Kuna msemo wa Kiswahili kuwa mtu mzima hatishiwi nyau. Msemo huu unapotumika mara nyingi unataka kutuma ujumbe kwa mtu kuwa mtu mzima hapigwi mikwara ya kitoto. Hata hivyo msemo huu unakosa ukweli mmoja ambao ni dhahiri; paka akibanwa hupigana kama simba. Rafiki yangu mmoja hivi majuzi alijikuta yuko kwenye mapambano na paka wa jirani ambaye aliingia kwenye sebule yake bila kukaribishwa. Kwa vile jamaa yangu hapendi paka basi akaamua kumtolea uvivu kwenye eneo la baraza lililozungukwa kwa uzio wa nyavu nyavu za chuma huku mlango wa sebule ukiwa umefungwa na ule wa kutokea nje ukiwa umefungwa pia.
Mwenyewe aliliita hilo ni pambano la karne. Paka wa watu hakutaka ugomvi na mtu alichotaka yeye ni kuruhusiwa kwenda zake nje. Jamaa akajifanya yeye jasiri akaanza kumtandika paka wa watu mangumi na mateke; paka akalia huku akikimbia kujificha akitafuta mahali pa kutokea. Mwishowe yule paka akaona hana la kufanya isipokuwa kujibu mashambulizi. Nilipopigiwa simu huyo bwana alikuwa amekimbizwa hospitali akiwa anavuja damu baada ya kupata kibano cha nyau. Alipotoka hospitali na kunisimulia kisa hiki nilishindwa kujizuia kuhuzunika bali nilibakia kucheka hadi masikio yakaniuma.
Nikagundua kuwa hata mtu mzima akitishiwa nyau lazima ashtuke kwa maana akijifanya yeye mjanja anaweza kutoka na mikwaruzo na kutolewa nishai na paka. Hata hivyo ninaamini msemo mzuri ni ule usemao (nimeutunga mwenyewe) Simba wa karatasi haungurumi wala hangati. Yawezekana kabisa mtu akamchora simba mkali kabisa akiwa amekenua meno na manyoya yametoka huku macho yake makali yakiangalia kwa hasira lakini akimsimamisha na kumuelekeza hata kwa mtoto mdogo zaidi atakachofanya mtoto huyo ni kuigusa hiyo picha ya simba mkali. Simba wa picha anaweza kutisha wale ambao hawajui vitu vya kuchora au picha (sidhani kama watu hao wapo). Mtu hata hawa na lengo gani akisimama na simba wake wa kuchora kuwatishia watu kinachofanyika watu watadhania ni msanii wa aina fulani ambaye anajaribu kuburudisha watu kwa vikatuni au vikaragosi. Naogopa kuwa mikwara ya Rais Kikwete imekuwa kama picha ya simba mkali asiyeunguruma wala kungata!
0 comments