IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BAADHI ya wafanyabiashara maarufu hapa nchini na makada wa chama kimoja kikubwa cha siasa wanahusishwa katika kashfa ya kutengeneza noti bandia ambazo zimepenyezwa katika mzunguko wa fedha hapa nchini kwa muda mrefu sasa.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili, imezipata kutoka vyanzo vya kuaminika zinabainisha kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakijihusisha kufadhili na kudhamini shughuli mbalimbali kwenye jamii kiasi cha kujizolea umaarufu.
Fedha hizo zinachapishwa na makampuni ambayo yanamilikiwa na baadhi ya wafanyabiashara matajiri (tycoons), ambao faida yake wamekuwa wakiitumia kwa wanasiasa, viongozi wa dini na watendaji wa serikali kila wapatapo nafasi ya kujumuika na makundi hayo.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa noti zinazotengenezwa na wafanyabiashara hao ni zile za sh 5,000 na sh 10,000, ambazo zimekuwa na viwango vya hali ya juu, kiasi cha kumfanya mtumiaji asiweze kubaini kuwa ni bandia.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, mzunguko wa fedha hizo ni mkubwa kiasi cha taasisi zinazojishughulisha na fedha kujikuta zikishindwa kuzizuia, kwa hofu ya kuingia hasara kubwa.
Noti hizo ambazo baadhi yake Tanzania Daima Jumapili imeziona, zinashabihiana kwa kiasi kikubwa na hata baadhi ya wafanyakazi wa benki wamejikuta wakizitumia.
Vituo vya mafuta na mabasi ya abiria ni miongoni mwa sehemu ambazo gazeti hili limebaini kuwa fedha hizo chafu zinatumika kwa kiwango kikubwa, ambapo huchanganywa na nyingine ambazo ni halali.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa baadhi ya vigogo wanaotengeneza fedha hizo wamekuwa wakizitawanya sehemu mbalimbali hapa nchini, huku wakiwapa ‘kamisheni’ mawakala wao wanaozisambaza fedha hizo.
Ili kuzuia matumizi ya fedha hizo kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeamua kuchapisha noti za sh 500, 1,000, 5,000 na 10,000 ikizitumia kampuni za kimataifa za utengenezaji wa fedha hizo.
Oktoba mwaka jana, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, akiwa katika Ofisi Ndogo ya Bunge, jijini Dar es Salaam aliwaambia wanahabari kuwa tayari serikali imeshatoa zabuni ya kuchapisha noti hizo.
Katika mchakato wa kuchuja na kupata kampuni itakayokidhi haja hiyo, Cren Currency ya nchini Sweden ilishinda na kupatiwa zabuni ya kuchapa noti za sh 500, 2,000, 5,000 na 10,000, wakati noti za sh 1,000 pekee zitachapwa na Kampuni ya De-rarue ya nchini Uingereza.
Hadi sasa BoT haijawa tayari kutoa taarifa kuwa ni kiasi gani kitatumika mpaka zoezi hilo litakapofikia kikomo.
Tanzania Daima Jumapili iliwasiliana na kitengo cha mawasiliano cha BoT, juu ya mbinu zinazotumika kudhibiti fedha bandia, ambapo kitengo hicho kimesema utengenezaji wa noti mpya utazingatia alama za usalama (Security features) zitakazoendana na teknolojia ya kisasa.
Ofisa wa kitengo hicho, John Kimaro, alisema wamezingatia zaidi teknolojia ya kisasa ili kuwepo na tofauti kubwa kati ya noti halali na bandia, kwa lengo la kumuwezesha mtu kuzitambua kwa urahisi zaidi.
“Tumezingatia maendeleo ya teknolojia zinazotumiwa na watu wanaotoa noti bandia, sisi tutakuwa juu zaidi na tuna uhakika noti zitakazokuja zitakuwa za viwango vya hali ya juu kiasi cha watu kushindwa kuzitengeneza zinazofanana nazo,” alisema ofisa huyo.
Pamoja na baadhi ya watu wanaomiliki mitambo kukamatwa na Jeshi la Polisi, BoT imesema kuwa haina taarifa ya kuwapo baadhi ya wafanyabiashara wanaomiliki teknolojia hiyo ya kuchapa noti bandia na kutaka taarifa zitolewe haraka kwenye vyombo vya habari.
BoT imeongeza kuwa ipo tayari kushirikiana na vyombo vya dola na wananchi kuwashughulikia wale wote wanaozitengeneza noti bandia kwa kuwa wanahujumu uchumi wa taifa.
Tatizo la uwepo wa noti bandia hivi sasa linaonekana kuwa kubwa zaidi, ambapo Septemba mwaka jana, mkoani Dar es Salaam msikiti mmoja uliopo Mburahati ulipewa msaada wa kiasi cha sh milioni mbili na mfanyabiashara mmoja (jina tunalihifadhi), ambazo baadaye zilibainika kuwa ni bandia.
Katika sakata hilo, mfanyabiashara huyo alidai kuwa fedha hizo alizichukua dukani kwake kwa lengo la kutoa msaada katika msikiti wakati wa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Uwepo wa noti hizo mara kwa mara umekuwa ukiwafanya baadhi ya wafanyabiashara hasa ndogo ndogo kupata hasa mara wabainipo kuwa hawana fedha halali.
“Kwenye maduka huwa naona sh 5,000 na 10,000 zikiwa zimebandikwa na hazitumiki, nikiuliza naambiwa ni feki, wafanyabiashara ndogo wengi hawazijui na inawakata mitaji wajasiriamali ambao mitaji yao ni midogo,” alisema Mwanaidi Hamis, mkazi wa Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, nguvu za Jeshi la Polisi zimekuwa zikigonga mwamba kwani pamoja na misako inayoendelea ya mara kwa mara ikihusisha mbinu shirikishi, bado tatizo hilo linaendelea.
Aprili mwaka jana, mkoani Ruvuma, Abel Mgaya (26), mkazi wa Iringa alikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia zenye thamani ya sh 520,000.
Mei, mwaka jana, jeshi hilo lilimshikilia Marko Sayi (26), mkazi wa Nyahanga, wilayani Kahama kwa kukutwa na vifaa mbalimbali vya kutengenezea noti bandia.
Shaibu Ibrahim alitaja vifaa hivyo kuwa ni karatasi zilizokatwa ili kutengenezea fedha bandia, wino na pamba.
Katika sakata hilo ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amewapa watu mbalimbali kiasi cha sh milioni 2.5, ambazo ni bandia ili wazitumie kununulia mazao na mifugo kutoka kwa wananchi.
Hayo yamekuwa ni baadhi ya matukio yanayotoa picha halisi ya namna ambavyo biashara hii inavyoshamiri siku hata siku, licha ya jeshi hilo kujitapa kuwa linadhibiti hali hiyo na BoT ikitoa matamshi ya kukabiliana na matukio ya namna hiyo.
You Are Here: Home - - Vigogo wahusishwa kufyatua noti bandia
0 comments