Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Ngeleja; Sweden Kuna Kashfa Ya Nishati Yetu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa William Ngeleja leo anawasilisha bajeti ya wizara yake huku kashfa ya nishati yetu ikiwa ni moja ya ajenda ya shirika la Misaada la Kimataifa la Action Aid lenye tawi lake nchini Sweden.


Shirika hili linaishinikiza Serikali ya Sweden kuacha kufadhili kwa kuyapa mitaji ya kuwekeza makampuni yenye kukwepa kodi kama ilivyo kwa kampuni ya Pan African Energy.


Kampuni hii Pan African Energy iliyosajiliwa kwenye visiwa viwili; Mauritius na Jersey inavuna gesi ya Songosongo huku ikiwa imeingia mkataba wa miaka 25 na TANESCO kupitia Shirika la Nishati ina Madini la Taifa TPDC. Ni mkataba wenye kuifanya kampuni hiyo kutokulipa kodi ya faida ya mapato wanayopata kutokana na mauzo ya umeme unaotokana na gesi asilia wanayovuna Songo Songo.


Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid iliyotolewa mwezi Mei mwaka huu, tangu Pan African Energy waanze kuvuna gesi asilia kule Songo Songo mwaka 2004, kampuni hiyo imevuna faida ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 60. Nusu ya faida hiyo ilipatikana mwaka 2009 na kampuni hiyo ilitarajiwa kuongeza uzalishaji. Hivyo, kuvuna zaidi gesi yetu asilia ya Songosongo.


Mpaka kufikia sasa, Pan African Energy imefanikiwa kukwepa kodi inayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 40. Hiki ni kiasi cha fedha kinachotosha kusomesha watoto wa Kitanzania 175,000 ( Laki moja na sabin ina tano elfu) kwa mwaka kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid.


Kwa kifupi tu, ripoti hii inadhihirisha namna ufisadi unavyochangia kutuacha Watanzania tukiwa katika hali ya giza linalotokana na mgawo wa umeme. Tukiwa katika hali ya uzalishaji duni kutokana na uhaba wa nishati ya umeme. Ufisadi umetuletea giza na umasikini.


Kampuni hii ya Pan African Energy inanufaika na ’mkataba wa kifisadi’ usiotanguliza maslahi ya taifa.
Ni wakati sasa wa Waheshimimiwa wabunge wetu ’ kumweka kikaangoni’ Waziri wa Nishati na Madini Mh. William Ngeleja ili atoe maelezo ya kina juu ya kashfa hii ya Pan African Energy.


Na atwambie, ni hatua gani zitachukuliwa na lini kwa wote waliochangia kutufikisha kwenye kashfa hii. Hivyo basi, waliochangia kutufikisha katika giza hili tunalolishuhudia sasa kwa kukosa nishati hii muhimu kwa maana ya umeme.


Kama Mheshimiwa Waziri atashindwa kutoa majibu ya kuridhisha, basi, aombwe akae pembeni kupisha Watanzania wengine wenye uwezo wa kushika Wizara hiyo nyeti kwa taifa.

0 comments

Post a Comment