IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ameonya Muungano usiangaliwe kwa kufananisha Zanzibar na Tanzania Bara kwa kuwa mwisho wake si mzuri.
Alifafanua kuwa Tanzania Bara, wapo Watanzania zaidi ya milioni 42 wakati Zanzibar milioni moja na ushee; watu wa namna hiyo wakiuangalia Muungano huo katika mazingira ya kufanana, itakuwa vigumu.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalumu, Mwanamrisho Abama (Chadema), aliyetaka kufanyike kura ya maoni ili Watanzania wa pande zote za Muungano kuamua kama wanataka Muungano na uwe wa aina gani.
Abama pia alisema Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume, alisema Muungano ni kama koti, likikubana unaweza kuvua na kwa kuwa kuna kero za Muungano, anaona wakati umefika wa kulivua.
Mbunge huyo wa Chadema ambayo ina sera ya kutaka Muungano wa na Serikali tatu, alisema ikiwa Zanzibar watataka kuvunja Muungano, je, Tanzania Bara itakuwa tayari kutoa baraka zake.
Akijibu maswali hayo, Pinda alisema Tanganyika na Zanzibar ni nchi mbili zilizoungana ingawa yapo matatizo ya hapa na pale, kikubwa ni kuendelea kuzungumza.
"Muungano umeleta heshima, mimi napata faraja kuona Wazanzibari wamejenga majengo makubwa Tanzania Bara na wanaishi bila wasiwasi, lakini kama kuna mambo, tuyajadili," alisema.
Kuhusu muda wa kuvunja Muungano, Pinda alisema sasa Watanzania wanazungumza kuhusu Katiba mpya na kuwataka katika mazungumzo hayo kuwa waangalifu kuendelea kuheshimu Muungano unaotambua kuwepo nchi ya Zanzibar, kwa kuwa kuifananisha na Tanzania Bara, mwishowe si mzuri.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alimtaka Pinda aeleze lini watamuondoa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta katika nyumba anayoishi ambayo analipiwa Sh milioni 12 kwa mwezi.
Alisema, Sitta alikuwa akiishi katika nyumba hiyo kwa heshima yake kama Spika, lakini tangu aache nafasi hiyo, ameendelea kuishi katika nyumba hiyo na kutaka Serikali iseme lini atahama na kwenda kuishi na wenzake Kijitonyama.
Pia Mbunge huyo alitaka Sitta, mkewe na msaidizi wake wasisafiri katika daraja la kwanza la ndege kama alivyofanya hivi karibuni alipokwenda India.
Lakini Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisimama na kufafanua kuwa Sitta ni Spika mstaafu na stahiki zake zinagharamiwa na Bunge kama ilivyo kwa maaspika wastaafu akiwemo Pius Msekwa na hivyo anayepaswa kuulizwa si Waziri Mkuu, bali Bunge.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Pinda- Tanzania Bara isifananishwe na Zanzibar
0 comments