Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Hali ya hewa yachafuka tena Arusha. Risasi za moto, mabomu zapigwa kuizima Chadema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa (katikati)
 na Mbunge wa Jimbo la Arusha,
Godbless Lema (kushoto kwake) wakisindikizwa na wafuasi
wa chama hicho kutoka mahakamani jana mjini
Arusha baada ya kutoka kusikiliza kesi yao.
MPAMBANO kati ya Jeshi la Polisi na wafuasi wa Chadema jana umetikisa tena Jiji la Arusha baada ya chombo hicho cha dola kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi kuwatanya mashabiki hao waliokuwa wakimsindikiza ofisini mbunge wao, Godbles Lema, akitokea mahakamani.

Tukio hilo limekuja takribani mwezi mmoja baada ya mpambano mkali kati ya polisi na wafuasi wa chama hicho chenye ngome kubwa ya kisiasa katika Ukanda wa Kaskazini, ambao ulisababisha mauaji ya watu wawili na majeruhi.

Jana mnamo saa 5:30 asubuhi, wakati wafuasi hao walipokuwa wakitokea kwenye Mahakama ya Hakimu Mfawidhi mkoani Arusha kusikiliza kesi inayowakabili viongozi wakuu wa chama hicho, walianza kutembea barabarani wakiwa na mbunge wao huku wakimsindikiza kwa umbali wa kilomita tatu.

Wakiwa na mbunge huyo katika msafara wao, wafuasi hao walitembea kuanzia nje ya Mahakama Kuu na kupitia Barabara ya Uhuru, kisha kuingia Barabara ya Boma mkabala na ofisi za Mkuu ya Mkoa wakielekea kwenye ofisi za mbunge huyo.

Katika msafara huo wa kumsindikiza mbunge wao, wafuasi hao walisikika wakiimba nyimbo mbalimbali kumshutumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakisema, “Waziri mkuu Pinda  kaudanganya umma” pamoja na kumkataa Meya wa Arusha wakisema, “Hatumtaki Meya wa Arusha.”

Hata hivyo, wakati wafuasi hao wakiwa katika barabara ya Boma mkabala na ofisi ya Mkuu wa Mkoa,  polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Zuberi Mwombeji, walifika na magari mawili waliyoyatumia kuyakinga kwa mbele gari la mbunge huyo pamoja na wafuasi wao, kisha kuanza kufyatua risasi za moto hewani na mabomu ya machozi kuwatawanya.

Matumizi hayo ya risasi za moto na mabobu yalifanyika baada ya polisi kuona wafuasi hao walikaidi amri halali, iliyowataka kutawanyika kwa amani.

Katika tukio hilo, kiongozi huyo wa polisi alisikika akiamuru vijana wake akisema, "Pigeni pigeni," ndipo askari hao walianza kufyatua mabomu ya machozi na kurusha risasi za moto hewani.

Rekodi za Mwananchi ziliweza kuthibitisha kwamba, katika tukio hilo ilisikika milio sita ya mabomu ya machozi iliyolenga  kuwatimua wafuasi hao wa Chadema huku  polisi wakitumia magari hayo mawili moja likiwa na namba PT 1844 .

Hali hiyo iliwalazimisha wafanyabiashara waliokuwa karibu na eneo hilo kufunga maduka yao huku ofisi za Manispaa ya Arusha, zikifungwa kwa muda na baadhi ya watu wakionekana wakitoka nje ya ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha kushuhudia huku wengine wakikimbia ovyo.

Raia wa kigeni watimua mbio

Raia mbalimbali wa kigeni walionekana wakitimua mbio nje ya Hoteli ya New Safari iliyopo mkabala na eneo hilo, huku baadhi ya wakazi wakihaha kutafuta maji kwa ajili ya kujinusuru na moshi wa mabomu ya machozi.

Hata hivyo, Lema alifika na baadhi ya wafuasi wa Chadema katika ofisi zake ndani ya jengo la Mkuu wa Wilaya ya Arusha ambako baada ya polisi kutoweka, wafuasi wa chama hicho walisimama nje ya jengo hilo na kuanza kuimba nyimbo za uhuru, huku wakitoa kauli za kulilaani Jeshi la Polisi.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu muda mfupi baada ya vurugu hizo, Lema alilaani polisi kuwasambaratisha wafuasi waliokuwa wakimsindikiza kuelekea ofisini kwake baada ya kutoka mahakamani akidai hapakuwa na ulazima wa kupiga risasi za moto na mabomu ya machozi  kuwatawanya wafuasi hao.

Lema aonya mpasuko mkubwa kutokea

Hata hivyo, Lema alidai endapo viongozi wa Serikali wasipokubali ukweli na kushidwa kuutatua mgogoro wa Arusha huenda wakaiingiza nchi katika machafuko.

Akizungumzia sakata la kauli yake aliyoitoa bungeni hivi karibuni kuwa Waziri Mkuu kuwa aliudanganya umma, Lema alisema watakula sahani moja na kiongozi huyo.

“Nchi itaingia kwenye machafuko yasiyo na ulazima kama Tunisia endapo viongozi wetu serikalini wasipokubali ukweli na kutafuta namna ya kuutatua mgogoro huu,na suala la Waziri Mkuu bado tunakula naye sahani moja,”alisema Lema.    

Polisi wajitetea kutumia mabomu

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Akili Mpwapwa alisema polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kutokana na mazingira ya tukio hilo.

Mpwapwa alifafanua kwamba, baada ya kuona wafuasi hao wakitoka nje ya Mahakama hiyo kwa mfumo wa maandamano huku wakizidi kuongezeka barabarani walizazimika kutumia njia hiyo ili kuwatawanya, lakini akakanusha jeshi hilo kutumia risasi za moto.

Aliweka bayana kwamba, ni uvumi wa mitaani kuwa wao walitumia risasi za moto, huku akisisitiza hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo na iwapo wafuasi hao wangetoka mahakamani hapo kama walivyoingia basi polisi wasingetumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

“Tumelazimika kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi kwa sababu walikua wakitoka mahakamani kwa mfumo wa maandamano huku wakisema, “Peoples Power.”

"Kama wasingetumia mfumo huo kama walivyoingia sisi tusingepiga mabomu, lakini hatukutumia risasi za moto huo ni uvumi tu,”alisisitiza Mpwapwa.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili baadaye jana, zilisema tayari polisi imemfungulia jalada Godbless Lema kwa kuandamana bila kibali.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimetangaza kuanza maandamano kesho ikiwa ni mkakati wake kupinga kupanda bei ya umeme, malipo kwa kampuni  tata ya kufua umeme ya Dowans na kushinikiza uwajibikaji baada ya mlipuko wa mabomu Kambi ya JWTZ, Gongo la Mboto.

Akizungumza nje ya Viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, aliwaambia mamia ya wafuasi wa chama hicho baada ya kesi inayomkabili yeye na wafuasi wengine kuahirishwa, akisema katika maandamano hayo pia watazungumzia mauaji wa Arusha.

"Tunawashukuru sana kwa kuja mahakamani kutuunga mkono. Kama tulivyoahidi, yale maandamano ya nchi nzima yataanza Mwanza kesho kutwa (kesho) na baada ya hapo tutaenda mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa,"alisema Dk Slaa.

 Dk Slaa alisema baada ya kumaliza Mkoa wa Mwanza watakwenda katika mikoa ya Mara, Shinyanga na Kagera huku akibainisha kuwa watakaa Kanda ya Ziwa  kwa siku 10.
Tags:

0 comments

Post a Comment