IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BAADA ya Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa kuibana serikali kuhusu vipengele vilivyoongezwa kinyemela katika muswada uliosaniwa na Rais Jakaya Kikwete kwa mbwembwe wiki iliyopita, taarifa mpya zinasema Rais amefura, akitaka maelezo ya kina ya walioingiza vipengele hivyo.
Tanzania Daima lilipozungumza na mmoja wa wasaidizi wa Rais Kikwete kuhusu sakata hilo jana, alidokeza kwa maneno machache, na kwa msisitizo, akisema: “Rais amefura.”
Msaidizi huyo wa rais alisema kutokana na kasoro hiyo ya kwanza ya aina yake kuwahi kutokea katika historia ya nchi hii, Rais Kikwete ametaka maelezo ya kina ili kubaini waliohusika kuchomeka vipengele hivyo.
Naye Dk Slaa, ambeye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amezidi kuibana serikali akiitaka irejeshe bungeni Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kifungu kilichochomekwa kinyemela kiondolewe.
Alisema hilo ni hitaji la lazima la kisheria; na kwamba serikali isipofanya hivyo katika mkutano ujao wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, itachukuliwa hatua za kisheria. Alitaka waliohusika wawajibishwe.
Dk. Slaa, mmoja wa wabunge wanaosoma sana na wenye upeo mkubwa bungeni, ndiye aliyeibua sakata la kasoro hiyo wiki hii.
Jana alisema: “Naomba serikali ichukue hatua kuwasilisha Miscellaneous Amendment katika mkutano wa 19, yaani Bunge la Aprili, ili kifungu hiki ambacho ni kinyume na demokrasia kiondolewe kwenye Sheria ambayo rais ameisaini, vinginevyo tutachukua hatua za kisheria.
“Kama ilivyoripotiwa na gazeti la Tanzania Daima, Mhe. Spika jana wakati anajibu kwenye taarifa ya saa mbili usiku ya TBC1 ni dhahiri alionyesha kuwa hajasoma na hakuwa ameelewa vizuri kinacholalamikiwa.
“(Kama) Angekuwa amesoma, Spika angekuwa mwangalifu kutamka aliyoyatamka. Mheshimiwa Spika anakiri kulikuwa na mjadala, lakini hakutamka mjadala ulihusu nini na wala hakumnukuu Mwenyekiti wa siku hiyo ambayo alikuwa Mhe. Naibu Spika alitoa maagizo gani.
“Ni hatari kwa viongozi wetu kutoa matamko kwa mambo mazito bila kufanya utafiti angalau mdogo. Mhe. Spika atakubali kuwa kwenye Hansard, hakuna popote ambapo imejadiliwa achilia mbali kukubaliwa kuwa ‘Timu ya Kampeni itathibitishwa na Msajili (kwa
mgombea urais) au Katibu Tawala (kwa mgombea ubunge) au na Mtendaji wa Kata kwa (mgombea udiwani).’ Hii ni dhana mpya kabisa, siyo tu haijajadiliwa wala haikufikiriwa kama Hansard inavyoonyesha.”
Dk. Slaa alitoa kauli hii ya jana wakati akijibu kauli ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye juzi alizungumza kupitia kituo cha Televisheni cha TBCI, akitetea udhaifu huo wa kuchomeka kipengele hicho kiholela.
Dk. Slaa alifafanua kuwa kilichojadiliwa ambacho yeye alishiriki ni hoja aliyoleta Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kutaka kufanyia mabadiliko pendekezo la serikali kwa kifungu cha 7(2).
Alisema katika kifungu hicho, Chenge alitaka makundi ya sanaa yaingizwe baada ya neno voters.
“Hivyo ni vyema naye Spika akiri tu kuwa utaratibu wa kutunga sheria umekiukwa. Haifai kubishana kwa sababu ya kubishana wakati Hansard ndiyo ushahidi wa wazi wa jambo hilo.
“Mimi ndiye namwomba Mwanasheria Mkuu, rafiki na ndugu yangu, aisome vizuri kwa kuwa yeye ndiye hajasoma. Amesema vizuri kututaja ambao tulikuwa na mjadala ukumbini, sasa anionyeshe mahali popote katika mjadala huo ni wapi approving authority ilijadiliwa, na kuwa hiyo approving authority iwe Msajili, DAS na WEO.
“Hivyo, ni ustaarabu tu kukiri kuwa kifungu hiki kimechomekwa na kuwa akubali,” alisema Dk. Slaa.
Hata hivyo, tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema juzi aliliambia gazeti hili kwamba iwapo itabainika kuwa kauli ya Dk. Slaa ni ya kweli, serikali itaomba radhi na kupeleka muswada bungeni kwa ajili ya masahihisho hayo.
Dk. Slaa alidai Rais Kikwete amepotoshwa katika baadhi ya vipengele, kikiwamo kipengele kinachohusu uthitibishwaji wa wajumbe wanaounda timu za kampeni kwa ajili ya wagombea urais, wabunge na udiwani.
Alisema Bunge halikukubaliana kuhusu kipengele hicho, wala hakimo katika kumbukumbu za Bunge; na kwamba kiliongezwa baadaye, kabla ya Rais Kikwete kusaini muswada huo kuwa sheria.
Kifungu kinachodaiwa kuchomekwa ni cha 7 (3), ambacho hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu kidogo cha pili, kinaeleza maana ya timu ya kampeni kuwa ni kundi la watu lililoundwa na mgombea wakati wa zoezi la uteuzi lenye madhumuni ya kumwakilisha au kumsaidia mgombea kwenye kampeni za uchaguzi ambaye amepitishwa kuwania.
“(a) Kwa kesi ya urais watathibitishwa na Msajili, (b) Kwa kesi ya Mbunge watathibishwa na Katibu Tawala wa Wilaya na (c) Kwa kesi ya Diwani watathibitishwa na Katibu Tarafa...,” ilieleza sehemu ya sheria hiyo iliyosainiwa na Rais Kikwete ambayo nakala yake tunayo.
Muswada huo wa sheria ulioasisiwa na Rais Kikwete mwenyewe, ulipitishwa kwa mbinde Februari 12 mjini Dodoma huku ukiibua malumbano makubwa baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema, na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pamoja na wabunge wengine kuhusu vipengele mbalimbali vya muswada huo.
You Are Here: Home - - Dk. Slaa amfurisha Kikwete kuhusu sheria ya Uchaguzi
0 comments