Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Waziri wa Ujenzi John Magufuli ajiuzulu?

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KUNA taarifa zisizothibitishwa kwamba Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, amejiuzulu wadhifa huo.
Taarifa za kuaminika kutoka serikalini zimepasha kwamba waziri huyo amemuandikia barua Rais Jakaya Kikwete, akimtaarifu uamuzi wake wa kujiuzulu.
Taarifa hizo zimeeleza zaidi kuwa Dk. Magufuli amefikia hatua hiyo baada ya kufadhaishwa na hatua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumuingilia katika utekelezaji wa majukumu ya wizara yake.
Vyanzo vyetu vimefafanua kuwa uamuzi huo umesababishwa zaidi na matukio ya hivi karibuni ya Pinda kukosoa hadharani kasi ya zoezi la bomoabomoa kwenye hifadhi ya barabara lililokuwa likitekelezwa na waziri huyo na kuagiza lisitishwe hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo na Baraza la Mawaziri.
“Ndio amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, lakini bado Rais hajamjibu mpaka sasa,” alisema mtoa taarifa wetu.
Hata hivyo Tanzania Daima ilipowasiliana na Magufuli mwenyewe ili kupata maelezo yake kuhusiana na uamuzi huo, jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana na nyakati fulani kuita bila kupokelewa.
Gazeti hili lilipowasiliana na mmoja wa watendaji wa wizara yake kuhusiana na suala hilo, alisema, “Sina taarifa yoyote kuhusu waziri kuandika barua ya kujiuzulu kwenda kwa Rais…, sijui kwa kweli, isipokuwa leo amefanya uteuzi wa viongozi wa wakala wa ujenzi. Lakini usinitaje tafadhali maana mimi sio msemaji hapa.”
Aidha, taarifa kuhusu kujiuzulu kwa Magufuli jana zilizagaa pia katika mitandao mbalimbali ya mawasiliano ya kompyuta na kuzua mjadala baina ya wadau mbalimbali wa mitandao hiyo kupitia mada moja iliyopewa kichwa cha habari kisemacho “Resignation of Dr Magufuli” (Kujiuzulu kwa Dk. Magufuli).
Hatua ya Pinda kusitisha hadharani zoezi la bomoabomoa ilitajwa kuwa moja ya sababu kuu ya Magufuli kufikia uamuzi huo kwa sababu ya kile kilichoelezwa kuwa amenyimwa uhuru wa kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa utashi na majukumu yaliyopangwa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa kabla ya kuanza kutekeleza bomoabomoa hiyo, Januari 13 mwaka huu Magufuli alitoa ilani kwa wananchi waliojenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba hizo mapema na kwamba wasitegemee kulipwa fidia.
Vyanzo zaidi vya kuaminika kutoka ndani ya serikali vililithibitishia gazeti hili kwamba kabla ya Pinda kusitisha zoezi hilo hadharani, tayari alikuwa ameshamwita waziri huyo takriban mara mbili akimtaka aachane na bomoabomoa hiyo lakini bado waziri huyo aliendelea nayo.
Pinda alitoa agizo la kusitisha zoezi la bomoabomoa hiyo Machi 6 mwaka huu wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Chato (jimboni kwa waziri huyo) ambapo pia alimtaka alisimamie.
Wakati akitoa agizo hilo mbele ya wapiga kura wa Magufuli, Pinda alisema kasi aliyoanza nayo waziri huyo katika wizara yake mpya imeitisha serikali na hivyo aliagiza kusimamishwa kwa zoezi hilo mpaka litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.
“Rais aliona kwenye barabara panalegalega na kumrudisha Magufuli kwenye wizara hiyo, huyu serikalini tunamwita ‘buldoza’ hata hivyo ameanza kwa spidi kubwa na tumwemwagiza asimamishe zoezi hilo mpaka litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri,” alisema Pinda.
Alisema baraza hilo litakaa na kuangalia upya maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya bomoa bomoa na kusema kuwa kabla ya kuruhusu zoezi hilo kuendelea lazima wakubaliane kwanza kwenye Baraza la Mawaziri.
Tags:

0 comments

Post a Comment