yake, Makamba aliongeza kusema: â€Ni kweli nitafungwa kama nisipomtetea Rais Kikwete.†Wiki iliyopita Makamba alilazimika kutumia vitabu vitakatifu vya dini za Kiislamu na Kikristo (Msaafu na Biblia) kumtetea Rais Kikwete dhidi ya watu wanaomtuhumu anasita kufanya maamuzi magumu. Miongoni mwa masuala ambayo rais anaonekana kusita kufanya maamuzi magumu ni pamoja na kutowachukulia hatua watu walio chini ya mamlaka yake ambao walitajwa katika maazimio 23 ya Bunge kuwa wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao kwa namna tofauti kwenye kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development LLC. Miongoni mwa watu hao ni mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah wakati watendaji wengine walio chini ya mamlaka yake wameshastaafu kwa mujibu wa sheria bila ya kuwajibishwa. Pia Kikwete anatuhumiwa kutokuwa imara kurejesha nidhamu kwenye chama baada ya makundi yanayopingana kushambuliana waziwazi hadharani, yakituhumiana kwa ufisadi. Badala yake halmashauri kuu ya CCM imeunda kamati ili kuchunguza kutoelewana huko kwa wanachama wake. |
You Are Here: Home - - Majibu ya Kikwete ya tuhuma za uongozi dhaifu yasubiriwa kwa hamu
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments