Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - JK: Mkapa jasiri*NI KWA KUINGIZA NCHI KATIKA MTIHANI:

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter RAIS Jakaya Kikwete amemsifu Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuwa ni jasiri kutokana na maamuzi aliyoyafanya kuiingiza nchi maskini kama Tanzania katika mtihani mzito wa kutekeleza ujenzi wa daraja la Umoja, ambalo limezinduliwa jana.

Akizungumza jana katika uzinduzi rasmi wa daraja la hilo linaloziunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji lililopo katika kijiji cha Mtambaswala, wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Kikwete alisema kwa Rais Mkapa kufanya uamuzi huo mzito, hata utekelezaji wa mradi huo haukuwa rahisi kwa sababu ya umaskini wa nchi hizo.

Kikwete alisema: "Nasema ni uamuzi wa kijasiri kwa sababu mbili. Moja, nchi zote mbili ni maskini tena tupo kundi la nchi maskini sana duniani. Kwa hali hiyo, miradi mikubwa kama huu, hautegemewi kutekelezwa na sisi wenyewe. Lakini alikuwa jasiri kuthubutu kuamua tuutekeleze wenyewe.

“Pili, Mkapa akisaidiana na Joachim Chissano, Rais wa Pili wa Msumbiji walichukua uamuzi huo wakati wao wenyewe wako mwaka wa mwisho wa uongozi wao, jambo ambalo kama wasingekuwa wazalendo wangesita kufanya uamuzi wa aina hiyo na kuwaachia wafanye wanaokuja”.

Alibainisha kwamba, viongozi hao waliongozwa na haja ya kufanya mambo yenye maslahi kwa taifa na watu wake hata kama hawatakuwepo wakati wa utekelezaji na ukamilishaji wake.


Kikwete alisema hayo mbele ya marais wastaafu Mkapa na Alli Hassan Mwinyi, Rais Armando Guebuza wa Msumbiji na wageni wengine waliohudhuria katika hafla hiyo.

Mkapa alipofika katika eneo la uzindizi alilakiwa kwa shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria katika tukio hilo.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 720 limejengwa Kusini mwa Tanzania eneo la Mtambaswala wilaya ya Nanyumbu, Mtwara kuelekea upande wa Kaskazini wa Msumbiji wa jimbo la Gabo Delgado.


Kikwete aliongeza sifa kwa marais hao akisema: "Nafurahi kwamba, kazi tunayoifanya leo (jana), kuzindua Daraja la Umoja ni uthibitisho kuwa tunatimiza ipasavyo wajibu wetu huo wa kihistoria. Daraja hili ni ndoto ya viongozi waasisi wa nchi zetu mbili yaani, hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Samora Machel wa Msumbiji.

"Viongozi wetu waliowafuatia, yaani Joachim Chissano, Rais wa Pili wa Msumbiji na Benjamin Mkapa, Rais wa Tatu wa Tanzania ndiyo waliochukua hatua za dhati za utekelezaji wa ujenzi wa daraja hili. Baada ya kutafuta wafadhili bila ya mafanikio, viongozi hao walifanya uamuzi wa kijasiri wa kutumia fedha zetu wenyewe kujenga daraja hili".

Alisema kukamilika kwa daraja la Umoja ambalo limejengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji kutaimarisha uchumi na kudumisha uhusiano baina ya nchi mbili.

Daraja hilo limejengwa na kampuni ya M/S China Geo Engineering Corporation, iliyopewa mkataba wa ujenzi Oktoba 16, 2005 chini ya mradi wa “Unity Bridge” kwa dola za Marekani 27.5 milioni sawa Sh34 bilioni zilitolewa kwa ushirikiano sawa kati ya serikali ya Tanzania na Msumbiji.

Kikwete alisema daraja hilo ni kichocheo muhimu cha kukuza uchumi na biashara baina ya nchi hizo na ukanda mzima wa Kusini mwa Afrika.

“Ni matumaini yangu kuwa baada ya muda mfupi tutaanza kuona matunda ya daraja hili. Usafiri wa watu utarahisishwa, biashara na uwekezaji vitakua, hivyo maendeleo ya maeneo yanayoguswa na daraja hili yatakua pia,” alisema Kikwete.

Kikwete alisema nchi hizi mbili ziko katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) hivyo kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa programu na miradi ya ukanda wa Mtwara (Mtwara Development Corridor).

Alibainisha kuwa pia itasaidia kuendeleza mambo mengineyo katika Jumuia ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na NEPAD.

“Kwa kuwa na daraja hili sasa nchi zetu hizi mbili lazima ziwe mipango madhubuti yenye lengo na mikakati ya kuchochea kuongezeka kwa biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi katika nchi zetu na eneo lote la SADC linaweza kunufaika na kuwepo kwa daraja hili,” alisema Kikwete.

Alisema wananchi wana wajibu wa kuzitumia vyema fursa zinazotolewa na kuwepo kwa daraja hilo, hasa wa mikoa ya mipakani ya Mtwara na Ruvuma kwa upande wa Tanzania na majimbo ya Cabo Delgado na Niassa upande wa Msumbiji.

“Watu wa Msumbiji na Tanzania wakitumie kiunganishi hiki kukuza biashara baina yao na uwekezaji kati ya nchi zetu. Sisi katika Serikali tunatambua vyema kuwa tunao wajibu wa kuwatengenezea mazingira mazuri yatakayowawezesha kuzitumia fursa zinazoletwa na daraja hili la umoja,” alisema Kikwete.

Rais Kikwete aliwahimiza wahusika kutoka idara za uhamiaji na mamlaka za mapato za nchi hizo mbili kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinaanza mara moja.

Alisema serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na barabara ya uhakika, imeshamalisha mipango ya kupata fedha za kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mangaka kwenda Mtambaswala.

Daraja hilo ambalo lina nguzo 18, tisa za Tanzania na zilizobaki za Msumbiji kama sehemu ya mpaka, ambao kwenda mbele unaunganisha upande wa kaskazini mwa nchi hiyo jirani kuelekea Cape Town, Afrika Kusini Rais Kikwete alisema kama likitunzwa vizuri manufaa yake ni makubwa katika kukuza uchumi wa nchi mbili na watu wake.

Sherehe za uzindizi huo ziliudhuriwa na viongozi wengi wa serikali mbili akiwepo Rais wa Msumbiji Armando Guebuza

Aidha Machi 2002 serikali ya Tanzania na Msumbiji zilitia saini makubaliano kwa madhumuni ya kuweka utaratibu wa kupatikana fedha na nyenzo za ujenzi wa daraja hilo ambalo uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo uliofanyika mwaka 2005 na marais Mkapa wa Tanzania na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji kwa kuweka jiwe la msingi.

Hata hivyo, mbali na mikakati ya ujenzi wa daraja hilo kuanza chini ya Serikali ya awamu ya tatu ya rais Benjamin Mkapa, serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete iliendeleza juhudi hizo kuhakikisha kuwa mradi huo wa kisasa unakamilika kwa ubora na viwango vinavyotakiwa kwa kuongeza fedha zaidi.
Tags:

0 comments

Post a Comment