Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - ‘Watanzania wanataka mgombea binafsi’

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MPANGO wa kujipima kwa kutumia vigezo vya utawala bora Tanzania (APRM) unatarajia kuwasilisha rasimu ya ripoti kwa viongozi wakuu wa Bara la Afrika inayoonyesha kuwa Watanzania wengi wanataka mgombea binafsi.

Ripoti hiyo yenye kurasa 600 imesema, kutotekelezwa kwa uamuzi wa kuruhusu mgombea binafsi, kunanyima haki ya msingi ya mtu kuchagua na kuchaguliwa.

Mratibu wa Tathmini ya Utawala bora wa APRM Tanzania, Severinus Hyera alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa rasimu ya ripoti hiyo inatokana  na utafiti uliofanyika kwa miaka mitatu, tangu mwaka 2007 hadi 2009.

"Katika utafiti huo uliofanywa na wataalamu kupitia maktaba, mtandao na mahojiano kati ya wananchi wa kawaida katika ngazi ya kaya na wasomi wa kada zote,
watanzania wengi wanataka kuwepo kwa mgombea binafsi katika chaguzi," alisema mratibu huyo.

Mratibu alizungumza hayo katika semina kati ya APRM na taasisi za kiraia kutoa mapendekezo ya rasimu hiyo kabla ripoti hiyo haijakabidhiwa katika mkutano wa viongozi wa nchi za umoja wa Afrika.

Alisema wataalamu 110 wa masuala ya utawala bora wenye umri kuanzia miaka 26 walihojiwa katika utafiti huo. Kati yao watu watatu walihojiwa kutoka mikoa 25 ya Tanzania Bara na Zanzibar na watu 35 walihojiwa katika semina maalumu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, mbali na watalaamu hao wengine waliohojiwa katika utafiti huo walitoka katika wilaya mbili za kila mkoa pamoja na vijiji, mitaa, shehia  mbili zilizowakilishwa kwa uwiano sawa wa jinsia.

Huu ni utafiti wa pili unaounga mkono suala la mgombea binafsi nchini baada ya jana katika utafiti wake kampuni ya Synovate kuonyesha asilimia 48 ya watu 2000 waliohojiwa, wanataka mgombea binafsi.


Kwa mujibu wa utafiti huo wa Synovate, wakati asilimia hiyo 48 ikiunga mkono mgombea binafsi, asilimia 25 ya watu waliohojiwa wamekataa mfumo huo na asilimia 27 walisema hawana jibu ya swali hilo.

Tafiti hizo zimetolewa huku leo Mahakama ya Rufaa ikitarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya mgombea binafsi katika rufaa iliyokatwa na serikali kupinga huku ya mahakama kuu.

Mei 5 mwaka 2006 Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa hukumu kuruhusu mgombea binafsi katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila lakini, serikali ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Mtikila alifungua kesi hiyo Februari 17, 2005 akiiomba Mahakama Kuu pamoja na mambo mengine, iamuru kuwepo kwa mgombea binafsi katika chaguzi za Tanzania.

Hukumu ya Mei 5 mwaka 2006 iliyoruhusu mgombea binafsi ilitolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama Kuu Dar es Salaam;  Jaji Kiongozi Mstaafu Amir Manento, Salum Massati (aliyekuwa Jaji Kiongozi na Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa sasa) na Jaji Thomas Mihayo (mstaafu kwa sasa).


Katika kupinga hukumu hiyo serikali ilitoa sababu kadhaa ikiwamo Mahakama Kuu kukosea kisheria kutamka vifungu vya katiba kwa kuwa mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kisheria kusikiliza na kutoa maamuzi katika shauri hilo.

Ilieleza kuwa suala hilo lilikuwa linahusu Katiba na mahakama hiyo haikuwa na uwezo huo na kwamba, hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutengua Katiba ya Jamhuri  au kifungu chochote cha katiba hiyo kwa kuwa ndio msingi na kipimo cha sheria nyingine zote.
Tags:

0 comments

Post a Comment