Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Familia ya Kingunge yakataliwa Machinga Complex

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Familia ya Kingunge yakataliwa Machinga Complex
Na Aziza Athuman

WAFANYABIASHARA ndogondogo jijini Dar es salaam wameikataa Kampuni ya familia ya mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombare Mwiru ya ‘Smart Holdings, kuchukua ushuru katika jengo la Machinga Complex na bodi imeagiza tenda irudiwe kupata kampuni yenye sifa.

Wafanyabiashara hao walifikia hatua hiyo katika mkutano,baada ya kuwa na wasiwasi wa kupoteza mapato na kushindwa kumaliza deni la jengo hilo, kulingana na uzoefu walionao wa kampuni hiyo kutuhumiwa na sifa za kifisadi.

Akisoma risala mmoja wa wafanyabiashara hao, kwa niaba ya mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya wamachinga, Peter Amos alisema kumekuwa na udanganyifu mkubwa wa kutoa tenda na kwamba tenda hiyo, imetolewa kwa maslahi ya watu binafsi.

“Sisi tunaamini haya yote ni maslahi binafsi kwani hata ile kampuni iliyofanya ufisadi katika kituo cha mabasi cha Ubungo, tayari imepewa kazi ya kukusanya mapato katika jengo letu, tunaiambia serikali kuwa hatutakubali uamuzi huo.

“Jengo hili tumejengewa na Rais Jakaya Kikwete, lakini tunatakiwa kurudisha deni, sasa kwa hali kama hii, hatutaweza kumaliza deni wala kujenga Machinga Complex nyingine kama malengo yalivyo,” alisema Amos.

Naye Mbunge wa Ilala, Idd Zungu ambaye ni Mwenyekiti wa bodi wa jengo hilo, alisema bodi haikushirikishwa katika mchakato wa kuchagua tenda hizo na hivyo tenda hiyo, inapaswa kurudiwa.

“Kwa upande wangu hata kama nikiulizwa bado sina kitu cha kujibu kwa kuwa hata vigezo walivyovitumia kuchukua tenda sivifahamu, sisi tunashangaa wakati tunapigana jengo liishe, tayari tenda imetolewa,”alisema Zungu.

Alisema mkandarasi ambaye aliwekwa kutengeneza vizimba anakwenda taratibu na kukwamisha kukamilika kwa jengo hilo.

Afisa Biashara Mkoa wa Dar es salaam, aliyekuja kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Matambo Mhina, alikiri kuwa kuna mapungufu katika utendaji na kuahidi kuyafikisha malalamiko katika mamlaka husika ili yashughulikiwe.

“Mimi sina majibu ya moja kwa moja kwa hali hiyo, lakini nitafikisha kilio chenu kwa wakubwa wangu,”alisema Mhina.

Jengo hilo sasa litachukua watu 6,500 badala ya 10,000 waliotarajiwa kupata nafasi kutokana na sababu za kiufundi.

Tags:

0 comments

Post a Comment