IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
UBALOZI wa Tanzania nchini Nigeria unahitaji jumla ya sh bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi na makazi ya kudumu ya balozi na kwamba umekwisha kupatiwa notisi ya kunyang’anywa eneo baada ya kushindwa kuliendeleza.
Hayo yameelezwa na Balozi Msuya Mangachi, mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati alipotembelea ubalozi huo uliopo jijini Abuja juzi jioni kukagua eneo la kiwanja cha ofisi na kisha kuonana na watumishi wa ubalozi huo.
Balozi Mangachi alisema serikali ya nchi hiyo imeipatia Serikali ya Tanzania eneo la kujenga ofisi za ubalozi lenye ukubwa wa mita za mraba 5,294 na eneo jingine la kujenga makazi ya balozi lenye ukubwa wa mita za mraba 2,500 na kwamba tangu mwaka 1995 halijaendelezwa kwa sababu ya kukosa fedha za ujenzi.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imekwisha kutoa dola za Marekani 80,000 kwa ajili ya kujenga uzio ili eneo hilo lisichukuliwe.
Pia alimweleza Waziri Mkuu kuwa maeneo ambayo Tanzania inaweza kunufaika kwa kushirikiana na nchi ya Nigeria ni sekta ya elimu, kilimo, ufugaji samaki wa mapambo (Acqua-culture), biashara, michezo hasa soka na utengenezaji wa filamu.
Akitoa mfano, alisema Serikali ya Afrika Kusini imepata walimu wengi kutoka Nigeria wa masomo ya sayansi na Kiingereza lakini ni baada ya kuwafuata na kuwasaili nchini kwao (Nigeria) ili kubaini uhalisi wa vyuo walivyotoka na uhalali wa vyeti vyao.
Akizungumzia kuhusu fursa za kibiashara na Wanigeria, Balozi Mangachi alisema kuna fursa kubwa ya biashara, kwa sababu wakazi wake hawalimi kwa kiasi kikubwa na kila kitu wanaagiza kutoka nje ya nchi yao, hasa baada ya kugundua wana biashara kubwa ya mafuta.
“Sehemu kubwa ya bidhaa zao zinaagizwa kutoka China na Dubai... wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza kuleta bidhaa zao kwani kutoka Dar es Salaam hadi Lagos ni saa sita kwa ndege na haichukui muda mrefu kama mtu ataamua kusafirisha bidhaa kwa meli kupitia Afrika Kusini,” alisema.
Akijibu hoja hizo, waziri mkuu alisema kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kupata walimu kutoka Nigeria kama ambavyo Afrika Kusini imenufaika kwa sababu Tanzania bado inakabiliwa na uhaba wa walimu, hata katika vyuo vya kufundishia walimu hao.
Kuhusu kilimo, waziri mkuu alisema bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kuinua hadhi ya zao la muhogo ili uweze kupata soko zuri duniani.
Akielezea ufugaji wa samaki, waziri mkuu alikubaliana na ombi la balozi huyo la kutaka Watanzania wahimizwe kufuga samaki aina ya kambale kwenye mabwawa kwa kuwa wana soko kubwa sana nchini Nigeria na kwamba mbali na kuwa kivutio, pia ni chanzo cha uhakika cha kitoweo kwenye familia ambazo zitakuwa zinafuga samaki hao.
You Are Here: Home - - Ubalozi waTanzania wadhalilika Nigeria
0 comments